NA KOKU DAVID
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) ina jukumu la kuhakikisha mizigo yote inayotolewa bandarini au inayopitia mipakani inalipiwa kodi stahiki kwa mujibu wa sheria.
Nchi nyingi zilizoendelea duniani zimekuwa zikitumia kodi zinazotolewa na wananchi wake kufanya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuwapatia mahitaji mbalimbali ambayo ni muhimu kwa mwanadamu.
Kwa upande wa Tanzania, TRA ndiyo yenye jukumu la kuhakikisha inakusanya kodi kutoka kwa wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuziba mianya yote ya wakwepa kodi.
Katika kuhakikisha inafikia malengo iliyojiwekea, TRA iliamua kutumia njia ya TISS kulipia mizigo yote inayotokea bandarini pamoja na mizigo yote inayopitia mipakani.
Ulipiaji mizigo kwa njia ya TISS ni moja ya mikakati ambayo mamlaka hiyo imejiwekea kwa lengo la kuhakikisha ufanisi wakati wa utoaji wa mizigo bandarini na sehemu zote za mipakani unaongezeka.
Kabla ya mizigo hiyo kulipiwa, hufanyiwa tathmini na ndipo italipiwa kwa kutumia utaratibu huo ambao utasaidia kupunguza changamoto mbalimbali.
Pamoja na mizigo kulipiwa kwa njia ya TISS, TRA ililazimika kufanya maboresho kwa kuongeza muda wa kazi na kuwa masaa 24, badala ya ule muda wa awali, lengo likiwa ni kumwezesha mfanyabiashara kuwahi kulipia mzigo wake baada ya kufanyiwa tathmini.
Kuongezeka kwa muda wa kulipia mizigo ni makubaliano yaliyofikiwa baina ya TRA, Benki Kuu Tanzania (BoT) na taasisi nyingine za fedha ambao kwa pamoja walikubaliana kuwa mfumo wa TISS muda wake uongezwe kutoka muda wa kazi saa 10 hadi saa 2 usiku kwa siku za kawaida, huku siku wa sikukuu utakuwa ukitumika kuanzia saa tatu hadi saa 10 jioni.
Huo ni moja ya mkamkati wa TRA wa kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara wakati wa kutoa mizigo yao bandarini au mipakati.
Maboresho hayo ya malipo kwa njia ya TISS ambayo yanaufanya mfumo kufanya kazi kwa masaa 24 tofauti na muda wa awali, yatamwezesha mfanyabiashara kuwahi kulipia mzigo wake baada ya kufanyiwa tathmini.
Mfumo huo wa TISS katika ulipiaji wa mizigo umekuwa na mafanikio kutokana na kuwa utoaji wa mizigo bandarini umeongezeka.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, anasema chini ya utaratibu huo wafanyabiashara wataweza kulipia mizigo yao hadi saa mbili usiku badala ya saa 10 jioni.
Anasema wamelazimika kufanya maboresho hayo kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara kutoa mizingo yao bandarini na mipakani bila usumbufu wowote.
Utaratibu huo umeweza kupunguza mrundikano wa mizigo bandarini, kuongezeka kwa utoaji wa mizigo bandarini, ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia wafanyabiashara gharama zisizo za lazima.
Katika siku za sikukuu na zile za mapumziko, wafanyabiashara watakaotaka kutoa mizigo yao bandarini au mipakani, baada ya kufanyiwa tathmini watakuwa wakihudumiwa kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa 10 jioni ili kuwawezesha wadau wanaoshughulikiwa mizigo yao kulipa bila ya kuwa na kikwazo chochote au kusubiri siku za kazi.
Hata hivyo, changamoto iliyopo katika matumizi ya mfumo huo ni baadhi ya wadau na benki ambazo bado zinaendelea kufanya kazi zao kwa muda ule wa kawaida uliozoeleka.
Wananchi hasa wafanyabiashara wanatakiwa kutumia fursa hiyo kutoa mizigo yao katika muda huo ulioongezwa kwa kutumia mfumo wa TISS ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima.