Na PENDO FUNDISHA-MBEYA
KAMPUNI ya vinywaji baridi kupitia kinywaji chake cha Coca Cola kwanza, imesema itaendelea kuisaidia Serikali kupunguza tatizo la uhaba wa madawati linalozikumba baadhi ya shule za msingi na za sekondari.
Kampuni hiyo, imesema katika mwaka huu wa fedha, imetenga dawati 1,000 kwa shule za msingi na za sekondari mkoani Mbeya.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Basil Gadzios alisema imekuwa ikitoa huduma kwa wanafunzi, watoto, wazee, mashirika na makampuni, hivyo ni vema nao wakarudisha fadhira kwa jamii kupitia misaada mbalimbali.
“Kwetu hawa wote, ni wadau muhimu na nguzo pekee inachokiwezesha kiwanda hiki kuendelea,ni wajibu wetu kurudisha asante kwa jamii kwa kutoa msaada wa vitu mbalimbali hususani madawati,”alisema.
Alisema wanatambua changamoto zilizopo ndani ya jamii na kwamba Serikali peke yake haiwezi kuzitatua.
Alisema mwaka jana, kampuni hiyo ilichangia dawati 500.
Mbali na madawati, pia Kampuni hiyo imesema itaendelea kujenga vituo vya polisi na kuboresha miundobinu ya barabara.