NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amesema Rais wa Rwanda, Paul Kagame ni rafiki yake pia ni mmoja wa watu wanaomshauri mambo mbalimbali kuhusu maendeleo na jinsi ya kukuza uchumi wa Tanzania.
Magufuli ameutaja urafiki huo wakati uhusiano wa mtangulizi wake, Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Kagame ulizorota mwaka 2013 pale Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa (Monusco) vilipowachakaza waasi wa Kikundi cha M23 waliotuhumiwa kufanya mauaji, ubakaji na uporaji katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa madai ya kufadhiliwa na Serikali ya Rwanda.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam jana, Magufuli ambaye ziara yake ya kwanza nje ya nchi aliifanya mwanzoni mwa Aprili, mwaka huu alipokwenda nchini Rwanda baada ya kuchaguliwa kuwa rais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, alisema hata wazo la kununua ndege za Serikali kwa bei nafuu alipewa na Kagame.
Akimkaribisha Ikulu ya Dar es Salaam, Kagame aliyewasili nchini jana kwa mwaliko maalumu wa ufunguzi wa Maonyesho ya 40 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Magufuli, alisema ndege hizo zitawasili nchini Septemba, mwaka huu.
Pia alisema Kagame alimpa mbinu za kuhakikisha anapata ndege na katika hatua za awali alimpatia wataalamu wa kumshauri walioongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Rwanda.
“Nilipewa akili na rais hapa (Kagame), alinipa namna nzuri ya kupata ndege, nilipomwambia alituma wataalamu na walipokuja hapa akanipa Waswahili wanasema desa (maelezo yenye mbinu mbalimbali) nikaelewa,” alisema.
Magufuli alisema baada ya kupata maelezo hayo alimtuma Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kwa ajili ya kufanya mawasiliano na kampuni husika.
“Hadi sasa mambo yanaenda vizuri na negotiation (maelewano) ikienda vizuri kwenye mwezi wa tisa (Septemba) kabla haujaisha tutakuwa tumeshapata ndege mbili, ujanja huo nilifundishwa na rafiki yangu Kagame na baadaye tutaendelea hadi kwenye air bus na kadhalika,” alisema.
Pia alisema ndege hizo mpya aina ya Q400 zitatoka nchini Canada katika Kampuni ya Bombardier na zitasimamiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Kuhusu utaratibu wa kukusanya mapato katika kituo kimoja unaotumika nchini Rwanda kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Magufuli alisema nao utaanza kutumika hapa nchini.
“Ameniambia Rwanda wameendelea katika masuala ya ICT (Tehama), wanakuwa na kituo kimoja kwa ajili ya kukusanya kodi, sisi kila mtu anakusanya kodi na programu (utaratibu) wake ukienda huku Max Malipo zile programu wanazi-control (kuziendesha) wao na si sisi, nimeshatoa maelekezo lazima kuwa na kitu kimoja cha kurekedi mapato ya Serikali,” alisema.
Magufuli aliendelea kusema kuwa Kagame amekubali kutoa wataalamu wa Tehama ili watoe mafunzo kwa watendaji wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) kwa lengo la kuhakikisha kila fedha inayokusanywa na kuingia inaonekana katika mtandao.
“Njia hii itasaidia kudhibiti mapato tofauti na utaratibu unaofanywa na kila mtu anakuja na programu yake, ameniahidi wataalamu wa ICT kutoka Rwanda wapo tayari kutusaidia, tuna mambo mengi ya kujifunza kutoka Rwanda,” alisema.
Pia alisema Tanzania kama ilivyo Rwanda ina jukumu kubwa la kujenga uchumi na kwa sasa asilimia 70 ya bidhaa za Rwanda zinapita katika Bandari ya Dar es Salaam inayosimamiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) licha ya kuwepo na matatizo madogo madogo ikiwemo urasimu na rushwa yanayowapoteza muda wafanyabiashara.
Alisema vikwazo vingine vilivyokuwa vikiwapotezea muda wafanyabiashara ni kitendo cha kusimamishwa barabarani kila kituo jambo linalosababisha usumbufu lakini kwa sasa ukaguzi unafanyika katika vituo vitatu.
Mbali na hilo, pia alisema katika mazungumzo yake ya jana na Kagame pia wamekubaliana kufungua ofisi ya TPA jijini Kigali ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara wanaotumia Bandari ya Dar es Salaam.
“Tumeamua TPA ifungue ofisi Kigali nchini Rwanda ili wafanyabiashara badala ya kuwa wanakuja na nyaraka Dar es Salaam na kuongeza gharama sasa watakuwa wanaanzia Kigali,” alisema.
Magufuli alisema Tanzania imeamua kutoa eneo maalumu kwa ajili ya Kituo cha Bandari Kavu (ICD) kwa ajili ya mizigo inayoenda nchini Rwanda ili kupunguza urasimu.
Kuhusu miradi ya maendeleo, Magufuli, alisema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga Sh trilioni moja kwa lengo la kujenga reli mpya ya kisasa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam kwenda Kigali kupitia Lusaka, Zambia.
“Nilikuwa namtania leo (jana) ni siku ya Uhuru wa Rwanda kwa maana nyingine amekuja kuanzisha uhuru mwingine mpya Tanzania wa biashara ndiyo maana nakushukuru na tutaendelea kushirikiana katika kukuza uchumi wa nchi zetu na kwa pamoja tutafika,” alisema.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Kagame, aliyewahi kunukuliwa siku za nyuma kuwa angeendesha uchumi wa nchi kutokana na mapato ya Bandari ya Dar es Salaam kama angeisimamia, alisema nchi yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania.
“Namwahidi kaka yangu Magufuli tutaendelea kusimama imara katika ushirikiano na kutengeneza fursa nzuri kwa nchi zote mbili na wananchi kwa ujumla,” alisema Kagame.
Akizungumza wakati akizindua Maonyesho ya Sabasaba, Kagame, alisema katika maonyesho hayo kampuni 15 zimeshiriki kutoka Rwanda lengo likiwa ni kujenga uhusiano wa kibiashara na kampuni za Tanzania ili ziweze kuendelea na kubadilishana bidhaa kwa kuuziana.
“Kuna kampuni 15 za Rwanda zimekuja kuona fursa zilizopo na kuanzisha uhusiano wa kibiashara na wafanyabiashara wa Tanzania na Serikali hizi mbili zitahakikisha zinaimarisha miundombinu inayotuunganisha na kuondoa vikwazo vya kibiashara,” alisema Kagame.
Pia alisema Watanzania wamebarikiwa nchi nzuri yenye rasilimali za kutosha na ina watu wenye vipaji vinavyosaidia kuwa na maendeleo makubwa.
MAGUFULI AOMBEWA DUA
Baada ya kufungua maonyesho hayo, marais hao walitembelea baadhi ya mabanda yaliyopo katika Viwanja vya Sabasaba na wakati Magufuli anapanda gari lake baada ya Kagame kuondoka uwanjani hapo aliibuka kijana mmoja na kuanza kupiga kelele za kumwombea dua.
“Rais Magufuli Mungu akusaidie na akubariki rais wetu,” ilisikika sauti ya kijana huyo.
Katika hali ya kushangaza, Magufuli, aliposikia dua hiyo aliacha kupanda gari na kuomba kijana huyo aletwe karibu yake ndipo akakaguliwa na watu wa usalama na kuruhusiwa kuonana naye.
Kijana huyo alianza kwa kupiga picha na Magufuli na baada ya hapo akajitambulisha kwa jina la Abdallah Ramadhani na kuanza kumwombea dua.
“Rais wetu Mungu akujalie baraka, akupe afya uendelee kuwatumikia Watanzania na kama kuna wabaya wako Mungu akawalaani,” aliomba kijana huyo na kuagana na Magufuli huku akifurahi.
Imeandikwa na Aziza Masoud, Jonas Mushi na Christina Gauluhanga.