Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MAHAKAMA Ya Hakimu Mkazi Kisutu imempandisha kizimbani, Leornard Kyaruzi kwa mashitaka mawili ya kumtukana na kumdhalilisha Rais John Magufuli.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu, Magreth Bankika, Wakili wa serikali, Simon Wankyo alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa kutumia simu ya mkononi kwenye mtandao wa jamii wa’ Whatsapp’.
Alidai kuwa Juni 2, 2016 kwenye mtaa wa Tanzanite Tower barabara ya Bagamoyo Dar es Salaam, mshtakiwa alitumia simu ya mkononi na kuandika ujumbe wa maneno.
Alidai ujumbe huo ulikuwa unasomeka: “Hivi huyu Pombe ni kwamba hana washauri? Hashauriki? au ni zuzu! Bwege huyu jamaa, he doesn’t consider the law in place before opening his mouth! Au na yeye anaumwa ugonjwa wa Mnyika?”
Mwendesha mashitaka alidai kuwa shtaka la pili la mshtakiwa huyo ni kusambaza ujumbe huo wa kumdhalilisha kiongozi huyo kwenye mtandao huo.
Alisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo kuwapa siku 28 waweze kufanya upelelezi wa kina ikiwa ni pamoja na kuangalia maeneo ambayo yanahitajika zaidi kwenye kesi hiyo.
Hakimu Bankika alimtaka mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh milioni moja.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashitaka na kutolewa nje dhamana baada ya kukidhi masharti ya dhamana.
Hakimu Bankika aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 18 mwaka huu itakapotajwa tena.