25.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 19, 2022

MTAMA ZAO LENYE FURSA NDANI NA NJE YA NCHI

NA PATRICIA KIMELEMETA


LICHA ya Serikali kuwahimiza wakulima kulima mazao ya chakula kwa ajili ya matumizi binafsi na mazao ya biashara kwa ajili ya kuwaongezea kipato, baadhi ya mikoa bado inaendelea kulima mazao ya chakula pekee.

Mikoa hiyo ni pamoja na Pwani, Tanga, Morogoro na mingineyo ambayo bado inaendelea na kilimo cha mazoea cha kutumia jembe la mkono kwa ajili ya kulima mazao ya chakula pekee.

Tatizo hilo limetokana na mila na desturi iliyozoeleka ambapo wakulima hulima kwa ajili ya kutafuta chakula cha familia tu.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk.  Charles Tizeba, ameendelea kuwasisitiza wakulima kuachana na kilimo cha zamani na badala yake kulima kilimo chenye tija kitakachowaondoa kwenye umasikini.

Dk. Tizeba anasema licha ya kulima mazao ya chakula, pia mazao ya biashara ni muhimu kwa ajili ya kukuza uchumi pamoja na kujiongezea kipato cha mkulima mwenyewe na Taifa kwa ujumla.

“Tutaendelea kuwaelimisha wakulima kulima mazao ya chakula na biashara ili yaweze kuwainua kiuchumi, jambo ambalo linaweza kuwaondoa kwenye umasikini,” anasema Tizeba.

Anasema Serikali ni miongoni mwa wateja wa mazao hayo yakiwamo mahindi ambapo katika bajeti ya mwaka  2016/17, wameweza kununua zaidi ya tani 62 za mahindi.

Naye Meneja Mwandamizi wa Shamba la Bucharago lililopo Misenyi mkoani Kagera, Petros Bunzawabaya, anasema zao la mtama ni miongoni mwa mazao ambayo mkulima anaweza kulima kwa ajili ya chakula na biashara.

Anasema mkulima anaweza kupata masoko ndani na nje ya nchi ikiwemo kwenye makampuni yanayotengeneza vileo.

Anasema zao hilo zamani lilionekana ni zao la chakula pekee, lakini kwa sasa ni tofauti kwa sababu mkulima anaweza kupata soko ndani na nje ya nchi au kwenye makampuni yanayotengeneza vileo.

Anasema katika maandalizi yake, zao hilo linaweza kulimwa kwenye sehemu zenye wastani wa joto la chini kiasi cha nyuzi joto 18°C, ili kuweza kuota vizuri na kiasi cha nyuzi joto 25-30°C ili kukua vizuri.

“Zao la mtama zamani lilionekana ni zao la kawaida ambalo wakulima wanaweza kulima kwa ajili ya chakula na si biashara, lakini hali ilivyo sasa ni tofauti ambapo mkulima anaweza kulima na kupata masoko ndani na nje ya nchi,” anasema Bunzawabaya.

Anasema kutokana na hali hiyo, shamba hilo limeingia mkataba na kampuni moja ya kuzalisha kileo ambapo wanahitajika kuwapatia tani 3,000 kwa mwaka za mtama ili kuzalisha kinywaji hicho.

Bunzawabaya anasema lengo ni kuhakikisha kuwa, wakulima wa zao hilo wanapata soko la ndani na nje ya nchi kwa ajili ya  kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kupata fedha kwa za kujikimu na maisha.

“Kuna kampuni tumeingia mkataba nayo ya kuzalisha tani 3,000 kwa mwaka kwa ajili ya kutengeneza bia, jambo ambalo limetufanya kuwahimiza wakulima wetu ili kuzalisha tani hizo ambazo tunaamini zinaweza kutusaidia kupata fedha kwa ajili ya kujikimu na hali ngumu ya maisha,” anasema.

Anasema kampuni hiyo inahitaji tani 9,000 kwa mwaka kwa ajili ya kuzalisha kinywaji hicho, lakini kitendo cha kuwapatia tani hizo kunaweza kuingia mkataba mwingine wa kuongeza uzalishaji wa zao hilo, jambo ambalo linaweza kupanua wigo kwa wateja.

 

Kutokana na hali hiyo, Bunzawabaya anasema kilimo biashara ni mkombozi kwa mkulima kwa sababu fedha zake zinaweza kukusaidia kusomesha watoto, kulea familia na kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo.

 “Kutokana na hali hiyo, wakulima wanapaswa kutumia fursa iliyopo kwa kulima mazao ya biashara ambayo yatawasaidia kuongeza tija na kipato kwenye maisha yao, jambo ambalo linaweza kuwainua kiuchumi na kuondoa kwenye umasikini,” anasema.

Anaongeza kuwa mkakati wa kampuni hiyo ni kuwashawishi wakulima kulima zao hilo kwa ajili ya kujiongezea kipato.

Bunzawabaya anasema kwa miaka mitatu iliyopita, shamba hilo lilikuwa linaendesha mradi wa kilimo cha mahindi, mpunga, maharage na soya.

Anasema katika kipindi hicho, walikuwa wanategemea mvua, hali iliyosababisha uzalishaji kuathiriwa na ukame kwa kiasi kikubwa na mazao mengi kukauka.

“Kabla ya kupata zabuni ya kuzalisha mtama, tulikuwa tunazalisha mahindi, mpunga, maharage na soya, tukitumia kilimo cha kawaida kwa kutegemea mvua za msimu, lakini sasa hivi tumepata zabuni ya kuzalisha mtama tani 3,000, tutalima kwa kutumia mifumo ya kisasa ya umwagiliaji ili kuhakikisha kuwa kiasi hicho tunakipata.

"Kuzalisha tani 3,000 kwa mwaka ni kiwango kikubwa sana ukilinganisha na uwezo wetu, lakini tutajitahidi ili kuhakikisha tunatimiza malengo tuliyokusudia.

“Kwa uwekezaji huu tuliopata kutoka kwenye kampuni hii, kutatusaidia kujikita zaidi kwenye shughuli za kilimo biashara ili kuhakikisha tunapata wateja wengine kutoka ndani na nje ya nchi,” anasema.

Anasema katika maandalizi ya kilimo hicho, mpaka sasa zaidi ya watu 200 wamejitokeza kufanya kazi kwenye shamba hilo, jambo linaloonyesha wazi kuwa wataweza kuzalisha tani 3,000 kwa mwaka kama walivyokubaliana.

Mkurugenzi Mkuu wa Asasi ya Kusaidia Sekta Binafsi ya Kilimo (PASS), Nicomed Bohay, anasema asasi yake itahakikisha kuwa, wakulima wanapata tija kwenye mazao wanayolima ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Anasema kutokana na hali hiyo, watatumia fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo ili kuhakikisha kuwa, wanahamasisha wakulima kulima mazao ya biashara ili waweze kujiongezea kipato.

“Mtama ni miongoni mwa mazao ya kilimo ambayo yanaweza kugeuzwa na kuwa biashara. Hii itawasaidia wakulima kupata fedha mara baada ya kuuza mazao yao kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi, hivyo basi tutahakikisha tunawasimamia wakulima ili waweze kunufaika,” anasema Bohay.

Anasema PASS imeweza kuwasaidia wakulima kupata mikopo kwa riba nafuu ili kuendeleza shughuli zao za kilimo.

Anaongeza kuwa asasi hiyo imeweza kuisaidia Kampuni ya Global Agency ya Dar es Salaam kupata mikopo ya Sh bilioni 2 kutoka benki za kibiashara kw

“Tunapaswa kuwahamasisha wakulima ili wajikite kwenye kilimo cha biashara ambacho kitawainua katika maisha yao, bila ya kufanya hivyo wataendelea na kilimo cha zamani ambacho hakina faida zaidi ya kutumia nguvu nyingi na kipato kidogo,” anasema.

Anasema mkakati wa asasi hiyo ni kuhakikisha wakulima wanapata faida kwenye shughuli zao kilimo, jambo ambalo linaweza kuwaondoa kwenye dimbwi la umasikini.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,234FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles