27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

WABUNGE WAGEUKA MBOGO DAWA ZA KULEVYA

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM), wamehoji mahali ilipo orodha ya wauza dawa za kulevya aliyokuwa nayo Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Wabunge hao walitoa hoja hiyo bungeni jana walipokuwa wakichangia taarifa ya shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi kwa mwaka 2016/17.

BASHE

Katika mchango wake, Bashe alisema ili vita ya dawa za kulevya iweze kufanikiwa, kuna haja Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amfuate Rais mstaafu Kikwete ili ampe orodha ya wafanyabiashara wa dawa hizo.

“Kama Taifa, tunakabiliwa na mambo matatu makubwa, ambayo ni dawa za kulevya, ushoga na elimu ya ovyo tuliyonayo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alisema anayo orodha ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

“Kwa kuwa alisema anayo, namuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, amfuate Kikwete pale kijijini kwake Msoga ampe hiyo orodha ili waungane na kasi ya Makonda ya kupambana na dawa hizo.

“Hapa tumeshasema tunapambana na dawa za kulevya na wakati huo huo, tunaanzisha ‘sober house’ za kutibu waathirika wa dawa hizo.

“Ningekuwa mimi, ningefunga hizo sober house na atakayefikishwa hospitalini kwa sababu ya dawa za kulevya, ashughulikiwe,” alisema Bashe.

MDEE

Wakati Bashe akisema hayo, Mdee pia alikumbushia juu ya orodha ya wauza dawa hizo aliyowahi kuisema Rais mstaafu Kikwete.

 Katika maelezo yake, alisema anaamini orodha hiyo ipo Ikulu na inatakiwa kuanza kufanyiwa kazi kwa kuwa rais akimaliza muda wake, anaacha nyaraza zinazoweza kutumiwa na rais anayefuata.

“Hapa tusitafute ‘headline’ kwenye vyombo vya habari, lazima tuwe na ‘political will’, tuache usanii, tuache sanaa.

“Kama mheshimiwa rais hawajakwambia, basi ujue kwenye kampeni zako ulichangiwa na hao wauza dawa za kulevya.

“Vita hii inawezekana, Makonda katumwa kwa sababu (William) Lukuvi na Kikwete waliwahi kusema wana orodha ya wauza dawa, kwa hiyo ifanyiwe kazi.

“Nchini sasa tuna njaa, kwa hiyo, mnachotaka kufanya ni kubadili akili za Watanzania kwa hizi mbwembwe zenu.

“Mnasema Wema Sepetu anahusika na dawa za kulevya wakati alizunguka na makamu wa rais kwenye kampeni kwa miezi yote mitatu, ina maana hamkujua kama anafanya biashara ya dawa hizo?” alihoji Mdee.

Pamoja na hayo, mbunge huyo alipingana na kauli ya Rais Dk. John Magufuli, aliyesema jana kwamba kila mhusika wa dawa hizo akamatwe na kuchukuliwa hatua.

Katika maelezo yake, Mdee alisema vita hiyo haiwezi kufanikiwa kwa sababu Serikali haijatenga fedha za kupambana.

MSUKUMA

Kwa upande wake, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), alisema anashangaa kuona Taifa linaifanyia kazi taarifa ya Makonda, wakati mawaziri wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na Charles Kitwanga, wamewahi kusema wana orodha ya watu wanaouza dawa za kulevya na hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Wauza dawa za kulevya wanajulikana na hata walio mstari wa mbele kukamata wenzao wanashinda nao na kuwasafirisha nchi mbalimbali kama Marekani.

“Kwanini vyombo vya ulinzi na usalama visimchunguze Makonda maana anasafiri sana Ulaya, Ufaransa na Dubai, hivi anasafiri kwa mshara upi alionao?

“Tunaambiwa juu ya vita ya kupambana na dawa za kulevya halafu tunawakamata akina Ray C na Chidi Benz wakati hao ni wagonjwa.

“Kama Rais Magufuli amesema kama mkewe Mama Janeth anahusika na dawa za kulevya akamatwe, kwanini Makonda naye asihojiwe kwa sababu amewapangisha watu nyumba wakati wanajihusisha na dawa za kulevya?” alisema Msukuma.

ZITTO

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema Serikali imeshindwa kukiwezesha chombo kilichoundwa na sheria ili kudhibiti biashara na utumiaji wa dawa za kulevya.

Alisema pamoja na hali hiyo, Kamati ya Bunge inayohusika na suala la dawa za kulevya imelalamika kuwa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya wana bajeti finyu na hata hiyo nayo haitolewi na hivyo kusababisha kukosa vitendea kazi, kushindwa kutoa elimu kwa umma.

“Kukosa kwao kwa bajeti sasa wanashindwa kufanya operesheni za ukamataji wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya na kushindwa kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa dawa za kulevya.

“Mheshimiwa Spika, kwa siku kadhaa sasa kuna 'crackdown' (ukamataji mkubwa) ya watumiaji wa madawa ya kulevya ambapo Watanzania kadhaa na wengi wao vijana wametiwa nguvuni na Jeshi la Polisi kwa tuhuma kwamba ni watumiaji wa madawa haya.

“Watuhumiwa hawa inasemekana wameagizwa wataje wananunua wapi madawa wanayotumia kwa kuhojiwa na polisi na wengine kulazwa ndani kwa zaidi ya siku tatu bila kufikishwa mahakamani,” alisema.

Akizungumzia kampeni ya sasa inayoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema: “Ukiona kifaranga kipo juu ya chungu ujue chini kuna mama yake, leo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametamka kuwa vita ile sio ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam bali ni vita ya wote.

“Vita ya wote kuendeshwa na Mkuu wa Mkoa mmoja ni jambo la kushangaza kidogo, lakini halina ubaya kwani lazima awepo wa kubutua kombolera.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles