25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm: Uwanja kikwazo Mtwara

yanga-kochaNa MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, amesema kikosi chake kilishindwa kupata ushindi juzi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC, kutokana na hali ya uwanja kwani mazingira yake si rafiki kwa wachezaji wake.

Wakicheza ugenini kwa mara ya kwanza, mabingwa hao watetezi wa ligi kuu walibanwa mbavu na kulazimishwa suluhu na wenyeji wao Ndanda katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Kocha huyo raia wa Uholanzi, aliliambia MTANZANIA jana kuwa wachezaji wake walitawala sehemu kubwa ya mchezo lakini kwa mazingira ya uwanja, ilikuwa vigumu kucheza kwa kiwango kilichozoeleka.

Alisema wapinzani wao hawawezi kujilinganisha na kiwango walichoonyesha Yanga kwani pamoja na ubovu wa uwanja, wachezaji wake waliweza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao ambazo hazikuzaa matunda.

“Kwa sasa najaribu kufikiria mbinu nyingine zitakazotuletea ushindi katika mchezo unaofuata ambao pia tutacheza ugenini dhidi ya Majimaji FC,” alisema Pluijm.

Pluijm alisema baada ya kupata matokeo ya sare ambayo hakuyatarajia dhidi ya Ndanda, analazimika kukisuka upya kikosi chake ili wachezaji waweze kukabiliana na changamoto za viwanja vya ugenini.

Matokeo ya juzi yaliiwezesha Yanga kufikisha pointi nne na kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi unaoongozwa na vinara Azam FC waliojikusanyia pointi saba sawa na  Mbeya City iliyopo nafasi ya pili na Simba ya tatu.

Mbali na Pluijm, pia kocha wa Mwadui FC Jamhuri Kiwhelu ‘Julio’, aliwahi kulalamikia Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza unaotumiwa na timu za Toto African na Mbao FC kwa ajili ya mechi za ligi kuu.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa Ndanda, Hamimu Mawazo, alisema wachezaji walikosa umakini uwanjani, hali iliyowafanya washindwe  kuzitumia nafasi walizopata katika mchezo huo.

Alitamba kuwa wachezaji walicheza kwa kiwango cha juu tofauti na michezo miwili iliyopita, lakini hawakupata bahati ya kuwafunga wapinzani wao nyumbani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles