26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

JANGA JINGINE KWA MBOWE

Mtz Design Sunday.indd

Na OMARY MLEKWA-HAI

MIEZI takribani mitano tangu aondolewe Bilicanas, siku moja tangu Serikali imzuie asiendelee na shughuli za kilimo katika shamba lake, jana tena Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amepewa siku 14 awe amelipa kodi inayokadiriwa kufikia Sh. milioni 13.5 ya hoteli yake ya Aishi iliyoko Machame mkoani Kilimanjaro vinginevyo itafungwa.

Uamuzi huu mpya wa Serikali ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, umekuja ikiwa ni siku moja tu baada ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Gellasius Byakanwa, kutangaza kusitisha shughuli za kilimo katika shamba la Veggies analolimiliki Mbowe kutokana na kile alichosema kuwa lipo ndani ya chanzo cha maji ya Mto Weruweru.

Takribani miezi mitano iliyopita, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilivamia na kutoa vitu vyote katika jengo maarufu la Bilicanas lililopo Mtaa wa Mkwepu na Makunganya, Dar es Salaam.

Jengo hilo lililovunjwa wiki mbili zilizopita lilidaiwa kumilikiwa na familia ya marehemu Aikael Mbowe ambaye ni baba mzazi wa Freeman Mbowe.

Hata hivyo, NHC ilieleza kuchukua uamuzi huo kutokana na mteja wake (Mbowe) kushindwa kulipa kodi ya pango zaidi ya sh bilioni 1.172 ambayo ni malimbikizo tangu miaka ya 1990.

Ingawa Mbowe mwenyewe amepata kusema kuwa jambo hilo limefanywa kwa sababu za kisiasa, lakini alipolifikisha Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Ardhi, kesi yake ilifutwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya kutembelea Hoteli ya Aishi, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Byakanwa, alisema amepata taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa jalmashauri hiyo kuwa Mbowe amekwepa kulipa kodi ya huduma ya biashara kwa takribani miaka mitano iliyopita.

Alisema hali hiyo imesababisha halmashauri kushindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato.

Byakanwa alisema Serikali ya awamu ya tano imelenga kukusanya mapato ili iweze kutekeleza majukumu yake ikiwamo kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, mbunge huyo ambaye ni mmiliki wa hoteli hiyo iliyopo Kijiji cha Nshara, hajawahi kulipa kodi ya huduma licha ya kuandikiwa barua Januri 21, 2016 ya kumtaka kulipa kodi hiyo ambayo hakuijibu.

“Hatuwezi kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani kama kuna wafanyabiashara wakubwa kama huyo wanakwepa kulipa kodi, na tena kwa kipindi chote hicho ameshindwa kuleta hali ya mauzo yake ambayo yataweza kujulikana kiasi anachostahili kulipa kodi.

“Hatufanyi hivi kwa kumwonea mtu, bali ni kwa mujibu wa sheria na endapo mtu atafuata sheria hakuna wa kumfuata, kila mtu ni lazima afuate utaratibu bila kujali cheo alichonacho,” alisema.

Alisema deni hilo lilipwe ndani ya siku 14 na akishindwa atachukua hatua ikiwa ni pamoja na kufunga biashara.

“Ikiwezekana tufafunga biashara hii, kwa kuwa amekuwa na tabia ya kutokujali kama nilivyomwita ofisini kwangu na hakufika na wala kujibu barua, sasa na hili puuzeni tutachukua hatua,” alisema Byakanwa.

“Mnaweza kusema kuwa DC labda anamwonea, mimi nakwenda na vielelezo na hapa pia nina taarifa nyingine kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa hajapeleka taarifa ya mauzo ili aweze kukadiriwa kodi kwa kipindi cha miaka mitano,” alisema mkuu huyo wa wilaya ambaye alikuwa ameambatana na Ofisa Mapato wa Halmashauri ya Hai, David Mlay.

Gazeti hili jana lilimtafuta Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, lakini hakupatikana.

Jana hiyo hiyo MTANZANIA Jumapili lilifanikiwa kuzungumza na dada wa Mbowe aitwae Neel Mbowe, anayesimamia shamba la Veggies, ambaye alisema nyaraka na taratibu zote za umiliki wa shamba hilo anazo kaka yake huyo.

Kuhusu umiliki wa shamba hilo, Neel alisema lilikuwa likimilikiwa na babu yao tangu mwaka 1940 na baadae akampa baba yao, marehemu Aikael Mbowe.

Kwa mujibu wa Neel, walimua kulima katika eneo hilo ambalo lilikuwa pori kwa muda mrefu ili kuongeza ajira kwa vijana wanaolizunguka.

Kuhusu sheria ya mazingira na umiliki wa shamba hilo, alisema anayejua yote hayo ni kaka yake Mbowe.

Juzi Byakanwa alitoa amri ya kusitisha shughuli za kilimo katika shamba hilo lenye ukubwa wa zaidi ya hekari mbili lililoko Kijiji cha Nshara.

Byakanwa alimshutumu Mbowe kwa kufanya uharibifu wa mazingira kwa kuvuna miti ya asili bila kibali cha mkuu wa wilaya kulingana na uamuzi wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) pamoja na kuvuta maji kwa kutumia mashine kinyume na kibali na taratibu za utumiaji wa maji ya mfereji.

“Nasitisha shughuli zote za kilimo zinazofanywa katika eneo hili ambalo ni chanzo cha maji ya Mto Weruweru kuanzia leo (juzi) mpaka pale mamlaka nyingine zitakapojiridhirisha na utapaswa kulipa faini zote kulingana na sheria ya mazingira.

“Pia naliagiza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathmini ya uharibifu wa mazingira katika eneo hili na kuchukua hatua pamoja na kuniletea taarifa walizochukua. Maofisa maliasili wa wilaya wafanye tathmini ya miti iliyokatwa bila kibali na kuleta kiasi cha faini ndani ya siku 14,” alikaririwa Byakanwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles