Mwenyekiti wa Kijiji cha Simike Kata ya Lufingo wilayani Rungwe,  Efram Kapondany’a amechapwa bakora mbele ya mkutano wa hadhara  baada ya kuwasilisha Sh 10,000 tu  akidai ndiyo mapato ya mwaka ya masoko na magulio ya kijiji.
Inaelezwa kuwa  mwenyekiti huyo alikuwa amegoma kuwasomea  wanakijiji mapato na matumizi ya kijiji kwa zaidi ya mwaka mmoja, hali iliyowakasirisha wananchi hao na kuamua kumcharaza viboko mkutanoni.
Kwa mujibu wa wananchi hao,  Mwenyekiti huyo na Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Babelina Mlaghala walichakachua mali za kijiji pia Kupiga chenga kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji hali iliyosababisha wachukue hatua madhubuti ya  kumcharaza bakora mwenyekiti huyo kama fundisho.