29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Upinzani Kenya kuadhibu wabunge wao wasioandamana Kenya

John MbadiNAIROBI, KENYA

MWENYEKITI wa Chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM), John Mbadi, amesema watawachukulia hatua za kinidhamu wabunge wanaokwepa kushiriki maandamano ya kushinikiza kuvunjwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Mbadi alisema chama chake kinapanga kuwaadhibu wabunge, madiwani na wanachama wote ambao hawatashiriki maandamano ya kuwalazimisha makamishna wa IEBC kung’atuka.

Alisisitiza kuwa akiwa mwenyekiti wa kitaifa wa ODM, ana mamlaka ya kuwachukulia hatua za kinidhamu wanachama wanaokaidi sera za chama hicho.

“Kama mwenyekiti wa chama, nina mamlaka na nguvu za kuadhibu wanachama wanaoenda kinyume na sera zetu na kuimarisha umoja kati ya maofisa na wanachama. Kwa sababu hiyo nitatumia madaraka niliyopewa,” alisema wakati wa ufunguzi wa ofisi za tawi la Kadogo la chama hicho juzi.

Mbunge huyo wa Suba pia aliwaonya wabunge wote wa ODM kuwa wasiposhiriki maandamano hayo, huenda wakatemwa wakati wa michujo ndani ya chama.

Aliwataka wafuasi wa ODM kuwakataa wanaoasi chama wakati wa uteuzi wa wagombea wa nyadhifa mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu ujao.

“Hatuwezi kuendelea na shinikizo za kutaka IEBC ivunjwe ikiwa baadhi ya wanachama wetu hawako nasi. Wafuasi wetu wanapaswa kuwakataa watu kama hao kwenye uteuzi ujao,” alisema Mbadi.

Hata hivyo, tofauti zimeibuka mjini Mombasa kuhusu maandamano hayo, ambapo viongozi wa Kiislamu wanasisitiza yasiendelee wakati wa mwezi wa Ramadhani.

Mwenyekiti wa Uwezo Fund eneo la Likoni, Salim Abdallah aliuhimiza muungano wa Cord kuheshimu mwito huo wa viongozi wa Kiislamu.

“Tunajua viongozi wa kisiasa hutekeleza mambo kwa sababu ya manufaa yao ya siasa zijazo za mwaka 2017, lakini ningeomba wakazi wa Mombasa waheshimu mwezi huu na waepuke zahama na polisi wakati Waislamu wanapoukaribisha mwezi huu wa Ramadhani,” alisema Abdallah almaarufu kwa jina la “Kuuza”.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kenya Muslim Yatima Foundation na ambaye pia ni katibu wa chama cha Cord upande wa mahusiano ya Waislamu, Sheikh Twaha Omar, alisema watashiriki maandamano ili kuonyesha kutoridhishwa na IEBC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles