Watoto 200,000 huzaliwa na magonjwa ya moyo

0
779

Sulende KubhojaNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

WATOTO zaidi ya 200,000 kila mwaka huzaliwa nchini wakiwa na ugonjwa wa moyo, lakini wengi wao hawafikishwi hospitalini mapema.

Hayo yamebainishwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Sulende Kubhoja wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.

Alisema tatizo hilo ni kubwa na kwamba kwa siku katika kliniki wanapokea watoto zaidi ya 30 na kuendelea na kwa sasa kuna watoto 500 ambao wanasubiri kufanyiwa upasuaji.

Dk. Kubhoja alisema kuanzia jana zaidi ya watoto 150 wanaosumbuliwa na maradhi hayo wamefikishwa katika taasisi hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa awali na wanatarajia kufanyiwa upasuaji hivi karibuni.

“Watoto wengi huwa hawafikishwi hospitalini ndiyo maana JKCI imeanzisha uchunguzi huo, tunawafanyia uchunguzi na baadaye tutawafanyia upasuaji wale watakaobainika kuwa na matatizo.

“Kuna wengine tumebaini wana tundu kwenye moyo na hawa tutawafanyia upasuaji kwa njia ya kisasa ya kuziba tundu pasipo kufungua kifua,” alisema.

Dk. Kubhoja alisema kwa kutumia njia hiyo, ni rahisi kuwafanyia upasuaji watoto watano hadi 10 kwa siku, na kwamba watakapoanza kufanya upasuaji huo watashirikiana na wataalamu wengine kutoka nje ya nchi, ikiwamo Marekani.

Alisema uchunguzi huo ni endelevu ambapo mbali na JKCI unafanyika pia katika Hospitali ya Bugando, Mwanza na Ifakara mkoani Morogoro.

“Hivyo wazazi wapeleke watoto katika hospitali hizo kwa ajili ya uchunguzi,” alisema.

Aliongeza kuwa duniani inakadiriwa kati ya watoto hai 1,000 wanane huzaliwa wakiwa tayari, lakini tatizo hilo linaweza kuepukwa kwa jamii kujenga utamaduni wa kupima afya zao.

Aidha, alishauri watu kuwa na utamaduni wa kupima afya kabla ya kupata mwenzi, ili wajijue afya zao na wakati wa kujiandaa kubeba mimba nao lazima wafanyiwe uchunguzi kwani ni njia rahisi ya kumwepusha mtoto na maradhi hayo.0000.0

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here