MANENO SELANYIKA NA PAULINA KEBAKI (TUDARCO)
MAWAKILI wa Serikali jana waliiomba Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kutupilia mbali kiapo cha maombi ya dhamana katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake.
Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani jana mbele ya Jaji Eliezer Feleshi na mawakili wa Serikali wawili, Shadrack Kimaro na Theophil Mutakyawa, wakati shauri hilo lilipotajwa kwa ajili ya kusikilizwa.
Wakili Kimaro alidai mahakamani kuwa upande wa Serikali unapinga uwepo wa kiapo kilichowasilishwa mahakamani na upande wa utetezi unaowakilishwa na Wakili Michael Ngaro kwa sababu kina upungufu kisheria.
Alidai kiapo hicho kina upungufu katika aya ya tatu inayoonyesha aliyeapa ni Wakili Ngaro na Semi Maimu ambapo kwa pamoja wanamwakilisha mshtakiwa wa kwanza.
Upungufu mwingine uliodaiwa na mawakili wa Serikali ni Wakili Ngaro kula kiapo hicho mwenyewe na kwamba alikipeleka mahakamani kwa mujibu wake mwenyewe hivyo kwa heshima ya mahakama hakistahili kuwa kiapo cha waleta maombi wote.
“Kiapo hiki kinaonyesha kina mawakili sita lakini aliyeapa ni mmoja, jambo ambalo ni kinyume cha sheria kwa sababu mawakili wengine nao walipaswa kuthibitisha kwamba wanawakilishwa na mmoja.
“Katika aya ya nane kiapo kinaeleza mawakili watawasilisha maombi, licha ya kwamba aliyeapa kwenye kiapo ni wakili mmoja hajaeleza mahakama kuwa maombi hayo watayawasilisha kwa njia gani wakati mla kiapo ambaye ni wakili mmoja ameshaeleza kwamba anawasimamia waombaji wote pamoja na mawakili wao,” alidai Wakili Kimaro.
Aliendelea kudai kuwa kasoro nyingine ipo kwenye aya ya tisa ya kiapo hivyo aliiomba mahakama ikione kiapo hicho batili na kisichostahili kuwepo mahakamani.
Hoja hizo zilipingwa na wakili wa upande wa utetezi, Ngaro aliyedai mahakamani kuwa hazina mashiko kwa sababu vipengele vyenye upungufu havina mizizi katika kiapo husika.
Wakili Ngaro alidai awali walipokutana mawakili wa Serikali na wa utetezi mbele ya Jaji kujadiliana dhamana ya washtakiwa haikupingwa.
“Wakili Kimaro hakulalamika tulipokutana mahakamani hapa na hakupinga waombaji kumchagua wakili wanayemtaka awasimamie, alisema ni haki yao kupata dhamana,” alisema.
“Mahakama bado ina uwezo wa kuamuru kuondoa upungufu uliojitokeza katika aya hizo tatu badala ya kukiondoa kiapo chote,” alidai Wakili Ngaro.
Alidai zaidi kuwa upungufu ulioelezwa na Wakili Kimaro hauna nguvu kukwamisha kiapo na kwamba hoja hizo tatu si sehemu yote ya kiapo.
Baada ya mvutano huo wa hoja za kisheria alisema atatoa uamuzi Septemba 5, mwaka huu.
Maimu na wenzake wanashtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.16.
Miongoni mwa anaoshtakiwa nao na vyeo walivyokuwa navyo kwenye mabano ni Benjamin Mwakatumbula (Kaimu Mhasibu Mkuu), Astery Ndege (Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers), George Ntalima (Ofisa Usafirishaji), Sabina Raymond (Mkurugenzi wa Sheria) na Xavery Kayombo.