27.5 C
Dar es Salaam
Friday, July 1, 2022

WAJASIRIAMALI DAR KUPELEKA BIDHAA DODOMA

Na FERDNANDA MBAMILA


TAASISI na vikundi mbalimbali vinaendelea kuchangamkia fursa zinazojitokeza wakati Tanzania ikielekea kuwa nchi ya viwanda.

Tangu Rais Dk. John Magufuli aeleze nia ya Serikali yake kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, taasisi na vikundi vya wajasiriamali vimejitokeza kuanzisha viwanda mbalimbali ambavyo pia vimeweza kutoa ajira kwa Watanzania.

Kutokana na mabadiliko ya kimaendeleo yaliyofanywa na baadhi ya wajasiriamali wadogo, imekuwa chachu kubwa ya kuwavutia  wajasiriamali wengine  kujiunga  na kufanya kazi pamoja.

Ushirika unaounganisha kata mbili za Temeke (Keko) na Kata ya Chang’ombe jijini Dare s Salaam, zimedhamiria  kuuza samani mkoani Dodoma kwa kipindi  ambacho  bunge  litakuwa limeanza.

Kata hizo mbili ziliungana mara baada ya  kuona kuna umuhimu wa ushirikiano wa kimaendeleo baina yao na pia utaweza  kuwasaidia vijana wajasiriamali na wenye uhitaji wa ajira.

Lengo na dhumuni la taasisi hizo ni  kulitangaza soko la ajira kwa vijana nchini ili waweze  kuamka na kufunguka,  kufanya kazi  kwa malengo na bila kuwa tegemezi, jambo ambalo litawasaidia kufikia lengo la kujikwamua kiuchumi.

Diwani wa Kata ya Temeke, Mohamed Fundi, anasema lengo la kuungana baina ya kata hizo mbili ni kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo ili waweze kukuza biashara zao kutokana na uuzaji wa samani zinazozalishwa hapa hapa nchini.

Bidhaa zinazotarajiwa kwenda kuuzwa mkoani Dodoma ni pamoja na vitanda, makochi (sofa), viti, meza na nyinginezo zinazozalishwa katika viwanda vinavyotengeneza bidhaa za mbao.

Anasema  lengo la kwenda kuuza bidhaa mkoani Dodoma  ni kukuza  biashara na kutanua wigo wa ajira kwa kuwa Dodoma ni mji ambao unakuwa haraka kutokana na azma ya Serikali kuufanya kuwa makao makuu ya nchi.

“Mbali na kuuza bidhaa hizo, utakuwa ni wakati mzuri zaidi kwa Serikali kutoa kipaumbele kwa kuweka msisitizo wa kununua bidhaa za wajasiriamali ili waweze kuinuka kiuchumi,” anasema.

Anasema hatua iliyofanywa na uongozi wa kata hizo mbili ya kuwawezesha vijana wajasiriamali ni kuungana na Serikali kuwajengea mazingira mazuri vijana na wajasiriamali ili waweze kuzalisha na kuuza zaidi.

Fundi anaongeza kuwa katika muunganiko huo, kuna  baadhi ya vijana ambao ni wazoefu katika fani hiyo ambao watakuwa wakufunzi na wakuu wa kuwaongoza  vijana wanaoibukia katika katika fani ya utengenezaji na uuzaji wa samani.

“Kwa vile tulivyojipanga kuhusu jambo hili endapo tutapata  eneo kubwa zaidi la kufanyia biashara, tunatarajia kuweka  kambi mkoani Dodoma ili tuweze kuuza bidhaa  kwa wingi zaidi,” anasema Fundi.

Anasema ubora wa bidhaa za vijana walio katika kikundi hicho ndio  msingi wa biashara yao hiyo ambayo malengo yake ni kuipanua zaidi.

Akielezea ubora wa kazi za vijana hao, anasema vikundi vya pande zote mbili vilifanikiwa kumuuzia mfalme wa Morocco bidhaa alipotembelea Tanzania.

Anasema uamuzi wa kupeleka bidhaa zao Dodoma unapewa kipaumbele kutokana na umuhimu pamoja na ukuaji wa Mji wa Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,419FollowersFollow
544,000SubscribersSubscribe

Latest Articles