BINGWA namba moja wa mchezo wa tenisi duniani kwa upande wa wanawake, Serena Williams, jana ameweka rekodi mpya ya kushinda michezo 308 katika michuano mikubwa ‘Gland Slam’, baada ya ushindi alioupata dhidi ya Yaroslava Shvedova katika michuano ya US Open inayoendelea jijini New York, Marekani.
Nyota huyo aliyepata ushindi dhidi ya mcheza tenisi wa Kazakhstan, Shvedova, baada ya kufikisha seti 6-2 6-3, alimpiku Roger Federe katika orodha ya wachezaji walioweka rekodi ya kushinda michezo mingi kwa muda wote katika michuano mikubwa.
Ushindi huo ulifanikisha safari ya nyota huyo kufuzu hatua ya robo fainali ambapo kwa sasa atakutana na Mromania, Simon Halep, ambaye alifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kumfunga Muhispania, Carla Suarez Navarro, kwa seti 6-2 7-5.
“Ushindi wa michezo 308 ni idadi kubwa, pia najiona nimepiga hatua katika kazi yangu, lakini bado naendelea kucheza na sijui lini nitaacha kazi hii,” alisema Serena.
“Nina furaha kuwepo hapa kwani nimeweza kuvunja rekodi ambayo sikujua kama siku moja nitaweza kufanya hivyo,” alisema Serena.
Mbali na Serena, wachezaji wengine waliofanikiwa kuingia hatua ya robo fainali katika michuano hiyo ni Simona Halep, Ana Konjuh, Karolina Pliskova, Caroline Wozniacki, Anastasija Sevastova, Roberta Vinci na Angelique Kerber.