Na WAANDISHI WETU- DAR ES SALAAM
KIPA tegemeo wa timu ya Medeama ya Ghana, Daniel Agyei, ametua nchini kumalizana na vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ili aweze kusajiliwa dirisha dogo na kuimarisha kikosi hicho katika mzunguko wa pili.
Kipa huyo aliyewasili jijini Dar es Salaam jana akitokea nchini Ghana, ataungana na makipa wengine wa Simba, Vincent Angban na Peter Manyika Jr, ikiwa atasaini mkataba wake na kumalizana na Wekundu hao wa Msimbazi.
Agyei ambaye alikuwa kipa namba moja wa kikosi cha Medeama ya Ghana, anatarajia kumalizana na uongozi wa Simba muda wowote ili kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba imejipanga kuanza duru ya pili ya ligi kuu ikiwa na safu imara ya ulinzi, kwani kabla ya kumleta kipa huyo tayari walikuwa wamemalizana na beki wao wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwa kumuongezea mkataba wa miaka miwili.
Wakati Simba wakiimarisha safu ya ulinzi, mahasimu wao Yanga wameimarisha eneo la kiungo baada ya kumsainisha mkataba wa miaka miwili kiungo mkabaji wa zamani wa klabu ya Zesco United ya Zambia, Justine Zulu.
Zulu aliyetua nchini juzi kimya kimya, amesajiliwa kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili katika klabu ya Zesco United.
Usajili wa Zulu ni wa kwanza kwa mabingwa hao watetezi wa ligi kuu katika dirisha dogo na umefanyika siku chache baada ya kutambulishwa kwa kocha mpya, Mzambia George Lwandamina, aliyerithi mikoba ya Mholanzi Hans van der Pluijm.
Pluijm aliyeipa Yanga ubingwa wa ligi kuu kwa mara mbili mfululizo, amepewa majukumu ya kuwa Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi la timu hiyo.
Yanga imefikia uamuzi wa kumsajili Zulu, baada ya juhudi za kumnasa kiungo mwingine wa Zesco United, Meshack Chaila, kugonga mwamba.
Wakati huo huo, mshambuliaji Amissi Tambwe wa Yanga, amesema hana haraka ya kuongeza mkataba na klabu yake hiyo hadi muda mwafaka utakapofika.
“Kwa sasa siwezi kuzungumzia suala la mkataba kwa sababu sina haraka, hivyo taarifa zilizoenea kuwa nimesaini mkataba mwingine, hazina ukweli wowote,” alisema Tambwe.