25.2 C
Dar es Salaam
Monday, April 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mbasha: Flora anaujua ukweli wa mtoto

MBASHA3gwajima2Veronica Romwald na Mwajuma Mazao, Dar es Salaam
HATIMAYE mwimbaji wa nyimbo za Injili nchini, Emmanuel Mbasha, ameibuka na kuweka wazi suala la mgogoro wa mtoto na mkewe Flora Mbasha.
Hatua hiyo imekuja miezi saba tangu wawili hao walipoingia katika mgogoro wa ndoa yao hali iliyosababisha Mbasha kufikishwa mahakamani kwa kosa la ubakaji.
Hivi karibuni, picha za mtoto mchanga zilisambazwa katika mitandao ya kijamii na kudaiwa kuwa ni wa Flora aliyezaa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana baada ya kuahirishwa kwa kesi ya ubakaji inayomkabili katika Mahakama ya Ilala, Mbasha alisema hayupo tayari kuzungumzia kuzaliwa kwa mtoto huyo, ila anayeweza kueleza ukweli kuhusu baba wa mtoto ni Flora mwenyewe.
Alipoulizwa kwanini anashindwa kueleza suala hilo la mtoto hali ya kuwa Flora bado ni mke wake kwa mujibu wa sheria, alisisitiza kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa.
“Siwezi kuongea chochote, ukweli wote anaujua Flora nendeni mkamfuate atawaeleza, na sijaongea na gazeti lolote kuhusu mtoto huyo… kwa sasa sipo tayari kusema lolote,” alisema Mbasha.
Februari 10, mwaka huu gazeti hili lilimtafuta Flora kwa njia ya simu ili kuzungumzia suala hilo ambapo alisema: “Siko tayari kuzungumza lolote kuhusu Mbasha kwa sasa. Yeye ana jeuri ya pesa ndiyo maana anafanya haya yote, lakini mimi ninasimama na Mungu wangu na ninajua Mungu atanipigania.”
Alipoulizwa kuhusu hali ya mtoto wake mchanga, alisema: “Mtoto hajambo, lakini mtoto anayesambazwa kwenye mitandao siyo wangu, na hizo picha nyingine nafikiri ni za kutengeneza tu.”
Kutokana na kuzagaa taarifa za picha za mtoto huyo ambaye anadaiwa kuwa amezaa na Flora, Mchungaji Gwajima, alisema taarifa hizo ni za uzushi na huenda zinasambazwa na Mbasha.
Mchungaji Gwajima alikwenda mbali na kusema pamoja na uzushi huo unaosambazwa dhidi yake kwa kuhusishwa katika uhusiano na Flora, anamwachia Mungu kila kitu.
“Si unajua hiyo issue (suala, jambo) ya Mbasha ni ya muda mrefu tu. Wakati mwingine mimi huwa sijibu ujinga.
“Awali niliwaza kuwashtaki (alipoanza kuhusishwa kwamba ana uhusiano na Flora) wanaoeneza uzushi huo, lakini nikaona ‘It doesn’t hold water’ (haina mashiko), najua shutuma hizo zinatoka wapi,” alisema Mchungaji Gwajima.
Alipoulizwa kuhusu mtu anayemshuku kueneza uvumi huo alisema: “Probably’ (nadhani) atakuwa Emmanuel Mbasha mwenyewe. Tangu mwanzo alipotuhumiwa kumbaka shemeji yake na kutoroka akihofia kukamatwa na polisi, mkewe alikuja kanisani kwetu na mimi nilimwagiza mwenyekiti wa kusaidia jamii amsaidie.
“Sasa Mbasha alipotoka huko alikokimbilia na kusikia kuwa mkewe yuko hapa kanisani, ndipo alipoanza kueneza uzushi,” alisema.
Gwajima alisisitiza kuwa Flora hakufikia kwake kwa jambo lolote bali aliendelea kuishi katika nyumba aliyopanga.
Alipoulizwa kwanini hamshtaki Mbasha ili kulinda heshima yake, alisema ameshawaita ndugu zake akiwamo baba yake mzazi, lakini nao wakaonekana kutommudu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya kituo cha televisheni ya East Africa (EATV), Agosti 27, mwaka jana Flora alihojiwa na kituo hicho kupitia kipindi cha Kikaangoni Live, kinachoendeshwa kwa njia ya mtandao wa kijamii wa Facebook na kusema ujauzito aliokuwa nao ni wa mumewe Mbasha na si Mchungaji Gwajima.
Alisema hawezi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mchungaji Gwajima kwa kuwa ni mjomba wake, na kwamba watu wamekuwa wakizusha kwa lengo la kumchafua na kumshushia hadhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles