*Philip Mangula awaangukia warudi bungeni
Kulwa Mzee, Dodoma na Grace Shitundu, Dar
WABUNGE wanaotoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamebadilisha mtindo wa kugomea vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk.Tulia Ackson kwa kufunga plasta midomo yao wakidai ni ishara ya kupinga unyanyasaji bungeni.
Wabunge hao wa Ukawa waliingia bungeni jana asubuhi na kutoka baada ya dua ya kuliombea Bunge iliyoongozwa na Naibu Spika, lakini tofauti na siku zote safari hii walikuwa wamefunga plasta midomo yao.
Kutokana na hali hiyo wabunge hao wamesema kuwa wamechukua uamuzi huo kwa kile walichodai kuyumba kwa kiti cha Spika na kutosikilizwa hoja zao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa katika viwanja vya Bunge, Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR Mageuzi), alisema Naibu Spika amekuwa akishiriki uchochezi wa hali ya juu kwa kunyamazia wabunge wa CCM, ambao kila wakati wamekuwa wakiwatukana na kumdhihaki Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe.
“Tunawahakikishia Watanzania tukio la leo (jana) la CCM kujaribu kutufunga midomo ili zidumu fikra za mtu mmoja John Magufuli (Rais) halitakubalika.
“Hata Mwalimu Nyerere (hayati Baba wa taifa) katika miaka ya 1980 alisema huwezi kusema zidumu fikra za mwenyekiti tu lazima ziwe sahihi.
“Hatutakubali mtu mmoja kusema ndiye mwenye akili kuliko wengine wote, Mwalimu alikataa dhana hiyo, leo hii katika karne hii ya demokrasia na kasi ya mabadiliko duniani, mtu mmoja tu atoe maagizo na muhimili mmoja wa Serikali kuhujumu na kupora mamlaka ya Bunge halafu tukae kimya, tunasema hatutakubali.
“Hii ni ishara ya kuonyesha hasira zetu, wakituzima midomo humu ndani hatutakubali, na tayari tumeanza, Alhamisi ya wiki iliyopita tumeanza kususia tukio la kushiriki futari aliyoandaa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa wabunge.
“Kitendo cha kususia tukio hilo la toba katika huu mwezi mtukufu wangejiuliza mara mbili, mara tatu, mara nne, siku zote meza ya maridhiano ndiyo inaleta suluhisho, tumejitahidi tuzungumze wao ndiyo wenye uongozi wameshindwa, wanataka kutawala kiimla sisi tunawaambia hapana, uwezo huo hawana.
“Wakituua sisi vizazi vingine vipo, wakimwaga damu zetu Watanzania wengine watajitokeza na kulilia damu yetu na hakuna dhambi mbaya kama wanavyofanya sasa hivi,” alisema Mbatia.
Waenda mbali zaidi
Habari zilizopatikana baadaye kutoka katika kikao cha wabunge wa Ukawa kilichofanyika katika Hoteli ya African Dream, iliyopo eneo la Area D, wabunge hao waliazimia kususa mawasiliano yote na wabunge wa CCM ndani na nje ya Bunge.
Katika maazimio hayo, Ukawa hawataingia kabisa bungeni na kwenye kantini ya Bunge kwa kipindi kilichobaki cha wiki mbili
“Leo tumefikia azimio kwamba hatutaingia bungeni wala kuingia katika kantini ya Bunge kwa muda wa wiki mbili.
“Tulisusia futari yao na sisi leo tumeandaa futari yetu Hoteli ya African Dream bila kuwaalika, hayo ni makubaliano ya wiki mbili, baada ya wiki mbili tutajua tumefikia uamuzi gani katika hatua za kutafuta kupata haki yetu,”alisema mmoja wa wabunge wa Ukawa ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa kuwa si msemaji wa kambi hiyo kwa sasa.
Wakati huo huo, Makamu Mwenyeketi wa CCM Taifa (Bara), Philip Mangula awangukia wabunge wa Kambi ya Upinzani na kuwaomba warudi bungeni, kwani michango yao inaumuhimu mkubwa hasa katika Bunge la Bajeti.
Mangula ametoa kauli hiyo baada ya hatua ya wabunge wa Ukawa kususia vikao vinavyoendeswa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson ikiwa ni kutekeleza azimio lao la kutokuwa na imani naye.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mangula alisema michango ya wapinzani ina umuhimu mkubwa na pia ni wachangiaji wazuri bungeni.
“Michango ya wabunge wa upinzani ina umuhimu mkubwa hasa katika mijadala ya kupitisha bajeti ya nchi ambayo pia inagusa katika majimbo yao.
“Kutoka ndani ya Bunge si njia ya kutatua tatizo kwa kuwa ndani ya vikao hivyo ndipo zinapojadiliwa changamoto za majimbo yao ambayo yote yanatemegea bajeti kuu” alisema Mangula.
Alisema suala la kususia vikao na kwenda kuijadili bajeti nje ya Bunge hakutaweza kuleta manufaa kwa taifa na hata kwenye majimbo yao.
Akizungumzia suala la adhabu walizopewa wabunge saba wa upinzani, Mangula alisema kila jambo lina utaratibu na kanuni zake za kufuata.
“Hili ni suala la kufata kanuni na utaratibu unasemaje, ni sawa na mchezo wa mpira wa miguu ukicheza ‘rafu’ unatolew nje, lakini endapo kuna kanuni ambazo hazikufuatwa na kiti basi wabunge wenyewe wanajua taratibu zao za kufuata”Alisema .
Mangula alikua akizindua kitabu kilichoandikwa na Amos Siyantemi kinachoitwa. ‘Majipu ya Nchi Yetu Tushirikiane kuyatumbua’.
Hata hivyo Mangula alisema yote yanayotendwa sasa na Rais Dk. John Magufuli ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.
“Yanayofanywa na Rais Magufuli si ya kwake bali ni utekelezaji wa ilani ya CCM ambayo ni lazima yashughulikiwe ndani ya miaka mitano” alisema.
Alisema katika miaka mitano CCM ilidhamiria kuendelea kuondoa umaskini, kutatua tatizo la ajira, vita dhidi ya rushwa pamoja na kupambana na wabadhirifu na mafisadi.
Naye Mwandishi wa kitabu hicho Siyantemi alisema maudhui ya kitabu hicho yanachochea moyo wa uzalendo na uwajibikaji kwa watendaji, viongozi na wananchi kwa ujumla.
Alisema Serikali ya awamu ya tano imeonyesha dhamira ya dhati ya kujenga Tanzania mpya ikilinganishwa na awamu iliyopita.
“Kuna tofauti kubwa ya utendaji wa awamu ya Tano hasa katika kiwango cha miiko na maadili, ukusanyaji wa mapato, udhibiti wa matumizi yasiyo na lazima na pia umakini wa watendaji wanaoteuliwa katika awamu hii”, alisema Siyantemi.