28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Marekani na Urusi wanahusika kuiangamiza Syria

150929145342-un-obama-putin-0928-01-super-169
Rais wa Urusi, Vladimit Putin akiwa na Rais wa Marekani Barack Obama

KUNA baadhi ya migogoro endelevu duniani ambayo hubadilika kila baada ya hatua na kusababisha kuzungumziwa mara nyingi kutokana na matukio mapya yanayoshabihiana na kuongeza mafuta kwenye moto unaowaka.

Hicho ndicho kinachojitokeza nchini Syria ambako kila kukicha huzuni inajigubika kwenye mapigano yaliyokosa mwelekeo, kwani makundi yote yanayohusika hayana malengo na kusababisha vita hiyo isijulikane mwisho wake sawa na mchezo wa kamari ya kupambanisha majogoo, ushindi ukitarajiwa kwa nasibu kwani hakuna mikakati ya hatimisho iwe kwa kushinda au kushindwa.

Tukio la kusikitisha la hivi karibuni kwenye vita inayoendelea nchini Syria ni kuvurumishwa makombora yaliyoharamishwa yanayotawanyika kwa kujigawanya vipande, ambayo kwa kawaida hutumika kushambulia eneo kubwa kwa mara moja bila kuwa na shabaha halisi yaliyotumika kuishambulia hospitali ya M10 iliyoko mjini Aleppo. Shambulizi linaloshutumiwa kutekelezwa na ndege vita za Serikali ya Syria na mshirika wake Urusi, inayotumia kisingizo cha kupigana na makundi ya kigaidi yanayotaka kumn’goa madarakani Rais Assad ili kuyapiga makundi mengine pinzani yasiyo na mrengo wa uhafidhina yanayotumiwa na Marekani kutimiza lengo la kumng’oa Assad madarakani.

Inatia shaka kama hospitali hiyo ilipigwa kwa bahati mbaya kwani inafadhiliwa na chama cha madaktari wa Kimarekani na Syria, sanjari na makombora kuipiga hospitali hiyo iliyokuwa na majeruhi wa mapigano yanayorindima katika vitongoji mbalimbali vya mji wa Aleppo unaoshikiliwa na waasi kwa sehemu kubwa huku Serikali ikihaha kuunyakua tena, lakini matukio ya sasa ni mwendelezo wa kufeli kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kuingizwa mjini humo, hali inayosababisha idadi ya raia wasio na hatia wanaouawa katika vita hiyo isiyo na macho kuongezeka na jumuiya ya kimataifa ikipiga kelele zisizo na msaada wowote katika kurekebisha hali hiyo.

Inavyoelekea pande zote zinazopigana Aleppo hazijali mustakabali wa maisha ya raia wanaouawa kila siku, kwani kwa hali ilivyo hakuna upande unaouzidi mwingine kwa eneo hodhi na hata ushindi wa mapigano. Ukitaka kufahamu maafa yanayotokea Aleppo kwa takwimu si chini ya raia 30 huuawa kila shambulizi la ndege vita linapofanywa, wakati mwingine makombora ya kemikali huvurumishwa katika mashambulizi hayo.

Watu waliouawa tangu kuvunjika kwa makubaliano ya usitishwaji mapigano majuma mawili yaliyopita, wanafikia 320 kati yao wakiwamo watoto 100 idadi ambayo si ndogo hasa ukizingatia kuwa watu wengine 300,000 wamekwama kukimbia kutoka mji huo wakiwamo watoto 100,000 katika Wilaya za Mashariki mwa mji huo ambazo hupigwa makombora si chini ya mara 1,900 kila wiki na kuharibu miundombinu muhimu zikiwamo hospitali, makazi ya raia, vinu vya kuzalisha umeme na mitambo ya usambazaji maji. Lakini inavyoelekea idadi kubwa ya vifo vya raia haiwastui wanaohusika katika mapigano hayo zikiwamo Urusi na Marekani, kwani ripoti mpya imedhihirisha kwamba Urusi imeongeza zana zake za kivita nchini Syria kwa kupeleka ndege vita aina ya Su-24, Su-34 pamoja na Su-25 ambazo ziliwahi kutumika katika vita vya taifa hilo nchini Afghanistan mnamo miaka ya 80. Kwa ujumla ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tu wa mashambulizi ya Urusi inayomuunga mkono Assad, watu wasiopungua 9,364 wakiwamo raia 3,800 wameuawa kutokana na taifa hilo kuingilia kati mapigano yasiyolihusu.

Marekani na Urusi haziwezi kukwepa lawama kwa kinachotokea sasa katika mji wa Aleppo na Syria kwa ujumla na kuangamiza raia wasio na hatia, kwani zimeingilia kati mapigano hayo kwa maslahi yao binafsi katika kurejea upya vita baridi miongoni mwa mataifa hayo mawili makubwa yanayobadilisha viwanja vya kupigania kila baada ya muda. Ndicho ambacho wameshindwa kukimaliza Afghanistan, Krimea na sasa wamehamia Syria huku wakichekeana kinafiki kutokana na kutoaminiana wakidanganyana kuwa wanaweza kuelewana ikiwamo kutafuta suluhu ya amani. Urusi inajinadi inataka amani Aleppo ikiishutumu Marekani kwa kufadhili makundi ya kigaidi yanayompinga Rais Assad, likiwamo kundi la mkusanyiko wa waasi linalofahamika kwa jina la Jhabat Fateh al-Sham ambalo zamani lilitambulika kwa jina la al-Nusra Front, linaloshutumiwa kuwa chanzo cha kuvunjika makubaliano ya usitishwaji mapambano kwa muda. Marekani inashutumiwa pia na makundi yanayoitegemea katika vita hiyo kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake, kwamba endapo Serikali ya Syria itatumia silaha za sumu itaingilia kati kwa kujitosa kwenye mapigano kuwatetea wanaounguzwa na makombora ya sumu lakini licha ya silaha za sumu kutumika haijafanya lolote.

Kwa sasa si viongozi wakuu wa mataifa hayo mawili wanaojitokeza kulumbana bali wamewaachia jukumu hilo wasaidizi wao, kwa upande wa Urusi Waziri wa mambo ya kigeni, Sergei Lavrov, ndiye anayeongea zaidi na vyombo vya habari kubainisha msimamo wa Urusi kuhusu hali ilivyo sasa nchini Syria, Marekani inamtumia zaidi msemaji wake wa Serikali, Mark Toner, anayeishutumu Urusi kwa madai yaliyokosa mwelekeo kuwa Marekani inaunga mkono makundi ya kigaidi yanayopigana Syria, akidai kuwa yamejichanganya na makundi mengine yenye mrengo wa kati na raia hivyo inakuwa vigumu kuyatenganisha na kushambulia. Mkanganyiko huu wa Syria umegharimu maisha ya watu 430,000 tangu vita ilipoanza Machi, 2011 huku wengine wanaofikia takribani milioni tano wakikimbilia nje ya nchi na wengine milioni sita na nusu wakitangatanga ndani ya nchi baada ya makazi yao kubomolewa kwa mapigano hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles