MKUTANO wa nne wa Bunge la 11unaanza leo mkoani Dodoma, huku miswada sita ya Serikali ikitarajiwa kuwasilishwa.
Akizungumza jana mjini hapa, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya, alisema pamoja na mambo mengine, Bunge litajadili miswada ambayo imefanyiwa kazi na kamati mbalimbali.
Mwandumbya aliitaja miswada hiyo kuwa ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari namba 4 wa mwaka 2016, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali namba 8 wa mwaka 2016, Muswada wa Sheria ya Wanataaluma wa Kemia namba 1 wa mwaka 2016.
Pia Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini namba 5 wa mwaka 2016, Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo namba 2 wa mwaka 2016 pamoja na Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Uvuvi namba 3 ya mwaka 2016.
Mwandumbya alisema Muswada wa kwanza kujadiliwa katika mkutano huo utakuwa ule unaohusu sheria ya upatikanaji wa habari.
“Ratiba itaanza kwa maswali na majibu asubuhi na jumla ya maswali 110 yataulizwa katika mkutano mzima wa nne lakini pia kutakuwa na maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu’’alisema Mwandumbya.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mkutano huo unatarajiwa kuwa wa wiki mbili na utamalizika Septemba 16, mwaka huu.