NA JANETH MUSHI, ARUSHA
SERIKALI imeombwa ifanye mapitio ya sera na sheria zinazogusa maslahi ya wafugaji na wakulima kubaini maeneo yanayohitaji maboresho katika utekelezaji.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Magembe Makoye alisema hatua hiyo itachangia ukuaji wa mfumo wa uzalishaji mali, ustawi wa amani miongoni mwa makundi yote.
Alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki kwa niaba ya asasi 36 zisizo za kiserikali zinazotetea haki za wafugaji asili nchini, baada ya kumalizika mafunzo ya usalama na tathmini kwa watetezi wa haki za jamii za wafugaji.
Alisema sera hiyo itasaidia kusimamia haki, rasilimali ardhi na maendeleo ya sekta hiyo kwa vile sera iliyopo sasa haikidhi maslahi ya mfumo wa ufugaji wa asili, pamoja na elimu kwa wadau kutolewa kwa vyombo vinavyosimamia sheria juu ya haki za binadamu.
“Sekta ya mifugo ni miongoni mwa sekta zilizotekelezwa na Serikali hivyo tunaiomba serikali kwa kushirikiana na wadau kupitia sera hiyo na kuifanyia maboresho kupunguza baadhi ya changamoto zinazotokea ikiwamo migogoro kati ya wakulima na wafugaji,” alisema Makoye.
Aliiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kutenga maeneo ya malisho kwa ajili ya wafugaji waweze kufanya shughuli zao bila kuingiliwa na wakulima au wawekezaji.
Kuhusu vyanzo vya migogoro baina ya wakulima na wafugaji, alisema kuwa migogoro hiyo imekuwa ikichangiwa na wafugaji kutokuwa na haki miliki za ardhi na kutokuheshimiwa mipango halali ya matumizi bora ya ardhi.
Naye Wakili Benedict Ishabakaki kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), alisema matukio ya unyanyaswaji wa wafugaji na watetezi wa wafugaji yakiendelea, wataenda mahakamani kufungua kesi za katiba.
“Matukio yakizidi kuendelea kutokea tutaenda mahakamani kufungua kesi za katiba kwa sababu ya matatizo mengi yanayoendelea ya unyang’anyi wa ardhi na manyanyaso kwa watetezi wa haki za wafugaji,” alisema.
Mratibu wa THRDC, Onesmo ole Ngurumwa, alisema mafunzo hayo yalikutanisha wadau kutoka mashirika na taasisi zinazotetea wafugaji na vyama vya wafugaji kutoka maeneo yote nchini.
Alisema lengo ni kuwawekea watetezi hao mazingira mazuri ya usalama wanapokuwa kazini ikizingatiwa wengi wao wamekuwa hatarini wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao.