MWANASIASA mkongwe, Steven Wasira, amesema hana mpango wa kustaafu siasa baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kuhalalisha ushindi wa Mbunge wa Bunda Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ester Bulaya.
Wasira ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 71, aliyasema hayo jana wakati alipozungumza na MTANZANIA Jumapili lililotaka kufahamu msimamo wake kuhusu hukumu hiyo iliyotolewa juzi na mustakabali wake kisiasa.
Baadhi ya wafuatiliaji wa siasa nchini, wamekuwa na mtazamo kuwa huweda hukumu hiyo ingemfanya Wasira astaafu siasa kutokana na umri wake, lakini pia kulishikilia jimbo hilo kwa awamu tofauti tangu alipojiengua Chama cha NCCR-Mageuzi na kushinda ubunge mwaka 2005 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Nistaafu siasa kwa hukumu? Kukosa ubunge haihusiani kabisa na kustaafu, na kwanini hilo swali hamkuniuliza tangu mwaka jana baada ya uchaguzi?” alihoji Wasira wakati akizungumza na gazeti hili jana.
Akijibu swali la mwandishi ambaye alitaka kujua iwapo atakata rufaa, Wasira alimtaja wakili wake Constantino Mtalemwa kuwa ndiye anayepaswa kulizungumzia hilo.
Kuhusu kutokuwapo wakati wa hukumu hiyo juzi, Wasira alisema yeye alikwenda mahakamani hapo kama shahidi na kwamba wapigakura wake ndio walifungua kesi hiyo.
Hata hivyo, katika hatua nyingine, Wasira alishindwa kumzungumzia mshindi wa hukumu hiyo, Bulaya na kuishia kusema kuwa ni mwanasiasa aliyekuwapo tangu Bunge lililopita.
Wasira alihamia upinzani kupitia chama cha NCCR-Mageuzi baada ya kutoridhishwa na ushindi wa Jaji Joseph Warioba (Waziri Mkuu na Makamu wa Rais mstaafu) katika jimbo la Bunda na baadaye mwaka 1999 alirudi tena CCM.
Mwanasiasa huyo mwaka jana alikuwa miongoni mwa makada 42 wa CCM waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kupeperusha bendera ya urais, lakini hata hivyo aliikosa.
Wafuatiliaji wa siasa hapa nchini wanamtambua Wasira kama mwanasiasa mkongwe aliyeanza kuwa mbunge tangu akiwa na miaka 25 baada ya kushinda kiti hicho katika Jimbo la Mwibara mwaka 1970.
Katika nafasi za utumishi wa umma, Wasira alianza kuwa Naibu Waziri wa Kilimo chini ya utawala wa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Tangu enzi hizo za Mwalimu Nyerere, Wasira aliendelea kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini, huku akiwa mbunge katika tawala zilizofuata hadi utawala huu wa Rais Dk. John Magufuli alipoanguka ubunge.
Itakumbukwa katika kesi iliyotolewa hukumu juzi, kwa mara ya kwanza ilifunguliwa na wapigakura wanne wa Wasira baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana wakipinga matokeo yaliyompa ushindi Bulaya.
Wapigakura hao ni Magambo Masatu, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Asetic Malagila.
Maombi hayo ya kutaka kesi isikilizwe, yaliwasilishwa kwa mara ya kwanza kwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mohamed Gwae, ambaye Januari 25, mwaka huu aliitupilia mbali kwa hoja kuwa wapigakura hawana haki ya kupinga matokeo hayo.
Baada ya kukataliwa maombi hayo, walikata rufaa kwenda kwa Jaji Sirilius Matupa wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Kitengo cha Biashara, ambaye hata hivyo aliwarudisha walalamikaji hao kurekebisha baadhi ya vifungu, kisha ilipelekwa kwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Rosemary Ebrahim ambaye aliisikiliza na kuiondoa tena baada ya kubaini kasoro katika kiapo kuwa wakili aliyesaini siye aliyekuwa ameapa.
Makosa hayo yaliondolewa na baadaye kesi hiyo kupelekwa kusikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda hiyo, Jackilene Dimelo, ambaye aliiruhusu iende kwa jopo la majaji watatu ambao waliipiga tarehe ili iweze kusikilizwa na majaji watano ambao waliamuru irejeshwe kwa Jaji Lameck Mlacha.
Novemba 18, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza ilikohamishiwa kesi hiyo namba moja ya mwaka huu, katika Mahakama ya Mkoa wa Mara mjini Musoma, chini ya Jaji Noel Chocha, iliitupilia mbali na kumthibitisha Bulaya kuwa ni mbunge halali wa jimbo hilo.
Wakati huo huo, walalamikaji wa shauri hilo wamesema hawajaridhika na uamuzi huo, hivyo wanajiandaa kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa.
Akizungumza jana na gazeti hili kwa ujumbe mfupi wa simu, mmoja wa walalamikaji, Asetic Malagila, alisema baada ya kusikiliza hukumu hiyo walikubaliana na mwanasheria wao kuwa wakate rufaa kwa kile alichokiita walishindwa kwa sababu ya uonevu.
“Tumeshindwa kwa uonevu tutatafuta haki yetu katika mahakama ya rufaa, tuko katika hatua ya kukata rufaa Court of Appeal,” unasomeka ujumbe huo wa Malagila.
Habari hii imeandaliwa na Elizabeth Hombo, Agatha Charles (Dar es Salaam) na Ahmed Makongo (Bunda).