KOCHA wa klabu ya Arsenal ‘The Gunners’ Arsene Wenger, amedai kuwa mwezi huu ni wakati ambao anaweza kuzungumzia mwenendo wa klabu yake katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu nchini England.
Wenger amesema huu ni mwezi mgumu kwake kwa kuwa anakutana na ushindani wa hali ya juu na anatarajia kucheza na Tottenham pamoja na Manchester United na michezo mingine, hivyo baada ya kumaliza michezo hiyo anaweza kueleza mwenendo wa ubingwa kwa klabu yake.
Kwa sasa Arsenal inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi, huku nafasi ya kwanza ikishikwa na Man City ambayo ina alama 23 sawa na Arsenal wakitofautiana kwa mabao, lakini Wenger amedai kuwa kipindi hiki ni kipimo sahihi cha ubingwa kwake.
“Kwa sasa naweza kusema kuwa tupo katika wakati mgumu sana kutokana na michezo iliopo mbele yetu kwa mwezi huu, ninaamini mwishoni mwa mwezi huu tutaweza kusungumza mwenendo wa timu.
“Timu ina umoja kwa sasa na tunaamini tunaweza kufanya vizuri, kila mchezaji anapambana kwa ajili ya kuiweka klabu sehemu salama, lakini ushindani umekuwa mkubwa sana,” alisema Wenger.
Kocha huyo amedai kuwa kwa sasa amefanikiwa kupata safu ya ushambuliaji ambayo imekamilika hasa katika mfumo wake wa 4-4-2, ambapo Alexis Sanchez atasimama mbele na Giroud.
Amesema wachezaji hao wameonesha uwezo wa hali ya juu katika mchezo wa mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo walicheza na Sunderland na kushinda mabao 4-1, huku mabao hayo manne yakifungwa na wachezaji hao wawili.