24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge lawaliza wabunge CCM

NA MWANDISHI WETU

WABUNGE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameilalamikia Ofisi ya Bunge kuwa inatekeleza vitendo vya hujuma dhidi yao wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kibunge.

Wamesema wamebaini uwepo wa baadhi ya watumishi wa Bunge wanaokwamisha utekelezaji wa majukumu yao ya kuishauri na kuisimamia Serikali kwa kuwazimia vipaza sauti wanapokuwa wakichangia mijadala mbalimbali ya kibunge pamoja na kuvujisha mawasiliano ya maandishi baina ya wabunge wa CCM.

Wakizungumza na MTANZANIA Jumamosi, wabunge hao walisema wamebaini kuwepo kikundi cha watumishi wa Bunge ambao ni mawakala wa kambi ya upinzani wanaotekeleza mkakati wa kuwahujumu wabunge wa CCM.

Mbunge wa kwanza kueleza kuhusu kuwepo kwa hujuma hizo ni Ally Kessy wa Nkasi Kaskazini ambaye katika mahojiano yake na gazeti hili alisema hujuma zinazofanywa wa watumishi wa Bunge dhidi ya wabunge wa CCM zimekwishafahamika na zilijadiliwa kwa kina katika kikao cha wabunge wa chama hicho kilichofanyika mapema mwezi uliopita kwenye ukumbi wa White House, mjini Dodoma.

Kessy alimtaja mmoja wa watumishi hao aliyedai kuwa ndiye kiongozi wa hujuma hizo (jina lake tunalihifadhi kwa sasa) na kwamba mapema mwezi uliopita alimzimia kipaza sauti Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, wakati akichangia bungeni.

“Kuna mkakati ndiyo wa kuhujumu wabunge wa CCM unaotekelezwa na baadhi ya makatibu wa mezani wa Bunge, kuna huyu (anamtaja jina) alimzimia kipaza sauti Lusinde. Siku hiyo bungeni ilikuwa shughuli na tumeshalalamika kwa uongozi wa Bunge lakini wanalindana kwa sababu mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Hili jambo liko wazi, tulilizungumza hata kwenye kikao chetu cha wabunge wa CCM kwa sababu kweli linatuumiza na sasa tunalia, muulize Lusinde akwambie au nikupe namba yake,” alisema Kessy.

Alipoulizwa Lusinde kuhusu jambo hilo alikiri kuwa ni kweli na kueleza kuwa anashangaa licha ya kufikisha malalamiko kwa uongozi wa Bunge uko kimya.

“Hawa watu wa Bunge wameamua kutuhujumu, tena wanatuhujumu kwa namna nyingi tu lakini ambayo tumeithibitisha ni kuzima vipaza sauti hasa tunapoishughulikia Serikali, mimi siku hiyo mapema mwezi huu nilipewa nafasi ya kuchangia lakini ajabu baada ya dakika tano katibu wa mezani akanizimia kipaza sauti.

“Bunge likachachamaa kwa sababu wabunge wanajua muda wa mbunge kuchangia hadi mawaziri wakaja juu kwa taharuki wakitaka niruhusiwe kutoa mchango wangu lakini yule katibu wa mezani akagoma,” alisema Lusinde.

Alipoulizwa hatua alizochukua baada ya tukio hilo alisema alifikisha malalamiko yake kwenye kikao cha wabunge wa CCM na kwamba tayari amekwishaandika barua ya malalamiko kwa Kamati ya Uongozi ya Bunge lakini hajajibiwa.

“Hili suala ni kubwa si dogo kama mnavyofikiria, muda si mrefu mtaona tu kwa sababu na sisi tunajipanga kushughulika. Mimi nimekwishaandika barua ya malalamiko kwenye kamati ya uongozi na wao ndio wanajua wabunge wangapi wamekwishalalamika kwa sababu mimi nilikwenda mwenyewe kuangalia muda niliotumia nikakuta ni dakika tano tu badala ya kumi. Sasa tunasubiri majibu ya Ofisi ya Bunge halafu mambo mengine yatafuata,” alisema Lusinde.

Mwingine aliyezungumzia suala hilo ni mmoja wa mawaziri vijana ambaye pia alikuwa mbunge katika Bunge 10 lakini aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema tuhuma za kuwepo hujuma dhidi ya wabunge ni za kweli na kwamba yeye mwenyewe amekwishazimiwa kipaza sauti wakati akichangia kabla ya muda wake kumalizika.

“Ni kweli kuna tatizo, mimi mwenyewe nimekwishazimiwa kipaza sauti kabla ya muda wangu kumalizika na nilikwishamuita mtumishi mmoja anayefanya hivyo nikamuonya kuhusu hiyo tabia yake kwa sababu anatuhumiwa kutumiwa na wapinzani,” alisema Waziri huyo.

Awali Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza kuwepo kwa hujuma dhidi ya wabunge wa CCM zinazofanywa na watumishi wa Bunge kwa kuwazimia vipaza sauti wanapochangia mijadala ya Bunge.

Akizungumzia suala hilo, mkuu wa kitengo cha habari, elimu na mawasiliano, Ofisi ya Bunge, Owen Mwandumbya, alisema hayuko katika nafasi nzuri ya kulizungumzia kwa undani suala hilo mpaka litakapofikishwa rasmi ofisini kwake kwa ajili ya kulitolea taarifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles