20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mapya yaibuka ugonjwa wa ajabu Dodoma

nchaloNA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

MAPYA yameibuka kuhusu ugonjwa wa ajabu unaodaiwa kuingia katika wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma, MTANZANIA limebaini.

Hali hiyo imejitokeza, baada ya baba wa familia iliyolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kutokana na kula nyama ya ng’ombe iliyohisiwa kuwa na sumu kuishangaa Serikali kuhusu kile kinachoelezwa kuwa ni ugonjwa wa ajabu.

Wakati Serikali ikitoa taarifa kuwa idadi ya watu waliogua ikifikia 21 na wengine saba wakifariki dunia kutokana na ugonjwa huo ambao chanzo chake hakijajulikana, baba huyo wa familia amesema ugonjwa unaotajwa kuwa ni wa ajabu haupo na kuhusisha tukio hilo na wivu wa kimapenzi.

Katika tukio hilo lililotokea hivi karibuni katika Kijiji cha Mwaikisabe, Wilaya ya Chemba familia ya watu tisa ilikula nyama ya ng’ombe inayohisiwa kuwa na sumu ambapo watoto watatu wa familia moja walifariki dunia.

Akizungumza na MTANZANIA akiwa katika wodi namba 12 hospitalini hapo baba wa familia hiyo, Salum Nchalo, alimtuhumu mke wake mmoja kuwa ndiye aliyeweka sumu hiyo kwenye nyama kwa lengo la kumkomoa mke mwenzake.

Akisimulia mkasa huo akiwa wodini, Nchalo alisema katika maisha yake alifanikiwa kuwa na wake wanne, lakini baadhi yao aliwaacha na hivyo kubaki na wake wawili.

“Miongoni mwa wake hao, namhisi mke wangu (akamtaja jina) ndiye aliyeweka sumu katika nyama hiyo kwa sababu nilikuwa nimemkataza kukamua maziwa na jukumu hilo kuwapa watoto wa mke mdogo.

“Pale kwangu nina ng’ombe 12 ambao kati ya hao watatu ni wa mke mkubwa ambao nilimpa wakati nilipotaka kumuoa,” alisema.

Alisema awali jukumu la kukamua maziwa lilikuwa la mke mkubwa, lakini baada ya kuona watoto wa mke mdogo, wamekuwa wakubwa aliona jukumu la kukamua awaachie watoto hao wa mke mdogo hali ambayo iliharibu hali ya hewa kutokana na mke mkubwa kukasirika.

Alisema mke mkubwa alichukia kupita kiasi kutokana na jukumu la kukamua kuwapa watoto wa mke mdogo, hivyo alipokuwa akipelekewa maziwa kila siku alikuwa akiyakataa.

“Huu ni wivu wa kwanini watoto wa mke mdogo washike jukumu la kukamua maziwa. Nakwambia huu ni mwezi wa Ramadhan mke wangu mkubwa anahusika kutokana na wivu wa kwanini mke mdogo ana watoto wengi wa kiume na mimi nimekuwa karibu kwa mke mdogo kuliko yeye.

“Mke mdogo amezaa watoto nane tena wengi wakiwa wakiume tena ana mapacha mara mbili ambao ni pamoja na wale waliokufa wakati yeye watoto wake saba wote wa kike.

“Kwa hiyo polisi na Serikali wakifuatilia kwa makini juu ya suala hilo, ufumbuzi utapatikana kwa sababu kuna mahali pa kuanzia, mimi nashangaa wanasema ugonjwa wa ajabu, hakuna kitu kama hicho tatizo ni hili wivu wa kimapenzi” alisema.

Nchalo alidai kuwa anahisi kuwa mke wake mkubwa ndio amewaua watoto wake kutokana na kuwa na wivu na hata kuhoji kila wakati kwa nini mke wake mdogo ana watoto wengi wa kiume jambo linalomfanya yeye kuwa karibu naye.

Nchalo alisema jambo linalomsikitisha ni pale mke wake mkubwa alipopata taarifa ya kufariki kwa watoto wa mke mwenzake alianza kucheza ngoma kwa kujipongeza.

Alisema baada ya nyama hiyo kugawanywa kutoka nyumba ya jirani, kwanza ilipitia kwa mke mkubwa ndio ikaja kwao na huko ilikaa zaidi ya saa sita.

“Ukimuuliza yule mjukuu mdogo ambaye alitumwa alete ile nyama anasema wakati anakuja nyumbani mke mkubwa alipomwona alimwambia apeleke ile nyama kwanza kwake kisha jioni ndio akaenda kuichukua na kuileta kwa mke mdogo kuna nini hapo?

“Jingine, kwanini kaya nyingine ziliwahi na yetu ikachelewa, kwanini ilipita kwa mke mkubwa kabla ya kuja kwetu hapo sina majibu nenda kijiji kwetu mfuate mke wangu mkubwa muulize’’alisema.

“Kama ni kweli nyama hiyo ilikuwa na ugonjwa vipi mbwa watatu pamoja na paka wamekufa mara baada ya kula ile nyama sasa hapo unasema kuna ugonjwa hapo? hiyo ni sumu’’ alisema.

Wakati huo huo, mke mdogo, (jina limehifadhiwa) alisema nyama iliyosababisha vifo hivyo ilikuwa kama kilo moja na kwamba aliipokea jioni na kuipika kesho yake.

“Nyama ile niliipokea jioni na ikalala mpaka asubuhi wakati nataka kwenda shambani nikamwambia mwanangu mdogo Arafa aibandike ili wenzake watakapokuja kutoka shule waweze kupata mboga lakini ndio imekuwa chanzo cha kupoteza wanangu,” alisema.

Juzi Serikali kupitia Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii, Jinsia Watoto na Wazee,Ummy Mwalimu, alisema wamechukua vipimo vya familia hiyo na wamepeleka  kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles