Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM
SIKU chache baada ya kuvunja mkataba wake na klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini na kurejea nyumbani, Kiungo wa Kimataifa, Mrisho Ngassa, ameigawa klabu yake ya zamani Yanga.
Ngassa ameigawa klabu hiyo kwa kuwa wapo wanaotaka Winga huyo arejee Yanga na wapo wasiotaka uwepo wake, wakiona utavuruga timu hiyo.
Habari za uhahika zilizoifikia MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, zilisema kuwa tayari Kocha Mkuu wa klabu hiyo, Mholanzi Hans van der Pluijm, alitamka wazi kuwa kikosi chake hakimhitaji winga huyo kwani tayari wapo wachezaji wa nafasi yake, lakini uongozi wa timu hiyo unataka uwepo wa Ngassa katika timu hiyo.
“Uongozi unataka Ngassa apewe nafasi kuonyesha uwezo wake, hili linapingana na uamuzi wa Mwalimu ambaye alisema hana mahitaji na mchezaji huyo, hivyo suala hilo kuonekana kuwagawa,” kilisema chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Hata hivyo, taarifa ya Ngassa kurudi katika klabu yake ya zamani, imezua gumzo kwa wadau wengi wa soka nchini ambao wengi wao walikuwa wakihoji kiwango chake.
Inadaiwa kurudi kwa Ngassa kunahofiwa kurudisha makundi katika timu hiyo ambayo yalikuwa yameshakwisha na timu kuwa moja.
Ngassa alirejea nchini Jumapili akitokea nchini Afrika kusini, baada ya kuvunja mkataba wake wa miaka minne na klabu ya Free State FC inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo.
Winga huyo aliyewahi kuzichezea timu ya Toto African, Kagera Sugar, Simba na Azam na Yanga, alisaini mkataba wa kuitumikia Free State mwaka jana, alidai kuchukua hatua ya kuvunja mkataba baada ya klabu hiyo kukosa mataji.