NA ADAMU MKWEPU, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema kwamba hautabadili msimamo wake wa kugomea mamilioni ya fedha za udhamini za kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Ligi Kuu Tanzania Bara, zilizotolewa na Kampuni ya Azam Media msimu wa 2016/17.
Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya Azam Media kuongeza muda wa udhamini kwa miaka mitano ya kurusha matangazo ya ligi hiyo wenye thamani ya Sh bilioni 23 huku kila klabu ikitarajia kupokea Sh milioni 126 katika vipindi vitatu, ambapo timu zitapewa Sh milioni 42 katika robo ya kwanza.
Awali msimu uliopita 2015/16, Yanga iligomea fedha hizo za Azam Media wakati huo ikiwa imedhamini ligi hiyo kwa miaka mitatu, mkataba wenye thamani ya Sh bilioni sita, huku klabu zikichukua Sh milioni 100 katika vipindi vitatu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Baraka Deusdedit, alisema kwamba licha ya suala hilo kuendelea kujadiliwa na uongozi wa klabu hiyo ili kulitolea tamko rasmi, lakini hakuna kitakachobadilika juu ya msimamo wao.
“Mwenyekiti wetu tayari alishawahi kulizungumzia jambo hili, alikuwa na sababu za msingi na hizo hazitabadilika.
“Gharama za uendeshaji zinabadilika kila siku, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lenyewe linaingia mkataba ambao katika miaka mitano hakuna mabadiliko yoyote yanayoleta tija kwa klabu,” alisema Deusdedit.
Katika hatua nyingine, Deusdedit alitangaza viingilio katika mchezo dhidi ya Medeama unaotarajiwa kuchezwa Julai 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo mashabiki watakaokaa jukwaa la kijani watalipa Sh 3,000, blue na orange Sh 5,000 huku VIP B na C watalipa Sh 10,000 wakati VIP A wao watalipa Sh 15,000.
Kwa upande wake Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema kwamba maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri, huku wakitarajia kuipokea timu ya Medeama leo saa 8:30 asubuhi, ikitokea nchini Ghana kwa usafiri wa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ).