24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Lodhi: wanafunzi waliomuasi Mwalimu walikuwa sawa na mabwanyenye

mtz17-2

NA SARAH MOSSI,

WIKI iliyopita mwandishi wetu, SARAH MOSSI, aliyekuwa katika ziara ya kikazi nchini Sweden, alifanya mahojiano na Mwanazuoni Profesa Maalim Abdul-aziz Lodhi, mtaalamu wa Kiswahili anayefundisha katika Chuo Kikuu cha Uppsala nchini Sweden.

Katika mahojiano hayo alieleza historia ya wanafunzi zaidi ya 400 wa iliyokuwa Dar es Salaam University Students Union (DUSU), waliokamatwa Oktoba 1966 baada ya kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali kutoka Mnazi Mmoja Dar es Salaam hadi Ikulu ya Magogoni. Wanafunzi hao walikuwa wakipinga Muswada wa Huduma ya Jeshi.

Profesa Lodhi alikuwa ni miongoni mwa waliokamatwa na kuwekwa kizuizini ingawa kwa mujibu wa simulizi yake, hakuwa mmoja wa walioandamana lakini alikwenda Ikulu kudadisi akiwa kama ni kiongozi wa wanafunzi hao.

Profesa Lodhi alikuwa ni Katibu wa Habari wa Jumuiya ya Wanafunzi. Viongozi wengine waliokamatwa pamoja naye ni Charles Mwakasege ambaye alikuwa ni Naibu Mwenyekiti na Katibu wa Mambo ya Kimataifa, Tumaini Jeremiah aliyekuwa Katibu Mkuu na Katibu wa Mambo ya Kitaifa, Nizar Kassamali aliyekuwa Mhazini.

Kwa mujibu wa Profesa Lodhi, aliwekwa  rumande gerezani Dar es Salaam  na Police Guest Mgulani kwa siku nne na baadaye kizuizini Unguja, kwa muda wa miezi sita. Lakini alisamehewa baadaye Juni 1967, baada ya kuonekana hakuwa mmoja wa wanafunzi walioshiriki maandamano. Endelea…

MTANZANIA: Wakati mkipinga muswada ule wa Huduma ya Jeshi, unadhani kuna ambao wangeathirika zaidi na muswada ule?

PROF. LODHI: Katika darasa langu kulikuwa na watu wawili watatu waliokwishafanya huduma ya jeshi na kujitolea miaka miwili, baadaye wakaingia chuo kikuu, sasa sheria inasema unapomaliza masomo ya juu, lazima uende huduma ya jeshi miaka miwili, sasa ile miaka miwili waliyokwenda ilikuwa haihesabiki tena, sasa hii ni sheria gani hii lakini hawakutaka kusikiliza.

MTANZANIA: Unawakumbuka baadhi ya watu maarufu walioshiriki kupanga maandamano yale?

PROF. LODHI: Katika darasa langu alikuwapo Ali Mchumo, mimi nilipofika Dar es Salaam aliugua kwa hiyo shughuli zake zote nikapewa mimi, lakini tulipoingia kwenye mgogoro ule, Ali Mchumo alikuwa amesharudi, sasa sijui alichangia namna gani katika jambo hili.

Kwa sababu katika mabango yaliyochukuliwa na wanafunzi yaliandikwa ‘Remember Indonesia’, yaani tutapindua Serikali. Sasa wale wanafunzi wa Kilimani walisema wao hawajatengeneza mabango yale lakini yalitengenezwa na Prof. Chagula na watu wake na Ali Mchumo ndio walikuwa wanafunzi wake na siku zote Prof. Chagula alikuwa akiwasukuma.

MTANZANIA: Mambo gani mengine mlipendekeza yaingizwe katika ule Muswada wa Huduma ya Jeshi?

PROF. LODHI: Wanafunzi walisema hawakupinga Huduma ya Jeshi lakini tulipendekeza iitwe Huduma ya Kujenga Taifa, lakini pia waongezewe mshahara ile Sh. 180 hazitoshi, sisi tulipokuwa Chang’ombe tulikuwa tukilipwa posho ya Sh. 360, sasa itakuwaje mtu mzima unaishi na kodi ulipe kwa Sh. 180.

MTANZANIA: Je, sheria hii ilipitishwa na Bunge baadaye?

PROF. LODHI: Mwaka 1970, sheria ilibadilishwa ndio tukaweza kurudi lakini kabla ya hapo, kati ya 1967 mwanzoni na 1971 katikati walipoanza kutumia sheria hiyo, watu wengi waliwekwa ndani miezi kumi. Wakikataa mtu anawekwa ndani.

Wapo Wazanzibari pia waliwekwa ndani akiwamo Soud Hammed wa GAPCO, yeye alipelekwa Canada Civil Aviation mwaka mmoja, aliporudi jeshi walimtaka aingie katika Air Force lakini akakataa akasema yeye ni Civil Aviation si Military Aviation, wakamtia ndani miezi kumi (Court Marshall- mahakama ya kijeshi). Nani aliwapa jeshi haki hiyo ya kumweka ndani mtu ambaye hajafanya kosa la kijeshi wala si mtu wa jeshi vipi ahukumiwe na mahakama ya jeshi?

MTANZANIA: Kwanini unasema maandamano yale yalisaidia kuanzishwa kwa Azimio la Arusha?

PROF. LODHI: Hii ni kwa sababu Mwalimu Nyerere aliona walimu hawana mwelekeo wa kujenga taifa, kwanza wamepewa elimu bure kutokana na fedha za wakulima masikini, kwahiyo wanayo ‘attitude’ ya ubwanyenye. Na kweli wanafunzi wengi walikuwa na ‘attitude’  hiyo, kwahiyo kunatakiwa mapinduzi katika elimu katika utoaji wa elimu na upokeaji wa elimu. Kwamba mwelekeo wa wanafunzi lazima ubadilishwe kwamba hii elimu wanayopewa wanafunzi ni  Privilege (upendeleo, fursa) na si haki yao ni haki ya kila mwananchi. Kwamba inakuwa ‘Privilege’ kwa sababu ni wachache  asilimia moja tu wanapata.

Wakati ule ilikuwa katika watoto 100 wanaoanza shule ni mtoto mmoja tu anapata nafasi ya kwenda chuo kikuu. Hii ilikuwa ni wastani wa Afrika nzima. Ukiangalia wakati ule Afrika Mashariki yote ilikuwa na chuo kikuu kimoja tu. Asilimia 50 ya wanafunzi walikuwa wanapotea kabla ya kufika darasa la nane hasa wasichana.

Kati ya 50 wanaomaliza, ni 25 tu wanaingia sekondari, kati ya hao 25 ni 12 wanakwenda kidato cha tano na sita na vyuo vinavyotoa mafunzo kama nursing (uuguzi), Veta, ualimu na mmoja tu anakwenda chuo kikuu kusomea shahada(degree). Wale 12 wanakwenda kusoma stashhada (diploma) za aina mbalimbali.

Hali ilikuwa namna hiyo, mwalimu akaona sasa inakuwaje hawa wanafanya maandamano na kuitisha Serikali ndio  ikamfanya aharakishe Azimio la Arusha.

Simulizi hii ya Prof. Lodhi itaendelea wiki ijayo…..

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles