26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

Filikunjombe ataka wanasiasa wajipime

Deo-FilikunjombeNa Mwandishi Wetu, Ludewa

MBUNGE wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), amewataka viongozi wa siasa kujitafakari kuhusu nafasi wanazoziongoza kuona kama wapo kwa ajili yao binafsi ama kwa ajili ya jamii iliyowachagua.

Filikunjombe alitoa kauli hiyo juzi wakati akitoa salamu zake za pole kwa wakazi wa Ludewa katika mazishi ya aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wilayani hapo, Elizabeth Haule yaliyofanyika kijijini kwake Luana.

Alisema lazima viongozi kujenga utamaduni wa kuwatumikia wananchi ambao wamewawezesha kuwa na nafasi hizo badala ya kujinufaisha wao.

Mbunge huyo alisema Wilaya ya Ludewa imempoteza kiongozi imara na kuwa uongozi wa M-NEC huyo ulikuwa ni wa kuigwa kutokana na namna alivyokuwa akiwasilisha mambo yake na siku zote kuonyesha kuwatumikia wana CCM waliomwezesha kuwa NEC.

” Siku mbili kabla ya kifo chake nilipata kuzungumza naye kupanga juu ya sherehe ya CCM ila alinikumbusha juu ya barabara ya Malato, Itundu.

“Alikuja kwangu na kuniomba kila wakati …..hadi siku ya mwisho nikipangana naye mwishoni aliniuliza ahadi yake juu ya barabara vipi?

“Siku moja nilimtania kuwa ‘wewe ni mkazi wa Malato na unasali Anglikana na ile barabara inakwenda Kanisa Katoliki’… ila alisema wote ni watu wake …hivyo naomba nisema siwezi kuacha kutekeleza ombi lake la barabara,”alisema.

Mbunge huyo alisema amepata kujifunza mengi kutoka kwa Elizabeth enzi za uhai wake alikuwa akiomba pasipo kutumia nguvu.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo alikuwa akimuomba ni kusaidia kuchonga barabara ya kijiji hicho kuelekea Kanisa la RC lililopo umbali wa zaidi ya kilometa tatu kutoka barabara kuu ya Ludewa – Njombe itakayotumia Sh milioni 26 .

Alisema Elizabeth alikuwa akiutumia uongozi wake vizuri kwa kuwajali wananchi wake hivyo ni vema kila kiongozi wa siasa kuona anatumia vema nafasi yake aliyopewa na wananchi kwa kuwatumikia waliomchagua.

Mbunge huyo alisema kwa upande wake bungeni akiwa anaomba jambo kwa ajili ya wana Ludewa siku zote amekuwa akitumia nguvu lakini yeye alikuwa akiomba kwa unyenyekevu na siku zote alikuwa ni mtu wa kuwatumikia wananchi wake hivyo lazima kila kiongozi wa siasa kujitafakari zaidi .

Elizabeth katika uhai wake mbali ya kuwa mjumbe wa NEC akiwakilisha Wilaya ya Ludewa pia alikuwa ni mwenyekiti wa UVCCM wilaya ya Ludewa na mwenyekiti wa kikundi cha Sanaa Ludewa.

Alifariki dunia kwa ugonjwa wa moyo juzi katika Hospitali ya Wilaya ya Ludewa baada ya kuzidiwa akitokea katika sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles