KOCHA wa klabu ya Manchester City, Pep Guardiola, amekanusha kauli ya kwamba amekuwa akiwakataza wachezaji wake kufanya mapenzi huku wakiwa katika maandalizi ya timu yao.
Wiki iliyopita mchezaji wa klabu hiyo, Samir Nasri, ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo katika klabu ya Sevilla, aliweka wazi kuwa kocha huyo amekuwa akiwakataza wachezaji wake kufanya mapenzi na wachumba zao, hata kama wamepewa siku moja ya mapumziko.
Nasri alisema kocha huyo alikuwa anawaambia wachezaji wake kwamba endapo watakuwa wanafanya mapenzi huku wakiwa wanajiandaa na michezo yao, ni rahisi kupata majeraha ya misuli.
Guardiola ameonekana kukanusha kauli ya mchezaji huyo ambaye amemtoa kwa mkopo na kudai kuwa haiwezekani mchezaji akae bila kufanya mapenzi.
“Ni jambo ambalo haliwezekani kwa mchezaji kucheza soka la hali ya juu kama hafanyi mapenzi na mpenzi wake, sijawahi kumkataza mchezaji yeyote kufanya mapenzi, lakini ninaamini kama mchezaji akiwa anafanya mapenzi basi ataendelea kuwa katika kiwango kizuri endapo ataendelea kufanya na mazoezi,” alisema Guardiola.
Inasemekana kuwa, kocha huyo baada ya kujiunga na klabu ya Manchester City aliomba kuondolewa kwa mtandao wa wifi katika baadhi ya maeneo ya uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo kwa ajili ya kupunguza muda wa wachezaji kutumia mitandao ya kijamii mara kwa mara.
Tangu ujio wa kocha huyo ndani ya Manchester City, kumewapa wakati mgumu baadhi ya wachezaji wake, kama vile kiungo mwenye mchango mkubwa katika mafanikio ya klabu hiyo, Yaya Toure, huku wachezaji wengine wakitakiwa kuondoka kama vile Nasri na wengine.
Kocha huyo kwa sasa amesema kikosi chake kimeanza kukamilika na anaamini kitaleta ushindani wa hali ya juu katika michuano ya Ligi Kuu nchini England, huku akiamini uwepo wa beki wake, John Stones, ndio mwisho wa matatizo katika safu ya ulinzi.
Beki huyo wa zamani wa Everton anamfananisha na beki wa kati wa klabu ya Barcelona, Gerard Pique, na amedai kuwa mchezaji huyo atakuja kuwa beki bora duniani.