BUENOS AIRES, ARGENTINA
RAIS wa nchini Argentina, Mauricio Macri, ameomba kukutana na mshambuliaji wa timu ya Taifa hilo na klabu ya Barcelona, Lionel Messi, kwa ajili ya kujadili juu ya kuendelea kuitumikia.
Messi alitangaza kujiuzulu kucheza katika timu hiyo ya Taifa mara baada ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Copa America mwanzoni mwa wiki hii dhidi ya Chile, ambapo Argentina ilipokea kichapo cha mabao 4-2 kwa mikwaju ya penalti.
Kauli hiyo ya kutangaza kustaafu imewashtua wengi duniani kote, hivyo rais huyo alimpigia simu mchezaji huyo na kumtaka asiyasikilize maneno ya watu kwa kuwa taifa bado linamhitaji.
Hata hivyo, rais huyo amedai kwamba anatarajia kukutana na mchezaji huyo wiki ijayo kwa ajili ya kujadili suala hilo.
“Ukweli ni kwamba tumepata zawadi kutoka kwa Mungu, nchi yetu kuwa na mchezaji bora duniani, nashangaa kuona watu wakizungumza mengi kwa mchezaji huyo kushindwa kuipa ubingwa timu ya taifa, ukweli utabaki kwamba tunajivunia kile ambacho amekifanya, kuonesha uwezo wa hali ya juu.
“Ninahitaji uwepo wake katika timu ya taifa na ninatarajia kukutana naye wiki ijayo kwa ajili ya kuzungumza juu ya jambo hilo,” alisema Macri.
Hata hivyo, mashabiki wamemwandika barua mchezaji huyo na kumtaka afute kauli yake kwa kuwa bado wanamhitaji, baadhi ya mashabiki walijitokeza mjini Buenos Aires ilipo sanamu yake kwa ajili ya kuonesha upendo kwake.