30.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

JK ATIKISA BUNGE

*Wabunge wamshangilia sauti za ‘tumekumis’ zatawala
*Salma Kikwete aapishwa rasmi kuwa mbunge



Na Fredy Azzah-DODOMA


RAIS Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amelitikisa Bunge huku wabunge wa pande zote mbili wakiweka itikadi zao pembeni kwa muda wa dakika 3:16 kwa kumshangilia kiongozi huyo.


Kikwete ambaye jana alihudhuria kikao cha kwanza cha mkutano wa saba wa Bunge la 11 kwa kumsindikiza mkewe Salma Kikwete,  aliyeapishwa kuwa mbunge baada ya kuteuliwa na Rais Dk. John Magufuli.


Baada ya mama Salma kuapishwa na Spika Job Ndugai kuwa mbunge alisoma taarifa kwa wabunge juu ya miswada iliyopitishwa na Bunge na Rais Dk. John Magufuli kuisaini na kuwa sheria na baada ya hapo alimtambulisha Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kwamba ni mmoja wa wageni waliopo bungeni, hali iliyozua shangwe kutoka kwa wabunge wa pande zote mbili wa CCM na upinzani.

Baadhi ya wabunge hao walisikika wakisema ‘tumekumiss’ tunakukumbuka, rudi, huku wengine wakitaka kanuni zitenguliwe ili aruhusiwe kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge asalimiane nao.


Baada ya shangwe hizo Spika Ndugai alisema. “Kwa makofi haya naomba sasa mumpe, standing ovation (kitendo cha kundi la watu waliokaa kusimama wakipiga makofi kuonyesha heshima ya pekee) mpigieni mkiwa mmesimama,” alisema Ndugai.


Hata baada ya Spika Ndugai kuwataka wabunge hao kukaa, waliendelea kushangilia na waliponyamaza alisema kwa sasa hivi yeye yupo bungeni kwa awamu ya nne na katika miaka yote hiyo hajawahi kuona mgeni aliyepokelewa kwa kushangiliwa kwa kiwango hicho.

Wakati hayo yakiendelea, Spika Ndugai alichombeza kwa kusema. “Inaelekea hata waliommisi pia wapo” maneno yaliyopo kwenye wimbo wa msanii Ney wa Mitego, ambaye hivi karibuni alikamatwa na polisi kwa ajili ya wimbo huo kabla ya Rais Magufuli kuagiza aachiwe.
Wakati hayo yakiendelea, Kikwete aliyekuwa ameketi kwenye Jukwaa la Spika, alikuwa akiwapungia mkono wabunge.
Alipotoka nje ya ukumbi wa Bunge na waandishi wa habari kumtaka atoe neno lolote kwa mapokezi aliyopata, alijibu kwa ufupi. ‘Hamna neno, mimi si mbunge bwana’ kisha akapanda kwenye gari na kuondoka kwenye viwanja hivyo vya Bunge.
Salma alivyoingia 
Awali kabla ya kuapishwa, Salma aliingia bungeni huku akiwa anasindikizwa na kundi la wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),  waliokuwa wakiimba wakati wote kwa kutamka  maneno  “mama, mama, mama” mpaka walipomfikisha eneo la kuapa wakarudi kukaa kwenye viti vyao.
Alivyomaliza kuapa, alikwenda kusalimia na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, pamoja na kwenda kwa upande wa upinzani.
Baada ya kumaliza kusalimiana alikwenda kuketi katika kiti chake alichopangiwa ambacho awali kilikuwa kinakaliwa na aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Simba, ambaye hivi karibuni alifukuzwa uanachama na chama chake.


Pamoja na wabunge wakiwa bado wanamshangilia na alipoketi, Spika Ndugai alisema. “Nilikuwa kwanza nataka nione ni wapi mama atakapo kaa ili nimwone na nimpe nafasi ya kwanza ya kuuliza swali,” alisema.


Katika kipindi cha maswali na majibu Mbunge wa Mtambwe, Khalifa Mohamed Issa (CUF) aliuliza swali la mzingi na baada ya majibu kutolewa, alisimama Mbunge wa Kuteuliwa, Salma Kikwete (CCM) na kuuliza swali dogo la nyongeza.


Katika swali lake, Salma alitaka kujua mpango mahususi wa Serikali wa kuongeza usambazaji wa huduma ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini(TASAF), kwa watu maskini wa Mkoa wa Lindi.


Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema tayari wameshasambaza huduma hiyo kwa asilimi 70 katika Mkoa wa Lindi.


Waziri huyo alisema, hivi sasa imebaki asilimia 30 ambayo ni takribani wakazi 350,000 ambao hawajafikiwa na mpango huo na wanatarajia kuikamilisha katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/18.

Wabunge wachambua kishindo cha JK
Baada ya kipindi cha maswali na majibu, wabunge mbalimbali walizungumzia kilichowafanya kumshangilia  Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, ambapo Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema kutofuatwa kwa sheria mbalimbali ikiwamo ya bajeti na sheria nyinginezo, kumefanya wabunge wamkumbuke kiongozi huyo na kuamua kumshangilia.


“Bajeti haijatekelezwa na kuna pesa zimetumika bila idhini ya Bunge. Kuna pesa zimetumika kununua ndege na kuhamia Dodoma hazikuidhinishwa na Bunge. 
“Kununua ndege ni jambo jema lakini lazima sheria za nchi zifuatwe.  Sheria zinakiukwa waziwazi. Wakuu wa wilaya leo wana ving'ora,” alisema Msigwa.


Kiongozi wa Kambi ya Upinzania Bungeni, Freeman Mbowe, alisema. “Kipindi cha Kikwete wabunge walikuwa huru. Waliweza kwenda nje ya nchi kwenda kujifunza kinachofanyika ughaibuni.


“Sasa hivi nchi imejifungia kutoona wanayofanya wengine, hakuna safari za nje, ndiyo maana alipokuja  leo, watu wamefurahi na kukumbuka aliyokuwa anawafanyia,” alisema Mbowe.


Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo),  alisema uhuru wa kuzungumza wa mawazo na  demokrasia iliyokuwapo wakati wa awamu ya nne, ni moja ya jambo lililofanya wabunge waungane kumshangilia.


Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema Kikwete ameshangiliwa kwa sababu wapo wabunge wengi aliowakuza kisiasa.
“Kuna wabunge wengi aliowakuza, hata mimi binafsi, kipindi cha Kikwete ndiyo nilikuwa kisiasa. Amewagusa wabunge wengi. Kama alivyosema Nay wa Mitego — 'waliommisi  (waliomkumbuka) JK wapo, ndiyo kama wabunge,” alisema

.
Naye Mbunge wa Welezo, Saada Mkuya Salumu (CCM),  alisema Kikwete katika miaka 10 ya uongozi wake, alifanya makubwa sana kwa Tanzania kiuchumi na kuitangaza kimataaifa.


Kwa upande wake Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aesh Hilaly (CCM), alisema. “Kikwete alikuwa kiongozi wetu kwa miaka 10, tulikuwa tumemkumbuka kwa sababu muda mwingi hatujawa naye,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles