24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Jacob meya mpya ubungo  

boniface-jacobNa VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

DIWANI wa Kata ya Ubungo, Boniface Jacob (Chadema), amechaguliwa kuwa Meya wa Halmashauri ya Ubungo, Dar es Salaam.

Jacob ameshinda nafasi hiyo kwa kura 16 kati ya 18 zilizopigwa dhidi ya mpinzani wake, Yusuph Yenga (CCM) aliyepata kura mbili.

Akitangaza matokeo hayo jana, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo, John Kayombo, alisema Ramadhani Kwangaya (CUF), ameshinda nafasi ya naibu meya kwa kura 15 kati ya 18 zilizopigwa.

“Jumla ya kura zote ni 18, hakuna hata moja iliyoharibika, wajumbe wa Ukawa walikuwa 15 na CCM walikuwa watatu,” alisema.

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Jacob, alisema amejipanga kufanya kazi kwa kasi ili Ubungo ipate maendeleo.

“Nimepata umeya wa Ubungo, nimejipanga kufanya kazi zaidi ya nilivyofanya Kinondoni, utendaji wangu wa Kinondoni umemshawishi hadi leo (jana) mjumbe mmoja wa CCM amenipa kura.

“Naionya Serikali kwamba Ubungo ni kambi ya wapinzani, hatutakuwa na unyonge kama tulivyokuwa Kinondoni, huku wakija na heshima tutawaheshimu,  figisu zao na michezo yao michafu waiache huko huko,” alisema.

Alisema yeyote atakayefanya figisu watapambana naye.

“Ubungo tunaondoka na gia zote, wasije wakaona tumebadilika, huku ni nyumbani kwetu, wananchi walithibitisha wazi tangu Oktoba 25, mwaka jana kwamba wameichoka CCM.

“Wananchi wa Kinondoni wasikate tamaa, tumejipanga kuhakikisha wanapata haki ya kupata meya wao kwani aliyeko sasa ni meya wa ‘Kichina’,” alisema.

Kwa upande wake, Kwangaya alisema atashirikiana vema na Jacob kwa kumpa ushauri mzuri ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa Ubungo.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya muda ya uongozi ndani ya CUF, Julius Mtatiro, alisema uchaguzi huo umedhihirisha kuwa wananchi wamewaamini Ukawa na kwamba sasa ni wakati wa kuchapa kazi.

“Dola imehamishia nguvu zote Kinondoni, wananchi msiwaachie viongozi pekee kesi ile, nanyi jitokezeni kwa wingi mahakamani hadi haki ipatikane, 2019 tutakuwa tumejipanga kupata wawakilishi wengi zaidi Serikali za Mitaa na 2020 tutatoa wawakilishi wengi wa taifa, maana Rais John Magufuli anatusafishia njia, ” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles