JOSEPH HIZA Na MASHIRIKA YA HABARI
IMEKUWA rasmi sasa kuwa uchaguzi wa urais 2017 utakuwa ni marudio ya mechi kali ya 2013 kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto katika nusu ya kwanza ya uwanja na Raila Odinga na Kalonzo Musyoka katika nusu iliyosalia.
Lakini pia safari hii timu ya Raila, kombaini ya National Super Alliance (NASA) imeongezeka nguvu kwa kupata vifaa vipya vya ushambuliaji; Kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi na Kiongozi wa Chama Cha Mashinani (CCM), ambaye pia ni Gavana wa Bomet, Isaac Ruto.
Kumbuka kombaini ya 2013 ya akina Raila ikijulikana Coalition of Reform and Democratic (CORD) ilihusisha Raila (ODM), Kalonzo (Wiper) na Wetangula (Ford Kenya) ambao bado wamo chini ya mwavuli wa NASA.
Vinara hao watano (Pentagon) wamekubaliana kuja na muundo mpya kama ule uliopendekezwa katika muswada wa Bomas wenye cheo cha waziri mkuu na wasaidizi wake.
Katika hilo, wakati Raila atakuwa Rais huku naibu wake akiwa Kalonzo, Mudavadi akitarajia kuwa Waziri Mkuu Mratibu wa Shughuli za Serikali.
Kadhalika Wetangula anakuwa Naibu Waziri Mkuu wa masuala ya Uchumi na Ruto (Naibu Waziri Mkuu- Utawala na Huduma za Jamii).
Lakini kuna vitu, ambavyo wengi walitaka kufahamu; namna NASA ilivyofikia mwafaka wa kumteua Raila-Kalonzo kwa mara nyingine, siri ya makubaliano ya kugawana madaraka pamoja na kwanini ushirika huo unaamini utawala wa Jubilee utang’oka hiyo Agosti 8.
Mkakati uliosababisha kumpitisha Raila – Kalonzo pamoja na kuwasihi kwanini wanapaswa waridhie badala ya kujitoa, kwa mujibu ya wachambuzi wa mambo ulihusisha watu wenye ushawishi katika kada mbalimbali kuanzia siasa, biashara, wasomi hadi diplomasia.
Ni kwa vile kila kinara hasa kambi za Kalonzo na Mudavadi zilitaka Raila awapishe wao kugombea urais kama walivyowahi kumpisha na kumuunga mkono huko nyuma.
Ukiondoa watu wengine wenye ushawishi kutoka kada tajwa hapo juu, inasemekana Wetangula na Ruto walikuwa nyuma ya Raila na hivyo kuwafanya Kalonzo na Mudavadi kukosa jinsi.
Kwanini Raila? Watetezi wa chaguo hilo wanasema ana ushawishi zaidi katika maeneo mengi ya Kenya kulinganisha na wenzake waliojijenga mahali wanakotoka tu.
Ushahidi ni pamoja na nguvu ya chama chake pamoja na kura za maoni kuonesha yu mtu sahihi zaidi wa kumshinda Rais Uhuru akiwaacha wenzake kwa mbali.
Hali kadhalika ripoti ya kiufundi ya kamati iliyoratibu uteuzi wa mpeperusha bendera wa ushirika wao, ilitoa picha ya mwelekeo wa ugombea wa Raila.
Kwamba kiongozi huyo wa ODM alikuwa akishika nafasi ya juu katika vigezo vinne; nafasi kubwa ya kuvuta mwitikio mkubwa wa kura katika kanda, kupenya maeneo ya ngome za Jubilee, kugeuza ngome za Jubilee kuwa maeneo yenye ushindani mkali na mgombea, ambaye kutokuwapo kwake kutawaumiza wafuasi wengi wa upinzani.
Katika hilo ilielezwa Raila angeongeza mwitikio mkubwa katika maeneo mengi zaidi; kaunti 12 za Kisii, Nyamira, Migori, Kisumu, Busia, Siaya, Taita Taveta, Kilifi, Kwale, Homa Bay, Turkana na Mombasa kulinganisha na wenzake.
Timu iliona pia kwa nguvu yake pekee angekusanya kura milioni 4.6 kati ya milioni 8.2 zilizosajiliwa maeneo hayo.
Raila pia alionekana kuwa na nafasi ya kupenya katika kaunti tisa za Jubilee na kuingiza asilimia 40 ya kura; Kericho, Bomet, Meru, Tharaka Nithi, Nakuru, Uasin Gishu, Laikipia, Isiolo na West Pokot, ambayo yameelezwa maeneo anayoweza kunyaka kura milioni 3.5.
Timu pia iliona Raila anaweza kugeuza ngome za Jubilee na kupata asilimia 50 na kushinda kaunti zenye ushindani mkali kwa asilimia 60.
Na ilihofiwa kutokuwapo kwake kungepunguza asilimia 40 ya kura katika kaunti saba.
Baada ya kuupita mtihani huo mkubwa wa uteuzi wa mgombea urais, ambao ulitishia kuisambaratisha NASA iwapo wasingeafikiana, sasa imejipa matumaini ya ushindi licha ya kuchukua tahadhari kutoshangilia hadi watakaposhinda kweli.
Inaufananisha muungano wao na ule wa mwaka 2002 uliomwingiza madarakani Rais Mwai Kibaki ukimshinda Uhuru aliyewania kupitia kilichokuwa chama tawala cha KANU. Aidha unafanana na Pentagon ya 2007 iliyokaribia kumwingiza Raila madarakani.
Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huo, Raila alitengeneza Pentagon, yaani inayojumuisha vigogo watano kama ilivyo NASA, akiungana na Mudavadi, Naibu Rais wa sasa William Ruto, Joe Nyaga, Najib Balala na Charity Ngilu, ambayo iliwakilisha sehemu kubwa ya maeneo ya Kenya.
Hata hivyo, Kibaki alitangazwa mshindi kitatanishi katika uchaguzi huo kwa tofauti ya kura 230,000 huku chama chake cha PNU kikijipatia viti 43 tu vya ubunge ilhali ODM ikiiongoza na kusomba viti 99 kati ya 208 vya ubunge.
Utata wa kura ukasababisha machafuko yaliyoua watu zaidi ya 1,300,000 na wengine wengi kukosa makazi.
Ukiachana na hilo, waraka wa utafiti umeonesha NASA imejipanga kujipatia kura 9,109,344 dhidi ya kura 7,297,800 za utawala wa Jubilee.
Wamepanga kuhakikisha kunakuwapo mwitikio wa asilimia 85 ya wapiga kura (16,407,144) kati ya wapiga kura 19,302,522 waliojiandikisha.
Kuanzia maeneo ya ngome zake ya jamii za Luhya, Kamba na Luo, NASA imekadiria kwamba itajipatia jumla ya kura milioni 5.6 — 1.7 kutoka Wakamba, milioni 1.7 kutoka Waluo na milioni 2.2 kutoka Waluhya.
Kutoka waraka huo wa kimkakati, Jubilee itapata kura sifuri kutoka jamii ya Luhya na itapata sifuri kutoka jamii za Luo na Kamba.
Kinara wa NASA Pentagon, Musalia Mudavadi anasema wanatarajia kupata kura zaidi ya hizo walizofanya kwa kadirio la chini vile wataendesha kampeni nzito, ambayo haikupata kuonekana kipindi cha wiki chache zijazo.
Alisema wamepanga kupiga hodi nyumba kwa nyumba kuhakikisha wanashinda kura za urais katika raundi ya kwanza.
Kinara mwingine wa Pentagon, Moses Wetang’ula alisema watapenya katika ngome za Jubilee na kujitwalia kura zaidi.
Kwa mujibu wa waraka huo wa kimkakati, wapinzani wana matumaini ya kuongeza idadi ya kura zao kutoka jamii za Maasai (256,118), Kisii (660,000), Somali (660,000), Mijikenda (680,000), Meru (74,000), Turkana (300,000), Teso (124,000) na Kuria (81,000).
Chama hicho kinatarajia kinara mwenza mpya Isaac Ruto kuwapatia kura zisizopungua 205,000 kutoka jamii ya Kalenjin, ambako William Ruto ana nguvu sambamba na kiongozi wa KANU Gideon Moi aliyetangaza atamuunga mkono Uhuru.
Kwa upande mwingine, wadadisi wanakadiria Jubilee itasomba kura milioni 4.8 kutoka ngome zake kuu za jamii ya Kikuyu na Kalenjin. Katika Uchaguzi Mkuu wa 2013, jamii hizo mbili ziliipigia kura Jubilee mtu kwa mtu.
Kutoka kwa Wakikuyu, Jubilee itajitwalia kura zote za wapiga kura 3,035,621 ambao watajitokeza kupiga kura. Na kutoka Kalenjin Jubilee itapata kura 1,845,162.
Waraka unasema kwamba jumla ya wapiga kura waliojiandikisha wa Kikuyu ni milioni 3.5 lakini watakaojitokeza kupiga kura ni milioni tatu tu.
Hali kadhalika, kura za Wakalenjin zinasimama milioni 2.4 kwa mujibu ya wana mikakati wa NASA, lakini ni milioni mbili tu watakaojitokeza siku ya uchaguzi.
Kwa kuongeza kura zao milioni 7.2, NASA inaamini Jubilee itapata kura 64,000 kutoka Maasai, kura 283,000 kutoka Wakisii, kura 440,000 kutoka Wasomali, kura 667,000 kutoka Wameru, kura 128,000 kutoka Waturkana, na 297,000 kutoka Embu.
Katika Kaunti ya Nairobi, NASA inakadiria kura za Kikuyu zinasimama 706,000 ikifuatiwa na Kamba (381,000), Luhya (338,000) na Luo (324,000).
Ukokotoo huo uliofanywa na kundi la wataalamu ulipuuza athari za Jubilee katika maeneo ya Pwani na baadhi ya maeneo ya Mashariki na Magharibi.
Katika kura za Urais mwaka 2013 kwa mujibu wa takwimu rasmi, Rais Uhuru Kenyatta alimshinda Raila Odinga, mgombea mkuu wa upinzani kwa tofauti ya kura 832,887. Kenyatta alipata kura 6,173,433 dhidi ya Raila kura 5,340,546.
“Safari hii, tuko mbele yao katika mchezo huu. Tumefanya hesabu zetu na kuziamini zitatusaidia kweli kweli. Niamini, Agosti 8, tutaiangusha Jubilee,” Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ODM, Junet Mohamed alisema.