25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa, NEC hapatoshi leo

SLAANa Arodia Peter, Dar es Salaam
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) pamoja na vyama vya siasa, leo wanatarajia kukutana katika kikao cha pamoja ambacho kinaweza kuibua hoja kali kutoka miongoni mwa wadau.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Bunge uliotolewa Februari 4, mwaka huu baada ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, kutaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili kuweza kujadili hatua ya NEC kuanza uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo mpya wa kielektoniki (BVR) kuanzia Februari 16, mwaka huu bila kushirikisha wadau.
Katika mkutano huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam leo, NEC itakutana na vyama vyote vya siasa, huku viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakidai tume imefanya maandalizi hafifu bila kushirikisha wadau pamoja na uwapo wa njama za kuvuruga mchakato huo.
Kupitia gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA), NEC ilitangaza kuanza uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kuanzia Februari 16 hadi Aprili 29, mwaka huu.
Uandikishaji huo utaanza katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mtwara, Njombe na kumalizia Dar es Salaam na Zanzibar.
Akizungumzia mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema hatua hiyo ya NEC imeonyesha dharau na ukigeugeu kwani walikubaliana na vyama vya siasa kufanya tathmini ya awali juu ya uandikishaji wa majaribio katika majimbo ya Kawe, Kilombero na Katavi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Slaa, alisema wanaamini NEC inafanya kazi kwa kusukumwa na wenye mamlaka, ndiyo maana kila siku taarifa zao zinabadilika.
Alisema hatua ya tume hiyo kutangaza tarehe ya kuandikisha wapigakura bila kuwapo maandalizi yoyote ya uhamasishaji wananchi ni mbinu za kuvuruga mchakato huo.
“NEC imejiweka pabaya na hii inaonyesha uhalisia wake, ni dhahiri inaandaa mazingira ya kuvuruga uchaguzi na inakaribisha machafuko katika nchi.
“Na haya si maandalizi ya bahati mbaya, ni maelekezo ya ngazi za juu kwa sababu taasisi nzito kama NEC inakuwa kigeugeu kwa jambo zito na la kitaifa kama hilo, kuna njama za wazi, hatutakubali,” alisema Dk. Slaa.
Naye Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Mbatia, alisema hatua ya NEC kutangaza uandikishaji wa daftari bila kukaa meza moja na vyama vya siasa ni fujo na inaashiria machafuko ndani ya nchi.
Mbatia, alisema NEC imedharau maazimio ya Bunge ambayo yaliitaka kukaa meza moja na vyama vya siasa ili kukubaliana namna bora ya kuingia katika uandikishaji.
Alisema mfumo huo mpya wa uandikishaji kwa njia ya kielektroniki una changamoto nyingi na si jambo la kukurupuka kama ambavyo tume inataka kufanya.
“Bunge ndiyo chombo kikuu cha kuisimamia Serikali, ni juzi tu Bunge hilo limeiagiza NEC ikae na vyama vya siasa, lakini kinyume chake wameamua kufanya watakavyo bila kuzingatia azimio hilo la Bunge.
“Uzoefu unatuonyesha nchi zote zinazoingia kwenye machafuko huanzia kwenye uchaguzi ambao unasimamiwa vibaya na tume zake. Hiki kinachofanywa na NEC ni fujo na ni kiashiria cha kutaka kuleta machafuko katika nchi,” alisema Mbatia.

CCM YANENA
Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema kuwa anashangazwa na NEC kushindwa kujibu hoja za wadau kila zinapotolewa.
Alisema hatua hiyo inaifanya jamii iamini kila kinachoendelea CCM ipo nyuma hali ya kuwa haihusiki na jambo lolote katika mchakato huo.
“CCM kama mdau wa NEC kama vilivyo vyama vingine, tunashangazwa sana na NEC kukaa kimya, watu wana shaka juu ya muda na hata kusuasua kwa kazi hii… badala yake wahusika wapo kimya.
“Hili hapana, inaweza ikawa kuna jambo wadau wanahoji juu ya uwezo wa vifaa na fedha kwa NEC, leo hii likiharibika jambo lolote katika hilo, wa kulamiwa inageuka kwa CCM, hili hapana, nasi tutawaeleza ukweli juu ya hili,” alisema Nape.
Pamoja na mkutano huo wa wadau, NEC ilikiri kuwa mashine 250 zilizotumika katika majaribio ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki yaliyofanyika Desemba mwaka jana katika majimbo matatu nchini, hazifai.
Imesema baada ya kugundua kasoro zilizo kwenye mashine hizo, sasa inakusudia kufanya marekebisho wakati wa utengenezaji wa mashine mpya 7,750 zinazotarajiwa kuagizwa kwa ajili ya kutumika katika kazi hiyo kuanzia mwezi ujao.
Mbali na hilo, changamoto zilizojitokeza katika majaribio hayo ambayo yalihusisha watu 41,721 ni pamoja na matatizo ya programu za mifumo ya kompyuta.
Changamoto nyingine iliyotajwa na NEC kupitia Mwenyekiti wake Jaji Mstaafu Damin Lubuva, ni hali ya hewa ya joto ambayo iliharibu urahisi wa utendaji kazi wa mashine hizo pamoja na watumishi kutokuwa na ujuzi wa kuzitumia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles