31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga: Tutaendelea kuigomea Azam

YANGA

NA ADAMU MKWEPU, DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema kwamba hautabadili msimamo wake wa kugomea mamilioni ya fedha za udhamini za kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Ligi Kuu Tanzania Bara, zilizotolewa na Kampuni ya Azam Media msimu wa 2016/17.

Uamuzi huo umekuja siku chache baada ya Azam Media kuongeza muda wa udhamini kwa miaka mitano  ya kurusha matangazo ya ligi hiyo wenye thamani ya Sh bilioni 23 huku  kila klabu ikitarajia kupokea Sh milioni 126 katika vipindi vitatu, ambapo  timu zitapewa  Sh milioni 42 katika robo ya kwanza.

Awali msimu uliopita 2015/16,  Yanga iligomea fedha  hizo  za Azam Media wakati huo ikiwa  imedhamini ligi hiyo kwa miaka mitatu, mkataba wenye thamani ya Sh bilioni sita, huku  klabu zikichukua Sh milioni 100 katika vipindi vitatu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Baraka Deusdedit, alisema kwamba  licha ya suala hilo kuendelea kujadiliwa na uongozi wa klabu hiyo ili kulitolea tamko rasmi, lakini hakuna kitakachobadilika juu ya msimamo wao.

“Mwenyekiti wetu tayari alishawahi kulizungumzia jambo hili,  alikuwa na sababu za msingi na hizo hazitabadilika.

“Gharama za uendeshaji zinabadilika kila siku, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lenyewe linaingia mkataba ambao katika miaka mitano hakuna mabadiliko yoyote yanayoleta tija kwa klabu,”  alisema Deusdedit.

Katika hatua nyingine, Deusdedit alitangaza viingilio katika mchezo dhidi ya Medeama unaotarajiwa kuchezwa Julai 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo mashabiki watakaokaa jukwaa la kijani watalipa  Sh 3,000, blue na orange Sh 5,000 huku VIP B na C watalipa Sh 10,000 wakati VIP A wao watalipa Sh 15,000.

Kwa upande wake Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema kwamba maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri, huku wakitarajia kuipokea timu ya Medeama leo saa 8:30 asubuhi, ikitokea nchini Ghana kwa usafiri wa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles