NEEMA Lema (33), mke wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Alifikishwa mahakamani hapo jana na kuunganishwa katika kesi ya tuhuma za kusambaza ujumbe unaomkashifu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 351 ya mwaka huu, mshitakiwa mwingine ni Lema ambaye alifikishwa mahakamani hapo Agosti 20 mwaka huu.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Agustine Rwizile, Wakili wa Serikali, Blandina Msawa, aliiomba mahakama kufanya marekebisho kwenye hati ya mashtaka kwa kumuongeza Neema.
Akisoma mashtaka yanayomkabili Neema, wakili huyo alidai Agosti 20 mwaka huu, jijini Arusha, mshtakiwa alituma ujumbe kwa simu ya mkononi uliosema, ‘karibu tutakudhibiti kama Uarabuni wanavyodhibiti mashoga’.
Neema anayetetewa na Wakili Sheck Mfinanga, alikana kutenda kosa hilo na kupewa dhamana hadi Novemba 15, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani hapa, lilimkamata na kumhoji Lema kwa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema Lema alitoa lugha hiyo wiki iliyopita katika mikutano halali aliyoifanya jimboni kwake.
“Tumemkamata Lema kwa kutoa lugha ya uchochezi ambayo ni kinyume cha sheria.
“Baadhi ya maneno aliyotoa yenye uchochezi ni pamoja na kusema Rais Magufuli akiendelea kugandamiza demokrasia, taifa litaingia katika
umwagaji wa damu, nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa udikteta pamoja na kuwataka wananchi wawe tayari kwa lolote na waache uoga kwa vile uoga ni dhambi mbaya kuliko dhambi zote duniani.
“Baada ya kumhoji kuhusu maneno hayo, tulimwachia kwa dhamana na sasa jalada lale liko kwa Mwanasheria wa Serikali kwa ajili ya
kuandaa hati ya mashitaka afikishwe mahakamani,” alisema Kamanda Mkumbo.