27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

MICHE MILIONI 10 YA KOROSHO KUTOLEWA BURE

Na Mwandishi Wetu-Aliyekuwa Mtwara


FEBRUARI mwaka huu Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), ilianza mpango wa kugawa bure miche ya mikorosho kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CBT, Hassan Jarufu, amewaambia wadau wa korosho kuwa jumla ya miche milioni 10 itasambazwa kwa wakulima wa mikoa mitano inayolima zao hilo ya Lindi, Pwani, Tanga, Mtwara na Ruvuma mwaka huu.

“Tumeanza kugawa bure kwa wakulima miche ya mikorosho. Tutafanya hivyo kwa miaka mitatu mfululizo kwa kila mwaka miche milioni 10.

“Tunataka waitunze mpaka ikue ili hatimaye tuongeze kwa kiasi kikubwa uzalishaji,” alisema Jarufu katika mkutano wa wadau wa korosho uliofanyika Mtwara Februari 28 hadi Machi mosi mwaka huu, ukiwashirikisha pamoja na wajumbe wengine, wakuu wa mikoa ya Lindi, Pwani, Tanga, Mtwara na Ruvuma.

Mjumbe wa Bodi ya CBT, Profesa Peter Masawe, anasema utafiti unaendelea kutazama jinsi ya kuanzisha na kupanua kilimo cha korosho katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Kigoma na baadhi ya maeneo katika Mkoa wa Kilimanjaro hasa yale ya Upareni.

Profesa Masawe, Mtafiti wa kimataifa wa zao la korosho, anasema Tanzania inasimama katika nafasi nzuri ya kuongeza uzalishaji wa korosho ambalo ndilo zao lililobaki pekee lenye mipango endelevu na lenye soko lisiloyumba kwa sasa.

Lakini, mkakati huo wa CBT kugawa bure miche ya korosho kwa wakulima ni endelevu kiasi gani?

“Mkakati huu ni mzuri sana na umetumika katika nchi nyingine kama Ivory Coast kuongeza uzalishaji. Lakini inabidi tuongeze kipengele kinachoendana na anayepokea miche kuhakikisha inatunzwa. Ni muhimu kila anayepewa miche msimu ujao apewe elimu na mkataba wa kuutunza.

Hiyo ni kuhakikisha kuwa miche inayogawiwa bure haitelekezwi.  Mkataba uainishe kuwa mche ukifa bila mkulima kutoa taarifa, basi mkulima husika ataulipia mche huo. Kama atatoa taarifa kwa bwana/bibi shamba wake, basi anaweza kupewa mche mwingine ikithibitika kuwa mche haukufa kwa uzembe,” anasema Profesa Massawe.

Anaoongeza: “Mkakati huu utakuwa ni endelevu na utakuwa kichocheo cha kupanda mikorosho mipya. Halmashauri husika nazo zitalazimika ziandae mpango mkakati wa kuhakikisha agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kupanda mikorosho 5000 kila kijiji linatekelezwa kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania.

Bodi haitazalisha miche ya kutosha nchi nzima bali inachangia uzalishaji huo wa miche. Halmashauri na NGOs nazo zina fursa ya kuchangia uzalishaji miche pia.

Pamba, tumbaku, katani, kahawa, chai na pareto si mazao ambayo yanatajwa tena katika usafirishaji nje ya nchi, wadau wa korosho wanasema sasa zao hilo ndilo mkombozi wa mkulima na nchi.

Kwa mujibu wa Profesa Masawe, korosho za Tanzania zina soko kubwa duniani, zinapendwa kwa kuwa zina ladha nzuri na zinaingia sokoni katika miezi ambayo huko nje kunakuwa tayari kuna uhaba. Na sasa kuna hoja kwamba pamoja na kuziuza nje, Watanzania wahamasishwe kula korosho, ikibidi kwa kampeni kama ile ya uhamasishaji wa utalii wa ndani, ili kupanua soko lake.

Profesa Masawe anasema uhamasishaji wa ulaji korosho si jambo geni.

“Hii ni mbinu ya kibiashara ambayo hata makampuni makubwa ya vinywaji kama vile Pepsi, Cocacola na bia huendesha kampeni za kuhamasisha unywaji wa bidhaa zao.

“Hayo ni matangazo ya kila siku na ya bila kikomo. India ilitumia gharama kubwa sana kuhamasisha ulaji wa korosho nchini humo na sasa ndiyo inayoongoza duniani kwa ulaji wa korosho.

“Wakati tunaelekeza nguvu zetu kuongeza thamani ya korosho, ni lazima twende sambamba na uhamasishaji wa ulaji wa korosho na matumizi mengine ya korosho kama vile siagi ya korosho, tui la kupikia (cashew paste and powder).

“Uhamasishaji huo ni muhimu sana kwa kuwa korosho huuzwa kwa madaraja (kernel grade) yanayozingatia ukubwa na uzito wake.

“Korosho kubwa huuzwa kawa bei ya juu. Korosho ndogo huuzwa kwa bei ya chini kidogo. Korosho zilizokatika huuzwa kwa nusu  bei ambapo zikiongezewa thamani na kuuzwa nchini hupata bei ya juu zaidi.

“Uhamasishaji wa ulaji wa ndani ni muhimu sana ili kuhakikisha madaraja ya korosho ambayo hayanunuliwi kwa kasi katika soko la nje, yanauzwa ndani ya nchi. Mbinu hii hutumika pia nchini Brazil,” anasema.

Lakini ni mambo au uamuzi upi utakaofanya korosho kudumu kuwa zao kubwa la biashara? Ni nini kinacholipambanua zao hilo na mengine yaliyowika huko nyuma lakini sasa yamefifia?

Anajibu Profesa Masawe: “ Kwanza kabisa korosho ni zao ambalo kwa kiwango kikubwa haliathiriki sana na ukame kama mazao mengine. Uzalishaji korosho katika nchi nyingi duniani unashuka kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo ukosefu wa mbegu bora na ukosefu wa kanuni bora za kilimo cha korosho, kukosekana kwa wataalamu bora wa korosho na kukosekana kwa ardhi ya kutosha.

“Tanzania imetoa mbegu bora za korosho 38 na mbegu chotara za korosho 16 na kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kusajili mbegu bora 54 zinazokubalika na kutambuliwa na Taasisi ya Kimataifa ya International Union of Protection of Plant varieties (UPOV). Mbegu hizo zina tija katika uzalishaji na zina ubora wa kipekee barani.

“Tanzania pia ina wataalamu elekezi waliobobea barani Afrika ambao hutoa huduma ya kitaalamu ya zao la korosho,” anasema

Taasisi ya Utafiti Naliendele ni kitovu cha Utafiti wa Korosho Afrika (Centre of Excellency for Cashew in Africa).

Korosho haina lehemu (cholesteral free or zero cholesteral) na walaji wanaogezeka duniani wakati uzalishaji haukui kwa kasi hiyo ya ulaji.

Nchi zinazolima korosho duniani ni zile zile na haziongezeki kwa kuwa hali ya hewa hairuhusu. Nchi kama India maeneo yalimayo korosho yanaendelea kupungua kwa kuwa zao la mpira limechukua nafasi ya korosho na baadhi ya maeneo yamegeuzwa kuwa ya viwanda vya kieletroniki (Jimbo la Kerala; India kusini).

Mti wa mkorosho unakubalika katika kutunza mazingira  na kuzuia mmomonyoko wa ardhi ambao tunashuhudia maeneo mengi nchini.

Tukiongeza thamani mazao yote ya korosho yakiwemo mabibo, maganda ya korosho, mafuta ya korosho (CNSL), na baadhi ya vipande vya korosho vinavyovunjika wakati wa ubaguaji, wabanguaji watapata faida kubwa itakayowawezesha kuwalipa wakulima bei kubwa ya korosho ghafi.”

Ni katika mazingira hayo Wadau wa Korosho wamekutana kuangalia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika Msimu wa Korosho wa 2016/2017 ulioisha hivi karibuni ili kujipanga kwa ajili ya msimu ujao, na kwenda mbele, jinsi gani ya kupunguza adha kwa mkulima.

Itakumbukwa kwamba baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika msimu uliopita ni pamoja na kuweka udhibiti uliosababisha Korosho nyingi kuuzwa kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi Ghalani na hivyo kupunguza matumizi ya Kangomba, kipimo ambacho kwa muda mrefu kimekuwa kikimnyonya mkulima.

Aidha, kwa udhibiti huo, makusanyo ya korosho yaliongezeka kutoka tani 155,244.645 msimu wa 2015/2016 hadi tani 260, 216.148 katika msimu wa 2016/2017. Kwa msimu huu na ujao, nia ni kupandisha zaidi tani za kuuza.

Lakini, pengine kubwa zaidi ni kupanda kwa bei ya korosho kutoka Sh 2,800 msimu wa 2015/2016 hadi Sh 4,000  katika msimu wa 2016/2017, hiyo ikisukumwa zaidi na kuongezeka kwa wanunuzi wa korosho waliosababisha kuwapo kwa ushindani wa bei katika minada hasa wanunuzi kutoka Vietnam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles