NA BENJAMIN MASESE, NZEGA
MWILI wa Ismail Bashe ambaye alikuwa miongoni mwa abiria waliokuwamo kwenye basi la Kampuni ya City Boy lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Kahama, umezikwa juzi nyumbani kwao Nzega mkoani Tabora.
Ismail ambaye alikuwa na ndugu zake wawili alikutwa na mauti Julai 4, mwaka huu katika Kijiji cha Maweni Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, baada ya mabasi mawili ya kampuni hiyo kugongana uso kwa uso.
Basi moja lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Kahama na jingine kutoka Kahama kwenda Dar es Salaam.
Inaelezwa kuwa madereva wa mabasi hayo walikuwa na mtindo wa kusalimiana kwa kupishana kushoto na kulia, lakini siku hiyo mmoja wao alishindwa kurudi upande wake mapema na hivyo kusababisha yagongane uso kwa uso.
Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 30 papo hapo na wengine zaidi ya 72 kujeruhiwa.
Mwili wa Ismail ambaye ni mdogo wake Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) ambaye pia ni Ofisa Mkuu Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ulisafirishwa kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma hadi Nzega na kuzikwa katika makaburi ya Waislamu.
Maziko hayo yalihudhuriwa na mamia ya waombolezaji wakiwamo viongozi wa Serikali na wabunge.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Hussein Bashe, alisema wamepata pigo kubwa katika familia yao kutokana na kumpoteza ghafla Ismail ambaye alikuwa na ndugu wengine wawili akiwamo mtoto mdogo.
Hao walipata majeraha na wanaendelea kupatiwa matibabu huku hali ya mtoto ikiwa mbaya kwa vile alikuwa hajazinduka.
“Msiba huu ni mkubwa katika familia yetu, lakini kutokana na mipango ya Mwenyezi Mungu sisi binadamu hatuwezi kuzuia.
“Ismail alikuwa anatoka Dar es Salaam akiwa na ndugu wengine wawili akiwamo mtoto wa dada ambaye hali yake ni mbaya sana mpaka sasa yupo Dodoma anaendelea na matibabu lakini hajazinduka.
“Marehemu alikuwa anakuja Nzega kumsalimia baba na kusherehekea Sikukuu ya Idd El Fitri, malengo yake hayakuweza kutimia kutokana na ajali hii.
“Kwa niaba ya familia tunapenda kuishukuru Ofisi ya Bunge kwa msaada wao mkubwa wa kushirikiana na mimi hadi kuusafirisha mwili hadi hapa nyumbani.
“Pia tunawashukuru madaktari wa Manyoni, Singida na Dodoma kwa jinsi walivyojitoa kutusaidia, bila kuwasahau polisi na wananchi mlivyoshirikiana na familia hadi tunamfikisha marehemu hapa nyumbani pamoja na michango yao,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngudula, alisema wamesikitishwa na jinsi ajali ilivyotokea na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30 na kuwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri na madereva kuzingatia sheria za barabarani.
Alisema kutokana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuguswa na msiba huo inaungana na familia katika kipindi hiki kigumu na kutoa Sh 420,000 kama rambirambi yao.
Mwakilishi wa wabunge wa Mkoa wa Tabora, Mussa Ntimizi, alikabidhi rambirambi ya Sh milioni 1.3.