24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru waanza kutoa ushahidi kesi ya vigogo TFF

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam

OFISA Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sosthenes Kibwengo, amedai vigogo wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waliomba rushwa ya Sh milioni 25 ili wagawane na vigogo wenzao.

Mgao ulikuwa wa makundi matatu, kundi la kwanza Sekretarieti ya TFF Sh milioni 10, Uhamiaji Sh milioni tano na Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji Sh milioni 10.

Kibwengo alidai hayo jana alipokuwa akitoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Leonard Swai.

Vigogo hao wa TFF wanaotuhumiwa kuomba rushwa kwa viongozi wa Klabu ya Mpira wa Miguu Geita, ni Msaidizi wa Rais wa TFF, Juma Matandika na Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho hilo, Martin Chacha.

Shahidi alidai Februari 4, mwaka huu, Salum Kulunge na Costantine Morandi ambao ni viongozi kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita na Klabu ya Mpira wa Miguu Geita, walifika TFF kwa ajili ya kusikiliza rufaa ya mchezaji Mohammed Jingu wa timu ya Polisi Tabora, ambaye aliwekewa pingamizi kuwa si raia wa Tanzania, hivyo usajili wake ni batili.

“Viongozi hao walifuatilia kwa sababu Geita ililingana pointi na Polisi Tabora katika kundi C, walifuatilia kwa sababu uamuzi ungekuwa mbaya kwa Jingu wao wangefaidika kwa timu yao kupanda daraja.

“Februari 4, walikutana na washtakiwa ambao waliomba rushwa ya Sh milioni 25 ili iwe kishawishi cha kutoa uamuzi kwa faida yao, viongozi hao wa Geita walirekodi mazungumzo yote.

“Sh milioni 25 zilizoombwa zilikuwa zigawanywe katika makundi matatu, kundi la kwanza Sekretarieti ya TFF Sh milioni 10, Uhamiaji Sh milioni tano na Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji Sh milioni 10,” alidai.

Ofisa huyo alidai kuwa, walipofanya uchunguzi walipeleka ‘tape’ kwa Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, kwa ajili ya kuisikiliza na kutambua sauti na katibu huyo alizitambua sauti za washtakiwa.

Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, walidai wana mashahidi 10 na vielelezo ikiwemo hiyo ‘tape’.

Upande wa utetezi, ulidai una mashahidi wanne, mahakama iliahirisha kesi hadi Desemba 5, mwaka huu.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanakabiliwa na kosa moja la kuomba rushwa kinyume na sheria ya kuzuia rushwa.

Wanadaiwa Februari 4, mwaka huu makao makuu ya TFF wakiwa waajiriwa wa TFF, waliomba rushwa ya Sh milioni 25 kutoka kwa Salum Kulunge na Constantine Morandi kama kishawishi kwa TFF na Idara ya Uhamiaji Tanzania kutoa uamuzi dhidi ya Klabu ya Mpira wa Miguu Polisi Tabora, ili kuisadia Klabu ya Geita kupanda katika Ligi Kuu Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles