23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

WB inapozineemesha kampuni zinazokwepa kodi Afrika

Port Lous, mji mkuu wa Mauritius, taifa ambalo asilimia 40 ya wateja wa Benki wa Dunia waliowekeza kusini mwa Jangwa la Sahara AfrikaMATAIFA na taasisi kubwa za fedha duniani mara nyingi hukutana na viongozi wa Afrika kujadili namna wanavyoweza kusaidia ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu kwa bara hilo.

Hilo linaenda sambamba na ukuaji wa uchumi katika miaka ya karibuni licha ya changamoto zilizopo sasa zinazotokana na kuleg lega kwa uchumi wa dunia.

Katika majadiliano hayo, mataifa makubwa au taasisi hizo husisitiza matumizi mazuri ya fedha wanazotoa iwe kama mikopo au misaada kutokana na ufisadi kulitafuna bara hili.

Hata hivyo, mataifa hayo makubwa na taasisi hizo za fedha wana mchango wao katika uendekezaji wa madudu yanayotokea Afrika linapokuja suala la utumiaji wa misaada au mikopo hiyo.

Namna ni nyingi inaweza kuwa kuruhusu fedha zilizopatikana kifisadi kuingia katika akaunti za mabenki yao au kuwezesha ukwepaji wa kodi kwa kujua au kutojua.

Mfano mzuri ni ripoti ya hivi karibuni, ambayo ndiyo makusudio ya makala haya inayozinyooshea kidole taasisi kubwa za fedha kwa kuchochea vitendo vya ukwepaji kodi.

Kwa mujibu wa Shirika la Misaada la Oxfam la Uingereza, kiwango kikubwa cha mikopo inayotolewa na Kitengo cha Utoaji Mikopo cha Benki ya Dunia- Afrika kinaenda kwa kampuni zinazoficha mali katika maficho ya wakwepa kodi.

Kwa mujibu wa Oxfam, asilimia 84 ya uwekezaji wa kitengo hicho-International Finance Corporation (IFC), katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika mwaka 2015 ulikwenda kwa kampuni ambazo utumiaji wake wa maeneo ya kuficha fedha ili kukwepa kulipa kodi, hauna uhusiano bayana na kazi yao na kuna kiwango cha chini cha uwazi.

Ikijibu ripoti hiyo, IFC ilisema uchambuzi wa Oxfam umevurugwa na kwamba katika visa vyote kitengo hicho huzitaka kampuni zinazoendesha miradi yake kuheshimu sheria zinazotumika, ikiwa ni pamoja na sheria kuhusu kodi.

Lakini kwa mujibu wa ripoti ya Oxfam, IFC iliwekeza zaidi ya dola bilioni 3.4 katika ukanda huo wa Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika mwaka 2015 na asilimia 75 ya kampuni 68 ilizozipatia mikopo zilikuwa zikitumia maeneo yanayotumiwa na wakwepa kodi.

“Kwa kuruhusu uwekezaji katika maeneo hayo kunazinyima nchi masikini mapato zinayohitaji kupambana na umasikini na kukosekana usawa,” alisema Nick Bryer, Mkuu wa Oxfam anayehusika na ukosefu wa usawa.

Lakini IFC imeendelea kudai Oxfam limetumia fikra zisizo sahihi kwamba kampuni zinazopatikana katika maeneo hayo bila shaka zilikuwa zikikwepa kodi.

“Ripoti hii inamaanisha kuwa mamlaka zote za nje au vituo vya fedha vya nje ni maeneo salama ya kodi, kwa kuwa tu ni nje, na kuwa uwekezaji katika biashara kubwa za kimataifa ni ukwepaji kodi,” alisema Frederick Jones, msemaji wa IFC, wakati alipozungumza na Mfuko wa Hisani wa Thomson Reuters.

“Kuna matumizi halali ya mifumo inayopatikana katika visiwa wanavyoita ‘pepo salama’. Matumizi sahihi ya vituo vya fedha katika maeneo hayo kunaweza kuongeza mtaji binafsi kwa ajili ya uwekezaji unaowasaidia watu masikini.”

Kwa mujibu wa Oxfam, eneo mashuhuri linalotumiwa na wateja wa kitengo cha benki ya dunia ni Mauritius, inayofahamika kwa kuziruhusu kampuni kuhamisha fedha kisiwani humo kabla kuzirejesha kama uwekezaji wa moja kwa moja, hali inayoruhusu faida kwa upande wa kodi.

Ilisema asilimia 40 ya wateja wa IFC waliowekeza kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika wana uhusiano na taifa hilo.

Ripoti hiyo inakuja baada ya kuchapishwa katika vyombo vya habari nyaraka zinazoihusu kampuni ya sheria ya Panama, Mossack Fonseca.

Nyaraka hizo za tangu miaka 40 iliyopita zilibainisha namna kampuni hiyo ilivyowezesha huduma za utakatishaji fedha, ukwepaji kodi na shughuli za kihalifu.

Nyaraka hizo zilizofichuliwa na taasisi 100 za habari za kichunguzi zinabainisha uwapo wa wanasiasa karibu 140 wakiwamo viongozi wakuu au wanafamilia wao, waliopo madarakani, waliostaafu au kufariki dunia wakihusika binafsi au kupitia taasisi, mashirika na kampuni zaidi ya 210,000.

Zaidi ya benki 500 na benki zake tanzu na matawi pia zimefanya kazi na Mossack Fonseca tangu miaka ya 1970 kuwasaidia wateja wao kusimamia kampuni hizo za nje.

Ni aina ya kampuni ambazo huanzishwa maalumu kutimiza malengo aina hiyo kwa matajiri na watu wenye nguvu wanaotawala duniani.

Shirika la Oxfam limesema ingawa IFC inaongoza katika sekta ya binafsi linapokuja suala la ufichuzi, taarifa kuhusu inakokwenda asilimia zaidi ya 50 ya ufadhili wake haziko wazi kwa umma kwa sababu ya madalali wajanja wanaozificha.

“Kitengo cha Benki ya Dunia hakitakiwi kujiingiza katika hatari ya kuzifadhili kampuni zinazokwepa kulipa kodi Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na ulimwenguni kote. Kinahitaji kuweka sheria kuhakikisha wateja wake wanaweza kuthibitisha wanalipa sehemu yao stahili ya kodi,” alisema Byer.

“Haina mantiki kwa kitengo cha benki ya dunia kutumia fedha kuziwezesha kampuni kuwekeza katika maendeleo huku kikifumbia macho ukweli kwamba kampuni hizi huenda zinadanganya nchi masikini na kuzinyima mapato ya kodi yanayohitajika kupambana na umasikini na kukosekana usawa,” amesema Susana Ruiz, mshauri wa masuala ya kodi wa Oxfam.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), nchi zinazoendelea hupoteza takriban dola bilioni 100 ya mapato yanayotokana na kodi kwa mwaka kwa sababu ya ukwepaji kodi wa kampuni.

Ripoti ya Oxfam imeitaka WB na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) kuimarisha na kurekebisha mifumo yao ya utoaji fedha kwa sekta binafsi ili kutoingia mtego wa kusaidia kampuni kukwepa kodi na kuzinufaisha kwa mgongo wa mataifa masikini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles