Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
MFUKO wa Pensheni wa PSPF umewapa mafunzo wanasheria mbalimbali katika jiji la Dar es Salaam, baada ya kuhudhuria semina ya siku mbili.
Semina hiyo iliyomalizika jana iliandaliwa kutokana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda la kutaka wanasheria wa mkoa wake wapewe semina ili kuwajengea uwezo wa kutatua kero za wananchi ambao ni wanachama wa mfuko huo.
Katika semina hiyo iliyoanza Januari 3, mwaka huu wanasheria hao walipatiwa ufafanuzi wa kina kuhusu shughuli na majukumu yanayotekelezwa na PSPF.
Akizungumzia semina hiyo Meneja wa PSPF Huduma kwa Wateja, Leila Magimbi, alisema majukumu yao ni pamoja na kutambua na kusajili wanachama wapya, michango na kutunza taarifa za michango hiyo.
“Shughuli nyingine zinazotekelezwa na PSPF ni kulipa mafao kwa wanaostahili kwa mujibu wa sheria, kutunza kumbukumbu za wanachama na wastaafu, kuangalia upya ubora wa mafao na kufanya tathmini ya mfuko na kuweka mikakati endelevu,” alisema Magimbi.
Pia wanasheria hao walipata fursa ya kuelezwa aina za wanachama wa PSPF ambao ni watumishi wa umma, sekta binafsi ambao hawatachangia katika mfumo wa uchangiaji wa lazima na watu wote walio katika sekta isiyo rasmi, ambao wao watachangia katika mfumo wa uchangiaji wa hiari.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mafao, Haji Moshi alitaja mafao wanayotoa ni pamoja na fao la uzazi, mkopo wa elimu, mkopo kwa mwajiriwa mpya, mikopo ya viwanja, mikopo ya nyumba, mkopo wa fedha taslimu, mikopo kwa wastaafu yenye masharti nafuu, mafao ya muda mrefu, fao la ulemavu, fao la mirathi, fao la kufukuzwa au kuachishwa kazi pamoja na bima ya afya.