WAZIRI Mkuu wa zamani na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema kwa mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ametoa wito kwa jamii kuwasaidia watu wenye uhitaji.
Alitoa wito huo jana baada ya kutembelea vituo vitatu vya watoto yatima jijini Dar es Salaam na kutoa vyakula kwa ajili ya futari katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Vituo alivyovitembelea ni Makao ya Kulea Watoto Yatima na Wasio na Makazi Maalumu (CHAKUWAMA) cha Sinza Wilaya ya Kinondoni, Kituo cha Watoto Yatima cha UMRA Magomeni na Kituo cha Watoto Yatima cha Khayrat Kigogo.
Alitoa pia pongezi kwa waanzilishi wa vituo hivyo na kuwatia moyo kuendelea kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa vile kufanya hivyo ni kuisaidia jamii nzima.
Akiwa katika Kituo cha CHAKUWAMA, Lowassa alisema ataendelea kutoa ushirikiano katika kusaidia watoto wenye mahitaji huku akiwaasa wazingatie elimu na mafunzo ya dini zao.
“Tutaendelea kuwaunga mkono katika kuwalea watoto hawa na nitoe wito kwa jamii kuwasaidia watu wenye mahitaji kama watoto yatima ili tushirikiane kwa pamoja kuwalea kwa sababu ndiyo jamii yetu,” alisema Lowassa.
Akitoa shukrani kwa msaada huo, Mwanzilishi wa Kituo hicho, Saida Hassan, alisema kituo kilianza na watoto watano lakini sasa kina watoto 90 hivyo kufanya uhitaji kuwa mkubwa zaidi.
“Tunaomba viongozi wetu wafuate nyayo za Lowassa kuwakumbuka na kuwasaidia watu wenye uhitaji kama watoto hawa ambao wamezidi kuongezeka kadiri siku zinavyokwenda,” alisema Saida.
Akiwa katika kituo cha UMRA, Mlezi wake Rahma Kishumba, alisema aliipokea ziara ya Lowassa kwa furaha na kwamba ana amini kufika kwake kutakua chachu kwa viongozi wengine kuguswa na kuwasaidia watu wenye uhitaji.
Alisema kituo chake kina watoto 90, wasichana 44 na wavulana 46 na changamoto kubwa ni gharama za elimu kwa watoto hao.
“Nimepokea ziara ya Lowassa kwa furaha kubwa naomba aendelee na moyo huu kwa sababu Mungu ataendelea kumbariki,” alisema Rahma.
Kwenye kituo cha Khayrat, Lowassa alitoa pongezi kwa waanzilishi wa vituo vya watoto yatima na kuwataka waendelee na moyo huo na ataendelea kuwatembelea mara kwa mara.
“Napenda kuwapongeza sana kwa hatua mlizochukua za kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu si kwa sababu mna uwezo bali kwa sababu mna moyo wa kusaidia,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Nimeona niwatembelee na niwaletee watoto chakula kidogo kwa ajili ya futari, nawatakieni Ramadhani njema na Mungu apokee funga zenu.”
Mlezi wa Kituo cha Khayrat, Hadija Hussein alisema wanategemea sana misaada ya watu kwa sababu watoto hao hawana ndugu wala wazazi wa kuwasaidia.
“Hapa tuna watoto 64 ambao wanahitaji chakula, mavazi na elimu na wengine ni wadogo wanaohitaji uangalizi mkubwa kutoka kwa walezi,” alisema.
Akiwa katika kituo cha Khayrat, Lowassa aliombewa dua na watoto wawili ili Mungu amtunze siku zote za maisha yake na endelee na moyo wake mwema.
Katika hatua nyingine, Lowassa aliendelea kulaani serikali kutowasikiliza wapinzani na kwamba chama chao kinaendelea kulishughulikia suala la kukatazwa kufanya mikutano na makongamano ya siasa.
“Nasikitika sana serikali kukosa uvumilivu wa kuvisikiliza vyama vya upinzani lakini Mwenyekiti wangu, Freeman Mbowe anashirikiana na viongozi wengine kuhakikisha suala la kuzuiliwa mikutano ya hadhara linapata ufumbuzi,” alisema Lowassa.