32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kilitech yazindua miradi kutoa ajira, kuondoa umaskini  

Vijana wakiwa kijiweniNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

KUTOKANA na hali ngumu ya maisha kiuchumi, wananchi wa vijijini wanaathirika zaidi kwa kukosa maji safi na salama, elimu bora na huduma nyingine muhimu za jamii, vitu ambavyo vinafanya maendeleo vijijini yasipatikane kwa urahisi.

Ingawa serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha mfumo wa elimu na kutoa huduma muhimu za jamii, lakini haiwezi kufanya kila kitu na kufanikiwa kutokana na ukosefu wa fedha na viongozi wanaowajibika.

Kwa kuzingatia hilo, baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali yameanza kusaidia kwa kuanzisha miradi ya maendeleo vijijini.

Kilimanjaro Technology Foundation (Kilitech) ni moja ya mashirika yasiyo ya kiserikali lililoamua kuelekeza nguvu zake vijijini kwa kuanzisha miradi ya maendeleo Mkoa wa Kilimanjaro.

Kilitech, ambalo ni shirika la Kimarekani, limeelekeza shughuli zake hasa kwenye changamoto zinazowakabili wananchi waishio vijijini. Limeingia ubia na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kuanzisha miradi ya biashara ili wananchi wa vijijini waweze kupata unafuu wa maisha.

Kilitech wamezindua miradi Kijiji cha Kyomu, Majengo, Kata ya Kahe Mashariki, Wilaya ya Moshi. Lengo ni kuinua hali ya maisha ya wanakijiji.

“Miradi yake ni pamoja na mashine ya kusaga mahindi, kituo cha mafunzo ya ufundi, ufugaji nyuki na useremala. Kuna miradi mingine pia ambayo imepangwa kutekelezwa hapo baadaye kama vile kuwa na huduma ya simu kwa gari, kwa ajili ya kuwafikia wananchi wengi zaidi na ufugaji wa kuku,” anasema Meneja Mradi wa Kilitech, Nashon Chacha, katika mahojiano yake na gazeti hili.

Mmoja wa wanakijiji wa Moshi, Jospeh Mosha, anasema miradi ya Kilitech itaboresha maisha yao kwa kuwasaidia vijana kupata ujuzi na kujiajiri wenyewe.

“Unajua kwamba vijana hawana ajira nchini na Rais Dk. John Magufuli amekuwa akisisitiza kwamba anataka kuona kila mtu akifanya kazi na si kukaa vijiweni.

“Kupitia miradi ya Kilitech ina maana vijana wataweza kupata ujuzi na maarifa na kuanzisha biashara zao kama vile ambavyo serikali imekuwa ikiviagiza vyuo vya elimu ya juu kufanya ili kukabiliana na tatizo la vijana kukosa ajira nchini,” anasema Mosha.

Anawaomba vijana wenzake kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo kwenye vijiji vyao na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla. Hivyo, aliupongeza uongozi wa Kilitech kwa kuzindua miradi kwenye kijiji chao ambako ilichelewa kufika.

Kwa mujibu wa Chacha, Kilitech wanafadhili na bado wanaendelea kufadhili miradi mingine kama vile kutoa elimu kwa wabeba mizigo, mradi ambao unalenga kuwafundisha lugha ya Kiingereza wakati ambao watalii si wengi ili kuwasaidia kuweza kuwasiliana vizuri na wateja wao.

Kilitech wametoa msaada pia wa vifaa maalum vya kutunza taarifa za kompyuta katika Chuo cha Teknolojia Moshi (MIT).

Pia wanawafadhili vijana kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu.

“Siyo hayo tu, Kilitech pia tunashirikiana na TAREO, shirika lisilo na kiserikali, kusaidia makundi mbalimbali kuboresha maisha yao.

“Makundi haya yanaundwa na wananchi wanaotambua kwamba hawawezi kufanya kazi kila mmoja peke yake na kufanikiwa, yametambua pia kwamba wanaye adui mmoja tu, ambaye ni umaskini na kwa kufanya kazi pamoja wanaweza kumshinda. Kilitech na TAREO wamaeamua kuleta tofauti kwenye maisha ya

Wana – Kilimanjaro kwa kuanza na Kijiji cha Kyomu,” anasema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Fulgence Mponji, anasema Kilitech ni msaada mkubwa katika Wilaya ya Moshi, hasa katika eneo ambako walikuwa wamezindua miradi yao.

Anasema taarifa alizonazo ni kwamba Kilitech wanawasaidia makundi ya vijana na wanawake wajasirimali, ambacho ni kitu kizuri.

Mwalimu kutoka shule ya Majengo, inayofadhiliwa na Kilitech na iliyoko Kata ya Kahe Mashariki Wilaya ya Moshi,  Sanura Sechonge, anasema shirika hili limekuwa likisaidia shule yao kupata kompyuta, vitabu na kulipa mishahara ya walimu.

Naye Diwani wa Kahe Mashariki, Kamili Mmbando, anasema Kilitech wameleta maendeleo katika kata yao na kuwasaidia wanakijiji kwa njia nyingi hivyo anaahidi kuendelea kushirikiana nao kwa karibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles