NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
MBUNGE wa Ilala, Mussa Zungu (CCM), amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akipatiwa matibabu baada ya kupata tatizo la shinikizo la damu.
Zungu alifikishwa hospitalini hapo juzi jioni akitokea Hospitali ya Amana ambako alipatiwa matibabu ya awali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Zungu alisema anamshukuru Mungu sasa hali yake inaendelea vizuri.
“Hali yangu ilikuwa mbaya, nilianza kujisikia vibaya saa 8:30 mchana juzi nikiwa nyumbani, ikabidi wanipeleke Amana. Walininipatia huduma na saa 12.00 walinihamishia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
“Nilipokelewa pale ‘emergence’, baadaye nikahamishiwa JKCI. Waliponipima waligundua ‘pressure’ yangu ipo juu… kazi zetu zina msongo wa mawazo mengi ndiyo maana ilipanda ghafla,” alisema.
Aliwashukuru madaktari wote waliomhudumia na kuwakumbusha watanzania kupima afya zao mara kwa mara.
“Nawahimiza pia kukata bima ya afya maana ndiyo iliyoweza kunisaidia kupata huduma bora na wao waone umuhimu huo,” alisisitiza.
Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema bado wanaendelea kuchunguza afya ya mbunge huyo kujua tatizo gani hasa lililosababisha shinikizo la damu kuwa juu.
“Taasisi yetu inatibu watu wanaougua magonjwa ya moyo, siwezi kusema moja kwa moja iwapo Zungu ana tatizo la moyo, tunachunguza kujua sababu za shinikizo lake kupanda,” alisema.
Alisema wana imani kwamba hadi kufikia wiki ijayo watamruhusu kurejea nyumbani kuendelea na shughuli zake za kila siku.
“Nasema hivi kwa sababu hali aliyokuja nayo ni tofauti na alivyo sasa, hadi nyie (waandishi) ameweza kuzungumza nanyi.
“Jambo ambalo Watanzania wanapaswa kutambua mtu yeyote aliyeanzishiwa dozi ya matatizo haya ya ‘pressure’ anapaswa kuzitumia katika kipindi chote cha maisha yake hapa duniani.
“Tunapata wagonjwa wengi ambao tuliwagundua kuwa na tatizo hili walipoanza dawa na kuona wanaendelea vizuri wakaacha leo hii wanarudi wakiwa wagonjwa zaidi, wakumbuke kuacha kutumia dawa ni makosa makubwa,” alisema.