27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

CCM YAWAOMBA RADHI WATANZANIA

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole

Na AGATHA CHARLES – Dar es Salaam

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewaangukia Watanzania kwa kuomba msamaha kutokana na makosa yaliyojitokeza kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Msamaha huo umeombwa Dar es Salaam juzi usiku na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alipozungumza katika kipindi cha ‘Mada Moto’ kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Channel Ten.

Akiwa katika kipindi hicho ambacho mada ilikuwa ‘Mwaka mmoja wa Serikali ya CCM’, Polepole pamoja na mambo mengine, alizungumzia pia mwelekeo wa CCM kwa miaka 40, itakayodhimishwa Februari 4, kwa kusema kuwa ilifikia hatua baadhi ya wananchi walivunjika moyo kutokana na matendo ya chama hicho.

“Chama Cha Mapinduzi kimejifunza sana katika hii miaka 40, lakini kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015, inawezekana kabisa tumekosea sana na kweli ilifika pahala wananchi walivunjika moyo kwa baadhi ya matendo tuliyoyafanya, na mimi kama kiongozi nabeba dhamana ya wote, watusamehe,” alisema.

Pasipo kufafanua zaidi makosa yaliyojitokeza kabla ya uchaguzi huo na kufikia hatua hiyo ya kuomba msamaha, alisema CCM ni sikivu na kwamba ilisikia pale Watanzania waliposema igeuke.

“CCM ni sikivu, kimesikia pahala ambapo Watanzania walituambia geukeni hapo, na uongozi wa awamu ya tano, chini ya CCM na uongozi wa chama chetu chini ya uenyekti wa Dk. John Magufuli, Makamu wa Mwenyekiti Bara na Zanzibar, Katibu Mkuu Kinana (Abdulrahman), Naibu Katibu Mkuu Bara na Zanzibar na sisi katika sekretarieti na pia vikao vyote vya chama, mkutano mkuu, Halmashauri Kuu, Kamati Kuu walifika wakasema imetosha, hatuwezi kuendelea kutosikiliza sauti za Watanzania. CCM si tu kinapendwa na wanachama, bali na umma wa Watanzania,” alisema Polepole.

Hata hivyo, Polepole katika kipindi hicho alisema baada ya kujitazama ndani ya CCM wameamua kutumia msingi wa kujikosoa, kujisahihisha na kwamba imekuwa desturi ya chama hicho kuja na mageuzi makubwa yanayotazama maeneo matatu.

Polepole aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na mageuzi ya kiuongozi kwa kutaka chama hicho kiwe cha mfano.

“Tunataka kiongozi wa CCM ukimtazama unasema huyu ndiye. Ni mwadilifu, ni mwaminifu, mchapakazi, anapiga vita rushwa, ni mkweli, anaamini katika haki, usawa na mambo yanayofanana na hayo,” alisema na kuongeza:

“Ni mtu ambaye kwa hakika miongoni mwetu ni bora kuliko sisi, huyu ndiye kiongozi wa chama, mzalendo wa kweli anayejiweka yeye nyuma na kuweka wengine mbele. Si mbadhirifu, mnyenyekevu, si mwenye mwenendo usiofaa, hayo ndiyo mageuzi ya CCM.”

Polepole alisema licha ya sifa hizo, hata mtindo wa kiuongozi ni shirikishi unaosikiliza wanachama ili kukirejesha chama kwa wanachama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles