33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wiki nzuri kwa Clinton, mbaya kwa Trump

clinton_trump_split

NA JOSEPH HIZA,

WIKI iliyopita tulikuwa na makala kuhusu mijadala iliyojitokeza baina ya kambi mbili za wagombea urais wa Marekani kabla ya mdahalo wao wa kwanza uliofanyika Jumatatu ya wiki hiyo.

Mijadala hiyo kwa kuitazama ililenga kujihami dhidi ya uwezekano wa kushindwa au kujitengenezea mazingira ya ushindi wakati wa mdahalo huo ambayo huchangia kumpaisha mgombea urais.

Tuliona kambi ya mgombea urais wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton, ikisisitiza kwa waandaaji hasa msimamizi wa mdahalo huo kuhakikisha mpinzani wake ‘hachomiki’ iwapo atadanganya kutokana na uzoefu wa nyuma.

Wasiwasi wa kambi ya Clinton ulikuwa kutumia muda mwingi kuweka rekodi sawa, yaani kusahihisha uongo wowote ule kutoka mdomoni mwa Trump na hivyo kushindwa kupata muda mwingi wa kushambulia.

Kwa upande wa kambi ya mpinzani wake wa Republican, Donald Trump, ilipinga msimamizi wa mdahalo kuingilia kati kuweka rekodi sawa, ikisema si jukumu lake kwani kutamfanya awe sehemu ya mdahalo huo.

Aidha, kambi ya Trump wakati ikijigamba kuwa itashinda mdahalo huo, ulieleza wasiwasi wake uko kwa vyombo vya habari kupindua matokeo ya mdahalo huo ili kumpa ushindi mpinzani wake.

Wakati Clinton akichimbia kwa wiki mbili kujiandaa na mdahalo huo wa kwanza kati ya mitatu ikiwamo mbinu za kutumia midahalo bandia yenye Trump bandia.

Lakini Trump badala ya kujiandaa, alibeza yote hayo akimfananisha Clinton na roboti linalojazwa programu kichwani badala ya kujisimamia mwenyewe kama mwanadamu.

Katika hilo, alisema Clinton hafai kuwa Rais wa Marekani kwa vile kiongozi wa taifa hilo kubwa hutakiwa kujisimamia mwenyewe na kujibu maswali na si kujazwa maswali na majibu kichwani!

Hata hivyo, mwisho wa yote, Clinton alishinda na funzo lililojitokeza ni umuhimu wa maandalizi kabla ya kitu chochote kile.

Clinton aliingia ukumbini akiwa na hali ya kujiamini, akifahamu nguvu na udhaifu wa mpinzani wake ambao aliutumia vyema kumshinda mpinzani wake aliyelazimika kuitikia badala ya kushambulia.

Moja ya udhaifu wa Trump ambao Clinton aliutumia vyema ni kauli za nyuma zisizo na ukweli za Trump ni kama vile madai kuwa alipinga vita ya Irak wakati si kweli.

Nyingine ni kauli za kibaguzi dhidi ya wanawake, wenye ulemavu, Waislamu na wahamiaji ikiwamo kwamba Rais Barack Obama hakuzaliwa Marekani.

Mbali ya maandalizi, Clinton alitumia uzoefu wake wa kazi ya uwakili na kazi serikalini na Ikulu kueleza vyema masuala ya sera mbalimbali ikiwamo za kigeni.

Tangu mwanzoni kabla ya mdahalo maswali yaliyojiri kwa wengi yalikua je, Trump ataweza kuwa na nidhamu, je, atajizuia kuwatukana wageni, wanawake au Waislamu kwa kipindi chote cha dakika 90 za mdahalo?

Naam, Trump alionesha nidhamu, hakutoa matusi wala kashfa kwa wanawake na Waislamu pengine kutokana na kutahadharishwa au mikwara ya kambi ya Clinton.

Kwa kutumia kejeli, akili na ucheshi, Clinton alionyesha kuwa ukiacha maneno matupu na matusi ya nguoni, Trump hana jipya na hana lolote.

Mbele ya hadhara inayokadiriwa kukaribia watu milioni 100 ikiwa ni rekodi, Clinton alimwanika kweupe mpinzani wake, ambaye mwanzoni alianza vyema kabla ya suala la kodi kuibuka.

Trump aliishia kumkatisha mara kwa mara Clinton na kushindwa kuibua masuala aliyotaka kujadili kama vile uhusiano wa mke huyo wa Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton na wahisani matajiri.

Aidha, alishindwa kuibua kashfa kuhusu shambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Benghazi, Libya na barua pepe ambazo zote zilitokea wakati Clinton akihudumu uwaziri wa mambo ya nje.

Aidha, akikabiliwa na maswali kuhusu siasa za nje, kitisho cha ugaidi na masuala ya usalama, hata kuhusu masuala ya uchumi na kodi, Trump hakuwa na jibu zaidi ya kauli za mkato, kujisifu zikibakia dhana tupu.

Moja ya kauli hizo kuhusu kodi ni pale alipoulizwa na mpinzani wake kuhusu kitendo chake cha kutoanika marejesho yake ya kodi.

Alidai kwamba yu tayari kuanika marejesho yake ya kodi iwapo tu, Clinton ataanika maelfu ya barua pepe zilizofutwa.

Clinton akauambia umma, Trump amekataa kuweka wazi kodi zake kwa vile kuna uwezekano wa uwapo wa jambo muhimu ambalo hataki nchi ijue au huenda likawa jambo baya ambalo anajaribu kulificha.

Trump alijibu kifupi: Basi hiyo inaonesha niko smati.”

Yu smati alimaanisha nini? Bila shaka jibu hilo linaakisi ujanja ujanja kama kile kilichosemwa na wasaidizi wake mwishoni mwa wiki wakati gazeti la New York Times lilipotoa makala ikieleza kuwa Trump alipata hasara ya zaidi ya dola milioni 800, ambazo huenda zilimwezesha kutolipa kodi kwa miaka 18.

Wasaidizi wake hao walimtetea bosi wao huyo kuwa hakufanya kosa lolote na kuwa anaijua vyema sheria za kodi na kwamba yu smati kufuata sheria.

Ijapokuwa kisheria si kosa, jambo hilo lina athari au kashfa kwa Trump. Kwanini? Kwanza kuna uwezekano Trump alitumia ujanja ili kupata msamaha wa kodi.

Pili: Iwapo hakuna ujanja wowote ule, inafuta yale majigambo yake ya awali kuwa yu mfanyabiashara hodari aliyepanda kilele cha utajiri kwa juhudi zake mwenyewe. Kwamba ana kipaji cha biashara atakachotumia kuonesha namna gani mfanyabiashara kama yeye anavyoweza kuwa rais bora.

Athari nyingine za kuibuliwa kwa suala hilo lililomchukiza Trump baada ya kulishambulia gazeti hilo kutumika kumdidimiza, ni kwamba mfumo wa kodi wa taifa hilo una mianya inayopendelea matajiri kama yeye na kukandamiza watu wa kawaida ambao hawana nafuu au upendeleo wowote.

Ikumbukwe Clinton anaendesha kampeni ya kubadili sheria za kodi ili kuwabana matajiri wakiwamo watu wa familia yake, lakini Trump anataka kuzilegeza zaidi sheria hizo ili zinufaishe matajiri kwa kile anachodai zitawafanya watengeneze ajira zaidi na kupunguza umasikini.

Hakika matokeo ya mdahalo huo uliompandisha chati Clinton kama kura za maoni zinavyoonesha na kuibuka kwa taarifa mpya kuwa huenda mpinzani wake hakulipa kodi kumetengeneza wiki nzuri kwa Clinton na mbaya kwa Trump.

Trump anatakiwa kujipanga kwa mdahalo ujao utakaofanyika Jumapili hii ambao miongoni mwa wageni wake atakuwa kiongozi wa zamani wa chama cha UKIP nchini Uingereza, Nigel Farage.

Akikana minong’ono iliyoenea kwamba atamwandaa na kumfundisha Trump namna ya kumkabili Clinton, Farage ameshatoa ushauri kwa mshirika wake huyo akimtaka pamoja na mambo mengine kutojiingiza katika malumbano wakati wa mdahalo bali kuzungumza na watu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles