MCHUNGAJI Mawarire wa Kanisa la Baptisti ndiye mwanzilishi wa fukuto la kumpinga Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, fukuto ambalo sasa limekuwa ni vuguvugu na linaungwa na vyama 18 vya upinzani nchini humo.
Ingekuwa hapa kwetu sijui ingekuwaje hasa wakati huu ambao inaonekana kupaza sauti kupinga ukandamizaji na ukiukwaji wa Katiba na Sheria iliyoundwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi, unaonekana kuwa ni uchochezi na wanaofanya hivyo huswekwa selo na kufunguliwa mashtaka. Isitoshe, wanasiasa wa Tanzania kila mara hasa wakati wa uchaguzi, wanawaonya viongozi wa dini, kwamba wasichanganye dini na siasa.
Mchungaji Mawarire amevunja mwiko huo kama walivyofanya akina Mchungaji Ndabaningi Sithole, Askofu Desmond Tutu, Mchungaji Martin Luther King Jr na viongozi wengineo wa dini waliokuwa mstari wa mbele kupinga ukandamizaji wa haki za binadamu na ubaguzi wa rangi.
Wanasiasa wanapowakataza viongozi wa dini kutochanganya siasa na dini, wanasahau kwamba dini ni huduma ya kiroho tu, lakini mambo ya ubanwaji wa uhuru wa mtu na haki ambazo zimetamkwa katika Katiba, haki ya kukusanyika, haki ya kwenda popote anapotaka, haki ya kujiunga na kikundi chochote halali, haki ya kutoa maoni, haki ya kupata hifadhi katika jamii, haki ya kuchuma mali kwa njia halali, pamoja na haki nyingine nyingi, ikiwemo haki kuu ya mwanadamu nas haki ya kuishi.
Viongozi wa dini ni sehemu ya jamii na katu huwezi kuwatenganisha kwa sababu kama ni maumivu, kukosekana kwa chakula, kuanguka kwa uchumi, mfumuko wa bei na watu wengi kukosa kazi, viongozi wa dini huwezi kuwakataza wasiyaseme haya kwa sababu yanahusiana kabisa na siasa.
Hayo ndiyo yaliyomsibu Mchungaji Mawarire na kulazimika kujitokeza na kuyaweka wazi maumivu ya wananchi wa Zimbabwe. Anasema kwa miezi sita iliyopita, alifikirishwa sana na hali aliyokuwa nayo, alikuwa hana fedha za kuwapeleka wanawe shule kutokana na mdororo wa uchumi wa Zimbabwe inayoongozwa na Rais Robert Gabriel Mugabe wa chama cha ZANU-PF.
Mchungaji Mawarire akachukua bendera ya taifa na kuivaa, huku akijirekodi kwenye video akiorodhesha matatizo yaliyokuwa yanamkabili, yeye na familia yake. Alipomaliza akaiposti video hiyo kwenye mtandao wa Facebook na Twitter wakati wa kuadhimisha siku ya uhuru wa Zimbabwe, ambayo hufanyika Aprili 18 kila mwaka.
Video hiyo ndiyo imebadili taswira ya Wazimbabwe na kuwaondolea uwoga. Mawarire hakukusudia kutafuta umaarufu, lakini ndicho kilichotokea na amejikuta kuwa Wazimbabwe wanamwona ni mtu jasiri na anayefaa kuwa kiongozi wa fukuto. Mambo ambayo aliyarekodi ndio yanayowagusa wananchi wote nchini humo, wafanyakazi, vibarua, ‘wamachinga’ pamoja na jeshi kubwa la vijana wasio na kazi.
Serikali na viongozi wa chama tawala, wanaikosoa video hiyo na kusema ni ya uchochezi kwa kuwa inawafanya wananchi waichukie Serikali. Kama kawaida, Serikali ambayo wachunguzi wa mambo wanasema ‘imesimama kwa vidole’ na kwamba kongozi mkuu wa nchi, Rais Mugabe (92), ambaye ameitawala Zimbabwe kwa miaka 36, ametikiswa.
Mwanzoni mwa Julai mwaka huu, Mchungaji Mawarire aliongoza mgomo wa kutoenda kazini kwa siku moja (shut-down). Alikamatwa na polisi na kupelekwa mahakamani, lakini kutokana na wingi wa watu waliojitokeza kwenda mahakamani kama ishara ya kumuunga mkono, Serikali ambayo ilikuwa imeandaa mashtaka ya uhaini, ilisitisha kumsomea mashtaka na kumwachia huru bila masharti.
Vijana wengi wanajitokeza kwenye mikutano na maandamano yanayoongozwa na wanaharakati na kuhubiri maudhui ya Mchungaji Mawarire, wako vijana walio mstari wa mbele wakishirikiana na vyama vya upinzani kwenye maandamano ambayo wanasema ni ‘ad- infinitum’ hayataisha mpaka Rais Mugabe atakapoachia madaraka.
Inaelezwa kwamba Rais Mugabe alikasirishwa na umaarufu wa ghafla wa Mchungaji Mawarire na kama kawaida yake wanapotokea watu wanaompinga hata ndani ya chama chake, anawaona kuwa ni vibaraka wa nchi za Magharibi ambazo amekuwa akidai siku zote kwamba zinapanga kumpindua.
Kutokana na vitisho vya Serikali, Marekani imempa hifadhi ya kisiasa ya muda Mchungaji Mawarire. Ingawaje yuko nje ya nchi, lakini moto aliouwasha nchini Zimbabwe unaendelea kuwaka chini ya kaulimbiu ya ‘This Flag’.
Sasa kuna maandamano katika miji mikubwa na kumezuka vuguvugu jingine linaitwa Tajamuka tumegoma, ambalo limekuwa likiandaa migomo hiyo. Waandamanaji hawajifichi tena wanamwambia Mugabe ‘time to go’, yaani wakati umefika uondoke.
Zimbabwe kama ilivyo katika nchi nyingi za Kiafrika, ina matatizo ya kiuchumi, ukosefu wa ajira, kushuka kwa thamani ya dola ya nchi hiyo, rushwa na mambo yaliyosababisha hali ngumu ya maisha kama alivyoainisha Mchungaji Mawarire.
Lakini mbaya zaidi kwa Robert Mugabe na chama chake cha ZANU-PF, wanajeshi wastaafu waliopigana vita vya mstuni vya kumng’oa Ian Smith na utawala wa Wazungu wachache, wanakataa kumuunga mkono tena.
Wastaafu hao ambao walikuwa wanapendelewa na Serikali na kulipwa pensheni nzuri, nao wamemchoka. Wanasema hawamuungi mkono tena na hawatamuunga mkono katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika 2018, kutokana na kuongoza nchi kwa mkono wa chuma.
Mpinzani mkuu wa Mugabe wa chama cha Movement for Democratic Change, Morgan Tsvangirai, anawashangaa Wazimbabwe ambao bado wanamshabikia Rais Mugabe.
“Mnategemea mtu mwenye umri zaidi ya miaka 90 anaweza kuiletea Zimbabwe chochote, tunahitaji mtu mpya, mwenye nguvu na ajenda mpya ya kuijenga Zimbabwe mpya,” anasema Tsvangirai.
Mmoja wa vijana, Stern Zorwadza ambaye ni ‘mmachinga’ katika Jiji la Harare, anasema anawachukia polisi ambao kila mara wamekuwa wakimnyang’anya bidhaa zake na kuikosesha familia yake kipato, ndio maana anajiunga na mandamano ya kumshinikiza Mugabe kujiuzulu.
“Wakati huu nimeamua kwamba sitaacha utawala huu wa dhuluma uendelee kuwapo,” anasema akinukuliwa na gazeti moja nchini humo.
“Nitahakikisha kuwa nashiriki katika maandamano hadi utawala huu dhalimu utakapoondoka.”
Zorwadza alipigwa vibaya na polisi na baadaye wakamfungulia mashtaka ya usumbufu.
Imeripotiwa kwamba kuna mgawanyiko pia ndani ya Serikali kuhusu utumiaji nguvu kubwa wakati wa kuwatawanya waandamanaji. Waziri wa Elimu, Jonathan Moyo, ni mmoja wa watu waliopinga jambo hilo akisema:
“Kuzingatia sheria ni muhimu, hasa katika kipindi hiki cha vitendo vya uchokozi lakini uwepo uhalali. Kumbuka yaliyotokea 2007,” aliandika kwenye Twitter akiambatanisha picha inayomwonesha Tsvangirai akiwa amejeruhiwa vibaya mwaka 2007 alipoongoza maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu.
Ilibidi Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kuingilia kati na kumshauri Mugabe kuunda Serikali ya pamoja.