25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

ATCL kutangaza utalii kupitia safari za ndege

Mhandisi Emmanuel Korosso
Mhandisi Emmanuel Korosso

Na PATRICIA KIMELEMETA, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Ndege Tanzania (ATCL) limeingia makubaliano ya kutangaza utalii wa ndani kupitia safari za ndege kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Mhandisi Emmanuel Korosso, aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa miongoni mwa makubaliano hayo ni TTB kuandaa semina za mafunzo kwa wafanyakazi wa ATCL, wakiwamo marubani na wahudumu wa ndege kuhusu vivutio vya utalii wa ndani na jinsi ya kuvitangaza kwa abiria.

Alisema TTB pia imetakiwa kubeba jukumu la kutayarisha jarida katika ndege linalotoka mara nne kwa mwaka, pia TTB itatoa bure dawati la maonyesho yake ya utalii ili ATCL ijitangaze na ATCL kutangaza vivutio vya utalii kupitia runinga za ndani ya ndege.

“Tumekubaliana kutangaza utalii wa ndani kupitia abiria watakaokuwa wanatumia usafiri wa ndege, faida itakayopatikana itanufaisha pande zote mbili, hivyo basi ATCL itaweza kuwasafirisha watalii kwenda mikoa kama vile Arusha, Mwanza, Kagera na Zanzibar ambako kuna vituo vya utalii ili kuongeza idadi na mapato yatokanayo na utalii,” alisema Mhandisi Koroso.

Alisema Bodi ya ATCL itatoa ushirikiano kwa kuwasafirisha watalii hao na kuwafikisha kwenye miji yenye vivutio na si kuangalia vivutio vya utalii tu bali kuongeza pato la taifa na fedha za kigeni.

Alisema kupitia ndege hizo, wanatarajia kubeba watalii kutoka nje ya nchi ambako ndege hizo zinafika na kusababisha gharama za utalii kushuka.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Thomas Mihayo, alisema ushirikiano huo utalisaidia taifa kupata fedha kupitia watalii.

Alisema kusuasua kwa ATCL hapo awali, kulichangia kwa kiasi kikubwa kuyumba kwa sekta ya utalii na kwamba kusimama tena kwa shirika hilo ni kukuza sekta ya utalii nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles