26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

NI BAJETI NGUMU

Pg 1Na Khamis Mkotya, Dodoma

WAZIRI wa Fedha, Uchumi na Mipango, Dk. Philip Mpango, jana aliwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambayo pamoja na mambo mengine inapendekeza kuongeza  ushuru wa vinywaji baridi,  maji ya juisi, vinywaji vikali, sigara   na   usajili wa magari.

Hata hivyo,  ushuru  wa bidhaa za  mafuta (petroli, dizeli na mafuta ya taa) hautaongezwa.

Dk. Mpango alisema Bajeti hiyo itakuwa ya Sh trilioni 29.539,   kati ya hizo Sh trilioni 11.820 (asilimia 40 ya bajeti)  zikiwa  zitaelekezwa  katika miradi ya maendeleo,

Waziripia  alitangaza kufuta misamaha ya kodi katika maduka ya vyombo vya ulinzi na usalama na badala yake imeweka utaratibu wa kulipa posho maalumu kwa askari.

 

Vinywaji

Dk. Mpango ambaye alisoma hotuba yake kwa takriban saa mbili,  alipendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147, ambako ushuru wa vinywaji baridi umeongezeka kutoka Sh 55 kwa lita hadi Sh 58 kwa lita.

“Ushuru wa bidhaa kwenye maji ya matunda (juisi) iliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa hapa nchini kutoka Sh 10 kwa lita hadi Sh 11 kwa lita.

“Ushuru wa bia inayotengenezwa kwa nafaka ya hapa nchini na ambayo haijaoteshwa (unmalted) mfano kibuku Sh 409 kwa lita hadi Sh 430 kwa lita.

“Ushuru wa bia nyingine kutoka Sh 694 kwa lita hadi Sh 729 kwa lita. Ushuru wa bia zisizo na kilevi ikijumuisha vinywaji vya kuongeza nguvu kutoka Sh 508 kwa lita hadi Sh 534 kwa lita.

“Ushuru wa mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu inayozalishwa nchini kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka Sh 192 kwa lita hadi Sh 202 kwa lita,” alisema.

Mafuta

Akizungumzia kodi na tozo kwenye bidhaa za mafuta , Dk. Mpango alisema: “Kwa muda mrefu bei ya mafuta (petroli, dizeli na mafuta ya taa) imekua ikishuka katika soko la dunia hali ambayo imesaidia kuleta unafuu wa gharama katika shughuli za uchumi hususan kwa wananchi masikini.

“Maana bei za mafuta haya zinagusa kila mtu, hivyo Serikali imeamua kuwa ushuru wa barabara, ushuru wa petroli na ushuru wa bidhaa kwenye mafuta ya petroli utabaki ilivyo sasa,” alisema.

Magari

Dk. Mpango pia alipendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Magari (kodi ya usajili na uhamisho wa umiliki), Sura 124 kama ifuatavyo:

“Kufanya marekebisho viwango vya usajili wa magari na pikipiki kutoka Sh 150,000 hadi Sh 250,000 kwa kila gari na kutoka Sh 45,000 hadi Sh 95,000 kwa kila pikipiki.

“Kupandisha ada ya usajili wa namba binafsi za magari kutoka Sh 5,000,000 hadi Sh 10,000,000  kila baada ya miaka mitatu ili kuhuisha viwango hivyo kulingana na thamani halisi ya fedha,” alisema.

 

Maduka ya jeshi

Alisema Serikali imefuta misamaha ya kodi katika maduka ya vyombo vya ulinzi na usalama na badala yake imeweka utaratibu wa kulipa posho maalumu kwa askari.

“Ili kuendelea kutoa huduma kwa majeshi hayo pasipo kupoteza mapato ya Serikali, napendekeza kuwapatia posho majeshi yetu   kuwawezesha kununua mahitaji yao wenyewe.

“Dhamira ya hatua hii ni kusitisha msamaha wa kodi kwa majeshi  kuondoa uvujaji mkubwa wa mapato.

“Utaratibu mpya unalenga kuhakikisha motisha unatolewa kwa walengwa yaani askari badala ya utaratibu wa sasa wajanja wachache wanaendelea kunufaika na misamaha hiyo,” alisema.

 

Wabunge walizwa

Waziri   alipendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332   kuondoa msamaha wa kodi ya mapato katika malipo ya kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano.

“Serikali imeamua kufanya hivi ili kujenga misingi ya usawa na haki katika utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili kulipa kodi,” alisema.

Wakati Dk. Mpango akisoma kipengele hicho wabunge wengi walishangilia kwa kugonga meza, lakini aliporejea kusoma kwa mara ya pili,    waliguna na kuzua minong’ono na kuondoa utulivu bungeni.

Katika kuhakikisha utulivu unapatikana Naibu Spika, Dk. Tuli Ackson  aliwataka wabunge kuwa watulivu.

“Waheshimiwa hamna sababu ya kuguna na kupiga kelele kuhusu kipengele hicho  kwa sababu  mtapata fursa ya kuijadili bajeti mwacheni waziri aendelee,” alisema.

Waziri, vilevile alipendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sura 399 Sheria ya Kodi ya Majengo  kuiwezesha mamlaka hiyo kukusanya kodi ya majengo, ambayo kwa sasa inakusanywa na halmashauri.

Dk. Mpango  alisema Bajeti hiyo yenye kaulimbiu ya ‘kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua fursa za ajira’, imejielekeza katika kujenga misingi ya kujitegemea zaidi badala ya kutegemea wahisani.

Alisema  Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuongeza na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kudhibiti upotevu wa mapato na kudhibiti misamaha ya kodi isiyokuwa na tija.

Bajeti   inalenga kutatua kero za wananchi zilizojitokeza wakati wa kampeni na katika kukabiliana na suala la rushwa na ufisadi nchini, zimetangwa Sh bilioni 2.5  kuwezesha uanzishwaji wa mahakama ya mafisadi.

Katika kudhibiti matumizi, alisema Serikali itahakikisha mikutano yote ikiwa ni pamoja na mikutano ya bodi, mafunzo na semina inatumia kumbi za Serikali na taasisi za umma.

“Kuendelea kufanya ununuzi wa magari kwa pamoja na bidhaa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupata unafuu wa bei,” alisema Dk. Mpango.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles