32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

SEKRETERIETI YA MAADILI YA UMMA YANZA KUMKAANGA RC DAR

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


SEKRETERIETI ya Maadili ya Viongozi wa Umma, imeanza kazi ya kumkaanga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye anadaiwa kutumia vyeti vya mtu mwingine kujiendeleza kielimu.

Hayo yamebainishwa na Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob na kwamba wakati wowote kiongozi huyo atahojiwa ili kujibu tuhuma hizo dhidi yake.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meya Jacob, alisema kuwa ameandikiwa barua na Sekreterieti ya Maadili ya kumwita.

Alisema kwa sasa jamii ipo kwenye wakati mzuri wa haki kuonekana ikitendeka dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye alidai kwa vielelezo vyote anatambulika kama Daudi Albert Bashite.

“Mtakumbuka kuwa Machi 22, mwaka huu, niliwasilisha mashtaka yangu dhidi ya Daudi Bashite kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kutaka achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kukiuka maadili ya utumishi wa umma na  kukosa sifa ya kuwa kiongozi.

“Mashtaka yangu tume yalikuwa ni kughushi vyeti vya kitaaluma kulikofanywa na RC wa Dar es Salaam, huku akijua fika kuwa vyeti anavyotumia vya taaluma si vyake wala si muhusika na amekiuka sheria za nchi na kutenda jinai.

 “Pia alikula kiapo cha utii na uaminifu mbele ya Mheshimiwa Rais, kwa uhusika wa kughushi ni kosa kubwa sana kisheria, huku akijua fika kuwa Rais alipaswa amwapishe yeye,” alisema Jacob.

Pamoja na hayo, alisema kiongozi huo alijipatia mali kama magari na vinginevyo kinyume na maadili ya viongozi wa umma, ambayo yanataka zawadi zote zinazopokewa zitangazwe hadharani.

“Alikiuka misingi ya utawala bora, haki za binadamu na utawala wa sheria kwa kutuhumu watu ovyo hadharani kuwa walijihusisha na biashara ya madawa ya kulevya kabla ya kukutwa na hatia na kisha wengine kuachiwa huru baada ya kubainika hawakutenda makosa hayo,” alisema.

Meya huyo wa Ubungo alisema kuwa katika shtaka la tano dhidi ya mkuu huyo wa mkoa, ni hatua yake ya uvamizi katika kituo cha kurusha matangazo ya redio na runinga cha Clouds Media jambo ambalo alijua fika kwamba maadili ya viongozi wa umma, hayaruhusu kiongozi kushurutisha au kulazimisha jambo lolote kwa kutumia madaraka yake.

Kutokana na hali hiyo, alisema Aprili 12, mwaka huu alipokea barua kutoka kwa Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Harold Nsekela, akimjulisha kuwa tume hiyo imekubali mashtaka yake dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambayo wameanza kuyafanyia kazi.

“Taarifa hiyo ya Kamishna wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, imetoa mwanga mkubwa kwamba haki ambayo wengi wamekuwa wakiiomba, sasa mwanga umeanza kuonekana.

“Hivyo niwaombe wapenda haki wote popote walipo tushirikiane kwa hili ambalo mkuu wa mkoa amekuwa ni kero jijini Dar es Salaam, tupeane ushirikiano wa kuniongezea vielelezo vingine zaidi ya vile nilivyowasilisha tume, yaani vyeti na nakala nyingine za mali kama nimesahau jambo lolote.

“Mimi mlalamikaji na mashahidi wangu muhimu tupo tayari, mbali na matukio ya utekwaji na upoteaji wa watu, lakini tumeendelea kutaka kuona mwisho wa kero hii jijini Dar es Salaam, hivyo wakati wowote shauri litakapoanza kusikilizwa kwenye Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, tutakuwa mstari wa mbele kutaka haki itendeke,” alisema.

Alisema alikwenda Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) na kuangalia taarifa za kiongozi huyo, lakini hakuna kumbukumbu yoyote iliyopo ambayo inaonyesha kuwa kiongozi huyo alisoma shule ya msingi na sekondari kwa jina analotumia zaidi ya kuwapo kwa taarifa za Daudi Bashite.

“Lakini pia niliwasiliana na walimu wa shule anazodaiwa kusoma, ambao na wenyewe wanamtambua kwa jina la Daudi,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, amewataka walimu wa shule alizosoma kiongozi huyo kuanzia Kolomije hadi vyuo kujiandaa kutoa ushahidi pindi shauri hilo litakapoanza, jambo ambalo linaweza kuwarahisishia majaji wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema lakini pia wenye taarifa mbalimbali zinazomhusu kiongozi huyo wasisite kuwasilisha katika sekretarieti hiyo au ofisini kwake kwa sababu zitaongeza idadi ya mashahidi.

“Mimi niliamua kwenda mbali zaidi kwa ajili ya kumshtaki kutokana na tuhuma zinazomkabili, kuliko kupiga kelele nje huku tukishindwa kuchukua hatua za kisheria, hali iliyosaidia shauri langu kufanyiwa kazi,” alisema Jacob.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles